Mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya siku ya kimataifa ya Amani, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Mh. Seif Rashid akiwasili kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja kuhudhuria maadhimisho hayo na kupokelewa na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Albino Tanzania (TAS), Joseph Masasi (wa pili kulia), Kamishna wa Ustawi wa Jamii, Bw. Dunford Makala (katikati) na Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Tanzania , Bw. Ali Rajab (kulia) pamoja na viongozi wengine taasisi ya watu wenye ulemavu wa ngozi (Albinizim). (Picha zote na Zainul Mzige wa MOblog)
Na Mwandishi wetu
WAKATI Katibu Mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-moon anahimiza serikali duniani kutafuta chanzo cha kukosekana kwa amani na kuongezeka kwa watu wenye misimamo mikali, wasemaji katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa amani Duniani wameitaka serikali ya Tanzania kutupia macho makali mauaji ya albino nchini.
Akimwakilisha Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa katika adhimisho lililofanyika viwanja vya Mnazi mmoja leo Mratibu mkazi wa Umoja wa Mataifa na Mwakilishi mkazi wa UNDP nchini Alvaro Rodriguez, alisema ili kudumisha amani kuna mambo mengi yanatakiwa kufanyiwa kazi hasa kutambua chanzo cha migogoro inayosababisha msuguano mkubwa katika jamii na kukosekana kwa amani.
Alisema amani ina maana kubwa kwa jamii na ndio maana Umoja wa mataifa miaka 13 iliyopita iliamua kuadhimisha siku hiyo kwa lengo la kushawsihi makundi yanayosigana kupata nafasi ya kuzungumzia na kuona maana ya amani.
Alisema pamoja na kuwepo kwa hatua kubwa tangu kupitishwa kwa azimio la Umoja wa Mataifa la kuadhimisha amani, safari ya kufikia amani ni ndefu na ili kufanikiwa pande zote ni lazima kwenda hatua kwa hatua kwa kushirikiana.
Alisema mafanikio ambayo yamepatikana ni pamoja na UN kufanikiwa kufundisha kada ya habari juu ya uandishi katika mazingira tete na kusaidia majadiliano ya kitamaduni yanagusa masuala ya amani.
Mtaalam wa Mahusiano na Mawasiliano wa Umoja wa Mataifa (UN) Tanzania, Hoyce Temu (katikati) akimtambulisha Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez (wa pili kushoto) mara baada ya kuwasili kwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nchini Tanzania (THBUB), Bi. Mary Massay.
Aidha alisema kwamba wanafanyakazi na Wizara ya mambo ya ndani kuhakikisha kwamba wanastawisha mipango yote inayolenga kuzuia ghasia na kuboresha mipango inayoimarisha amani.
Akihutubia bada ya mashuhuda kuzungumzia hali ya tishio la amani nchini Tanzania hasa la kukosekana kwa amani miongoni mwa watu wenye ulemavu wa ngozi albino, Mwakilishi huyo wa Umoja wa Mataifa aliipongeza serikali ya Tanzania kw ajuhudi zake za kuimarisha amani katika kanda ya maziwa makuu na kushiriki katika operesheni mbalimbali za Umoja wa Mataifa ziliziolenga kuleta hali bora zaidi ya maisha kwa watu wanaoishi katika hekaheka za kivita.
Akiwa na mwezi mmoja tangu awalisili nchini mwakilishi huyo wa Umoja wa Mataifa nchini amesema kwamba anatarajia kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali na wananchi wa Tanzania kuhakikisha taifa la Tanzania linaendelea kuwa na amanai
Wakati Mwakilishi huyo amesema kwamba watu wengi duniani wanawaonea gere wananchi wa Tanzania kwa amani wlaiyonayo, mwakilishi wa Under the Same Sun, Vicky Ntetema ametaka kupitiwa upya kwa sheria ya uchawi ya mwaka 1928 iliyofanyiwa mabadiliko mwaka 2002 ili kukabiliana na mauaji ya albino nchini ambayo kwa kiasi kikubwa yanachochewa na waganga wa kienyeji.
Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez akisalimiana na Mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya siku ya kimataifa ya Amani, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Mh. Seif Rashid meza kuu.
Alisema sheria hiyo ina mwanya mkubwa wa wauaji kucheza nayo na kusababisha sehemu kubwa ya kesi zilizopo kushindwa kuwatia hatiani wahusika.
Alisema wakati tukielekea katika uchaguzi mkuu mauaji ya albino na ukataji wa viungo umeongezeka.
Tanzania ikiwa ni miongoni mwa nchi 25 za afrika zinazofanya ukatili dhidi ya walemavu wa ngozi, toka mwaka 2006 watu 74 wameuawa, 56 wamenusurika na 11 wameongezewa ulemavu huku makaburi 18 ya albino yakinajisiwa kwa kufukuliwa.
Watu wa kituo cha haki za binadamu wamesema pamoja na kuwepo na matukio 120 ya ukatili dhidi ya albino kesi 11 tu ndio zilizofikishwa mahakamani huku tano zikiwa zimekatiwa hukumu ambazo hazijaridhisha.
Vicky alisema katika matukio yote hayo chanzo ni ushirikina lakini kutokana na kukosekana zimeshindikana kuzimaliza zinavyotakiwa.
Brass band ya jeshi la Magereza ikiongoza maandamano ya kuadhimisha siku ya kimataifa ya amani wakiwasili kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam wakati wa maadhimisho hayo jana.
Vicky aliitaka jamii kuwalinda albino kwani serikali pekee haiwezi kufanya kitu chochote huku akisema kwamba hesabu ya albino mmoja katika kila wananchi 1,400 haiwezi kulindwa kwa dhati na serikali kutokana na idadi ya polisi kutokua sawa na wananchi.
