Wakala wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) umetangaza kufungwa kwa uwazi uliokuwa umeachwa kwa muda katika maeneo mawili tayari kwa kuanza kwa huduma ya mpito ya mradi huo kuanzia kesho Ijumaa (tarehe 08/04/2016).
Taarifa iliyotolewa na Kaimu Mtendaji Mkuu wa wakala wa DART, Mhandisi Ronald Lwakatare jana jijini Dar es Salaam imezitaja sehemu hizo kama katika kituo cha DART Ubungo Maji na kwenye kituo kikuu cha Mabasi yaendayo mikoani cha Ubungo.
Maeneo hayo mawili yamekuwa yakitumika na wenye magari kuingia na kutoka katika Wizara ya Maji na Umwagiliaji na pia katika kituo kikuu cha mikoani cha Ubungo.
“Ili kuwezesha huduma hiyo kukidhi mahitaji ya watumiaji kama ilivyopangwa, mkandarasi atafunga maeneo hayo yaliyokuwa yameachwa wazi,” alisema katika taarifa hiyo.
Mkandarasi anaejenga mradi huo ni STRABAG.
Kwa upande wa kituo cha DART Ubungo Maji, wakala huo umewaomba watumiaji wa vyombo vya usafiri waanze kutumia mzunguko uliosanifiwa eneo la Kimara Kibo (Rombo) huku wale kutoka katika kituo kikuu cha Ubungo wakiombwa kuanza kutumia mzunguko uliosanifiwa eneo la Shekilango kuanzia kesho.
Amesema hatua hiyo itasaidia kuondoa vikwazo kwa mazoezi ya mabasi yaliyokwisha anza kama ilivyokubalika wakati wa ziara ya wadau tarehe 16-17 Machi mwaka huu pamoja na kikao cha wadau cha tarehe 31 Machi mwaka huu chini ya uenyekiti wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Bw. George Simbachawene.
Wadau walioshiriki katika vikao hivyo na kukubaliana hatua hiyo ni pamoja na TAMISEMI, SUMATRA, TANROADS, Kikosi cha Usalama Barabarani kanda Maalum ya Dar es Salaam, Halmashauri za Manispaa za Kinondoni na Ilala, Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam, UDART, SMEC na STRABAG. |
0 Comments