Kisarawe.
 Watu tisa, wawili kati yao wakiwa polisi wa Kituo cha Oysterbay, Dar es Salaam wamekamatwa wilayani Kisarawe, mkoani Pwani kwa tuhuma za kukutwa wakisafirisha meno 70 ya tembo (kilo 305) kinyume na sheria.
Meno hayo kwa hesabu za kawaida ni sawa na tembo 35, wameuawa na kwamba thamani yake ni zaidi ya Sh850 milioni.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei, alisema watuhumiwa hao walikamatwa Kisarawe usiku wa kuamkia jana na askari wa wanyamapori waliokuwa kwenye operesheni.
Matei alisema watuhumiwa walikamatwa kwenye kizuizi cha Kauzeni, Kata ya Vikumburu, Tarafa ya Chole na kwamba, walikuwa wakisafirisha meno hayo kwa kutumia gari aina ya Toyota Surf kwenda Dar es Salaam.
“Ni kweli wamekamatwa watu tisa, wawili wakiwa ni Polisi wa Oysterbay, nimepata hiyo taarifa na nimeshamtuma Ofisa Upelelezi Mkoa (RCO) kuwaleta Kibaha,” alisema Matei.

Kamanda Matei alitaja watuhumiwa kuwa ni mkazi wa Tandika Yombo, mkazi wa Kinondoni Studio, mkazi wa Tandika hewa, mkazi wa Mbagala Charambe na mkazi wa Chanika. Pia, polisi wawili wanaodaiwa wa Kituo cha Oysterbay.

Wakati polisi hao wakikamatwa, Idara ya Magereza imetangaza kuwafukuza askari wanne wanaodaiwa kukamatwa wakiwa wamepakia meno ya tembo Julai 23, mwaka huu.
Kamishna Jenerali wa Magereza, John Minja, aliwataja waliofukuzwa kuwa ni Mrakibu Msaidizi, Joseph Kimaro, Sajenti Ketto Ramadhan, Koplo Silyvester Dionice na Wada Richard Barick.

Minja alisema askari watatu waliohusika wamefukuzwa kwa kosa la kwenda kinyume na maadili ya Magereza, watafikishwa mahakamani baada ya polisi kukamilisha uchunguzi.

Alisema Mkuu wa Gereza la Kiteto, Mrakibu Ally Sauko, amevuliwa uongozi na kuhamishiwa Ofisi ya Mkuu wa Magereza Manyara, akisubiri uamuzi wa mamlaka.

ya Nidhamu,” alisema Minja.

Chanzo cha habari ni Gazeti la Mwananchi