Aidha alishauri serikali kutoa msaada wa kisheria kwa waathirika kabla ya kuingia mahakamani ili waweze kusimulia vyema kadhia zao na pia wasiangushwe na wanasheria ambao wanatumia udhaifu wa kisheria kuwatoa watuhumiwa hatiani.
Pamoja na Vicky Ntetema kushawishi wananchi kulinda albino na kuwafichua wauaji Kaimu Mufti Sheikh Ismail Habibu Makusanya ameitaka serikali kuhakikisha kwamba kila mwananchi anapata utulivu wa kutosha kuendelea na shughuli zaka na kuhimiza mahakama kutenda haki.
Aliwakumbusha wananchi kama alivyosema Sydina Omar kwamba kila mmoja ataulizwa amefanya nini kukomesha madhila katika jamii wakati wa kiama na kusema serikali isipowajibika itasema nini na wananchi nao pia watajibu nini.
Pichani ni baadhi wadau kutoka taasisi mbalimbali pamoja na watu wenye ulemavu wa ngozi (Albinism) wakiwasili kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja huku wakiwa wamebeba mabango yenye jumbe mbalimbali za kuhamasisha amani nchini na kupinga mauji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (Albinism) nchini wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya amani iliyofanyika jana jijini Dar.
Alisema amani hailetwi kama mvua , inatafutwa na kusema watu wasipotafuta amani na kuhakikisha amani inakuwapo itakuwa shida kubwa kwa taifa hili ambalo miaka yote limeogelea katika bahari ya amani.
Aliwasihi waumini wa Kiislamu na wananchi wengine kuhakukisha kwamba amani inakuwa ajenda ya kudumu kila wanapokutana pamoja.
Katika maadhimisha hayo ambapo wananchi walianza maandamano shule ya Uhuru Mchanganyiko hadi viwanja vya Mnazi mmoja, mgeni rasmi Waziri wa Afya na Ustawi wa jamii Dk Seif Rashid alisema serikali imejipanga kuhakikisha inakomesha mauaji ya albino na kuwataka wananchi kuisaidia kwa kutokuwa waoga kutoa ushahidi na pia kuwaripoti watuhumiwa.
Alisema kauli mbiu ya mwaka huu ya haki ya amani kwa watu wote, komesha mauaji ya albino inahamasiaha umma wa Tanzania kulaani,kukemea na kukomesha mauaji kwani yanakwenda kinyume na katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 ibara ya 14 ambayo inaeleza kwamba kila mtu ana haki ya kupata hifadhi katika jamii.
Aidha waziri alitaka kutekelezwa kwa agizo lake kuhusu tiba mbadala na za asili na kusema serikali itaendelea kulinda amani na kutoa ulinzi kwa wathirika.
Meza kuu ikipoeka maandamano ya siku ya kimataifa ya amani kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Albino Tanzania (TAS), Joseph Masasi akitoa neno la ukaribisho kwa mgeni rasmi Mh. Seif Rashid (wa pili kulia). Kutoka kushoto ni Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez, Kamishna wa Ustawi wa Jamii, Bw. Dunford Makala, Balozi wa Uturuki nchini, Mh. Ali Davutoglu.
Mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya siku ya kimataifa ya Amani, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Mh. Seif Rashid, akisoma hotuba kwenye maadhimisho ya siku ya kimataifa ya amani yaliyofanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez, akisoma ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Ban Ki-Moon kwenye maadhimisho ya siku ya kimataifa ya amani duniani.
Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez akipongezwa na Balozi wa Uturuki nchini Tanzania, Mh. Ali Davutoglu baada ya kusoma ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la UNDER THE SAME SUN, Vicky Ntetema akisoma risala yake kwa mgeni rasmi wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya amani iliyofanyika jana jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mufti Sheikh Ismail Habibu Makusanya, akizungumza kwenye maadhimisho hayo ambapo alilaani vikali mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (Albinizim) na kusema kuwa watu wote wanaoshiriki katika mauaji hayo kamwe hawatoiona Pepo ya Mwenyezi Mungu.
Balozi wa Uturuki nchini Tanzania, Mh. Ali Davutoglu akisoma ujumbe kwa niaba wa umoja wa mabalozi kwenye maadhimisho ya siku ya kimataifa ya amani duniani.
Baadhi ya wadau kutoka taasisi na asasi mbalimbali nchini walioshiriki kwenye maadhimisho hayo.
Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nchini Tanzania (THBUB), Bi. Mary Massay akitoa nasaha kutoka kwa Tume hiyo, ambapo alitoa rai kwa mtu yeyote yule ambaye ana malalamiko au matatizo katika Haki za Binadamu anakaribishwa kwenye tume hiyo kwa ajili kupata msaada wa kisheria.
Shuhuda aliyenusurika kwenye mauaji ya Albino ambaye amekatwa mikono yote miwili, Mariam Stanford akitoa ushuhuda wake na killio chake mbele ya meza na wageni waalikwa waliohudhuria sherehe za maadhimisho ya siku ya kimataifa ya amani iliyofanyika jana jijini Dar es Salaam kwenye viwanja vya Mnazi mmoja.
Mke wa Balozi wa Uturuki nchini Yesim Davutoglu, akilia kwa uchungu baada ya kusikia shuhuda kutoka kwa mhanga wa mauaji ya Albino aliyekatwa mikono yote miwili, Mariam Stanford (hayupo pichani) ambaye hadi sasa anapewa matunzo na Shirika la Under The Same Sun.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la UNDER THE SAME SUN, Vicky Ntetema akimfariji mke wa Balozi wa Uturuki nchini Yesim Davutoglu, wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya amani duniani iliyofanyika kwenye viwanja vya Mnazi mmoja jijini Dar.
Kwa matukio zaidi ingia humu
regards,
0 Comments