Madereva wa pikipiki wamelaumiwa kwa kusababisha ajli nyingi za barabarani
Mamia ya wakaazi wa mji mkuu wa Liberia Monrovia, wamelazimika kwenda kazini kwa miguu baada ya sheria inayoharamisha bodaboda kuingia mjini humo kuanza kutumika.
Polisi waliweka vizuizi barabarani hasa katika maeneo muhimu ya kuingia mjini kuhakikisha huwa madereva wa pikipiki wanatii sheria hiyo.Hatua ya serikali inatokana na tuhuma dhidi ya madereva wa pikipiki hizo ambazo hutumiwa kwa huduma za Taxi, kwa kuziendesha ovyo na kusababisha ajali nyingi barabarani.
Pikipiki hizi ambazo humilikiwa na watu binafsi, hutumiwa sana na wasafiri wengi mjini Monrovia na pia katika miji mingi barani Afrika.
Baadhi ya madereva wa pikipiki hizo huwabeba hadi watu watano wakati wanaruhusiwa tu kuwabeba watu wawili.

Kwa mujibu wa taarifa ya poliisi, madereva wowote wa pikipiki hizo watakaopatikana mjini watatozwa faini ya dola miambili.
Mmoja wa madereva hao Daniel Howard alisema kuwa wameghadhabishwa mno na hatua ya serikali.
Mwandishi wa BBC mjini Monrovia, Jonathan Paye-Layleh anasema kuwa sio mara ya kwanza kwa maafisa wa serikali kujaribu kuzuia pikipiki hizo kuingia katikati mwa mji.
Mapema mwaka huu madereva wa Pikipiki hizo walizuiwa kuziendesha katika baadhi ya barabara za mji baada ya saa nne usiku.
Hata hivyo sheria hii ya sasa inasemekana kutatiza usafiri pakubwa mjini humo.