Makabiliano makali yameibuka kati ya wanajeshi wa Mali na watu wanaoshukiwa kuwa waasi katika eneo la Kidal Kaskazini mwa Mali na kusababisha hofu kuwa ghasia huenda zikakithiri.
Waasi hao waliwashambulia wanajeshi waliokuwa wanalinda benki mjini humo na ambao waliwafyatulia riasi.Wenyeji walioshuhudia tukio hilo na maafisa ambao hawakutajwa, walisema kuwa waasi kutoka kundi la Tuareg ambao walisema wanapuuzilia mbali makubaliano ya amani waliyoafikia na serikali.

Mkataba wa amani uliofikiwa mwezi Juni, ulikuja baada ya zaidi ya mwaka mmoja wa mapigano ambao ulisababisha jeshi la Ufaransa kuingilia kati.
Majeshi hayo yangali yanashika doria Kaskazini mwa Mali na jeshi la Mali limerejea mjini Kidal katika hali isiyoeleweka.
Mji huo ulikuwa mikononi mwa waasi wa (MNLA) kwa miezi mingi.
Gavana wa eneo hilo Adama Kamissoko aliambia shirika la habari la AFP mjini Kidal kuwa walisikia milio mingi ya risasi, na kwamba wanajeshi wa Mali walilemewa na kuondoka sehemu hiyo ingawa alisema hangeweza kuwatambua wapiganaji hao.
Hapakuwa na taarifa zozote kuhusu majeruhi kwenye makabiliano hayo.
Vurugu za Jumapili ndizo za hivi punde kutokea katika eneo hilo. Mnamo Ijumaa wanajeshi wawili walijeruhiwa mjini Kidal wakati waliporushiwa guruneti.