Mbinu za kibaolojia zimegundua uumbaji mpya wa binadamu baada ya kuchukua sehemu ya muunganiko wa mbegu ya kiume na yai la mwanamke ‘kiinitete’ hatimaye kuumba mtoto aliyekulia katika maabara.
Wanasayansi wanataja chembe hai hizo kuwa zinajulikana kama ‘Stem Cell’, ambazo hugawanyika na kuzidi kuzaliana. Wanaeleza kwamba chembehai hizo zinaweza kuzalisha binadamu wengine iwapo zitaachwa zizaliane kwa muda mfupi.
Hata hivyo wanabainisha kuwa chembehai hizo zitasaidia pia kutibu magonjwa kama ya kusahau pamoja na magonjwa mengine ya mfumo wa fahamu (Alzheimer desease).


Matokeo ya utafiti huo yanaibua uwezekano wa watoto hao kukulia maabara hali inayoelezwa kwamba itawaruhusu wanandoa wanaoshindwa kupata watoto kwa njia ya kawaida kuunda mtoto kupitia njia hii.
Ingawa tangu awali kiinitete cha binadamu kilikuwa kikipandikizwa, lakini hivi sasa kumekuwa na uwezekano wa kuchukua chanzo cha chembehai nyingine na kuunda mtoto mwingine. Timu hiyo ya wanasayansi kutoka nchini Marekani ilianza kwa kufanya utafiti wa dawa ya magonjwa ya kusahau na mengine ya mfumo wa fahamu, lakini ndani ya utafiti wao ndipo wakagundua kuwa chembehai hizo pia zinaweza kugemwa na kufanya upandikizaji wa mtoto.

Uwezo wa kuzalisha watoto
Mwanzilishi wa timu hiyo ya Human Genetics Alert Dk David King, anasema kuwa duania awali ilifanikiwa kupandikiza mbegu ya kiume na yai la kike, lakini kwa sasa ndani ya kiinitete hicho panaweza kuzalishwa watoto wengi watakaotoka katika mfumo huo.

Awali, mmoja wa watafiti hao Dk Shoukhrat Mitalipov alichukua mayai kutoka kwa mwanamke wa umri wa miaka 27 na kuondoa DNA, kisha baadaye aliweka mbegu za kiume na kukiacha kiini tete hicho kwa kuweka joto la umeme kwa muda wa siku sita, ambapo baada ya kiinitete hicho kutimiza siku sita alifanikiwa kuvuna chembehai hizo kutoka katika kiinitete.

Seli hizo zinazojulikana kama ‘master cells’ zina uwezo wa kugeuka katika kila aina ya seli kwenye mwili, zinaweza kutumika kama dawa maalumu ya kutibu magonjwa kadhaa mwilini na kuponya baadhi ya viungo katika mwili.

Dk Mitalipov aliyetumia miaka mingi katika kufikia mbinu hii anasema; “ugunduzi wa utafiti huu mpya wa kuzalisha seli zinazoweza kutibu magonjwa ya mfumo wa fahamu na ubongo, pia utasaidia kuunda watoto kwa njia ya upandikizaji. Chembehai nyingine zinaweza kutengeneza dawa maalumu ya kutibu magonjwa yanayoathiri mamilioni ya watu duniani, ambayo tutayaweka hadharani baada utafiti zaidi kukamilika.”

“Bado kuna kazi kubwa ya kufanyika ili kuendeleza usalama na ufanisi wa matibabu ya chembehai hii, tunaamini hii ni hatua muhimu katika kuendeleza chembehai zinazoweza kutumika kama dawa,” anaongeza Dk Mitalipov.

Anafafanua: “Matumizi ya yai na mbegu kutoka kwa watu wenye afya yalihakikishwa kuwa yana uwiano katika miili yao, hivyo ndivyo tulivyoweza kupata mafanikio na kuondoa haja ya dawa zenye
nguvu kumkandamiza mgonjwa kwa mfumo wa kinga.
Katika utafiti huu nimefanikiwa kuzalisha mtoto mmoja aliyetokana na chembehai za kimaabara zilizogemwa kutoka kwenye kiinitete na kutengeneza mtoto huyo aliyekulia katika maabara.”

Anasema pia chembehai hizo zinaweza kutumika kujifunza zaidi kuhusu magonjwa ya watu na kupata dawa itakayoweza kufanya kazi vizuri.

Wataalamu wa afya Dar

Mhadhiri na Mwenyekiti wa Idara ya Uzazi ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake kutoka Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki kilichopo jijini Dar es Salaam, Dk Monica Chiduo anasema kuwa kuna haja ya kufuatilia utafiti huo kwa kina kabla ya kutoa maelezo yoyote.

“Siwezi sema chochote utafiti huu ni wa hali ya juu na kwa kuwa bado sijapata maelezo ya kutosha kuhusu namna watafiti walivyofanya kazi, kwangu itakuwa ngumu kueleza chochote,”anasema Chiduo.
Hata hivyo Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Uzazi ,Dk Halifa Mkumbi anasema kwamba utafiti huo utasaidia kwa wengi wenye matatizo ya uzazi, licha ya kupata kinga zitakazoweza kutibu magonjwa mbalimbali.

“Utafiti huu upo kihisia zaidi, naweza kusema ni wa ndani kwani utafiti unafanyika kila siku lakini kupata wa namna hii ni nadra sana. Licha ya hivyo bado kuna maswali, iwapo imegundulika dawa ya kutibu magonjwa ya mfumo wa fahamu, nchi yetu ina matatizo hayo?,” anahoji DK Mkumbi na kuongeza;
“Kama tuna matatizo ya namna hiyo basi huo ni utafiti unaohitaji kufuatiliwa kwa kina ili kuweza kumaliza matatizo kama hayo. Kwa kawaida utafiti aliofanya mtu huwezi kuutengenezea hoja, kwa kifupi kuna changamoto nyingi.”

Wataalamu wa afya duniani

Profesa wa tiba kutoka University College London nchini Uingereza, Chris Mason anasema kuwa utafiti wa Dk Mitalipov kuhusu chembehai unaonekana kama ni mpango halisi.

“Ni vigumu mno mtu kufanya utafiti pasipo kupata jawabu la haraka, lakini Dk Mitalipov amevumilia kwa miaka mingi pasipo kuchoka hadi amefanikiwa kukamilisha utafiti huo utakaokuwa na faida kubwa duniani,” alisema Mason.

Dk Paul De Sousa kutoka Chuo Kikuu cha Ualimu na Utafiti Edinburgh kilichopo nchini Uingereza anasema: “Kuboresha uelewa wetu wa mayai ya wanawake kunaweza kusababisha tiba mpya kwa ajili ya utasa. Hata hivyo wanasayansi wengine walituonya kwamba utafiti wa sasa unatuletea binadamu kuzaliana kwa njia za upandikizaji ilhali kuna njia asilia,” alisema Sousa.
Mtaalamu wa Maadili ya Uzazi, Josephine Quintavalle kutoka nchini Marekani anasema: “Hoja ya utafiti huu siyo kuendeleza upandikizaji bali ni kutafuta njia mbadala ya wanandoa waliokosa watoto na walioshindwa kupandikiza pia, lakini ni namna ya kupata tiba mpya ya magonjwa ya mfumo wa fahamu.”

Utafiti mwingine

Mwaka 2004, Hwang Woo-suk kutoka Korea Kusini alidai kutengeneza kiinitete cha kwanza na kuondoa chembehai katika kiinitete hicho. Baadaye ilikuja kugundulika kwamba taarifa zake zilikuwa ni bandia na kushtakiwa mahakamani.