Maalim
HOTUBA YA MAALIM SEIF SHARIF HAMAD KWENYE MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI – PARK HYATT ZANZIBAR,
TAREHE 10 APRILI, 2016
Ndugu zangu Waandishi wa Habari,
Ndugu Waalikwa,
Naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutujaalia uhai na uzima tukaweza kukutana hapa leo. Namshukuru Mwenyezi Mungu pia kwa kuijaalia nchi yetu kwa kiasi kikubwa kubaki katika hali ya amani na utulivu licha ya jitihada kubwa zilizofanywa na zinazoendelea kufanywa na baadhi ya watu za kuivuruga amani yetu. Naendelea kumuomba Mola wetu aendelee kuibariki nchi yetu na watu wake, aijaalie kuwa nchi ya amani na atujaalie hekima na busara katika kuendesha mambo yetu.

Nichukue fursa hii pia kukushukuruni nyinyi waandishi wa habari kwa kuitikia wito wetu na kuja kutusikiliza. Shukrani maalum zije kwenu wale ambao mmesafiri kutoka Dar es Salaam na kuja Zanzibar makhsusi kwa ajili ya mkutano huu. Tunathamini sana mashirikiano yenu nyote tukitambua nafasi na mchango mkubwa wa vyombo vya habari katika maendeleo ya nchi yoyote ile.
Mtakumbuka kwamba siku saba zilizopita tulizungumza nanyi ambapo tuliwasilisha kwenu maazimio 13 ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la Chama Cha Wananchi (CUF) kuhusiana na msimamo wa Chama chetu dhidi ya ubakaji wa demokrasia Zanzibar uliofanyika tarehe 20 Machi, 2016 na ambao ulipewa jina la uchaguzi wa marudio.
Leo hii tumekuiteni ili kutimiza agizo nililopewa na Baraza Kuu lililonitaka nizungumze na wananchi wa Zanzibar ili kuwaeleza kwa kina mwelekeo wa hali ya kisiasa ya Zanzibar na hatua zinazochukuliwa na CUF kuhakikisha maamuzi halali ya kidemokrasia ya Wazanzibari waliyoyafanya tarehe 25 Oktoba, 2015 yanaheshimiwa.
UCHAFUZI WA TAREHE 20 MACHI, 2016
Nilieleza kwa urefu katika mkutano wangu na waandishi wa habari wa tarehe 11 Januari, 2016 nilioufanya Dar es Salaam juu ya nini kilitokea baina ya tarehe 25 Oktoba 2015 hadi tarehe 28 Oktoba, 2015, siku ambayo Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salim Jecha, alitoa tangazo batili na haramu la kufuta uchaguzi huru na wa haki uliofanyika tarehe 25 Oktoba, 2015. Nilieleza pia hoja za kikatiba na kisheria za kwa nini tangazo lile ni haramu na batili na hoja zile hadi leo watawala wameshindwa kuzijibu. Kwa hoja hizo hizo, nikaeleza kwamba hakuna vifungu vya Katiba wala Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar Nam. 11 ya 1984 vinavyozungumzia kitu kinachoitwa uchaguzi wa marudio ukiondoa pale inapotokea wagombea wanapopata idadi sawa ya kura.
Sikusudii kurudia yale ambayo nilishayaeleza siku ile maana hayo sasa yanaeleweka na kila mtu ndani na nje ya nchi.
Leo hii nataka niwapongeze kwa mara nyengine tena wananchi jasiri na shupavu wa Zanzibar kwa kuitumia tarehe 20 Machi, 2016 kukifedhehesha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa mara ya pili ndani ya miezi sita mbele ya macho ya Watanzania na mbele ya macho ya jumuiya ya kimataifa. Wananchi wazalendo wa Zanzibar wanaoipenda nchi yao waliwakataa watawala waovu wa CCM na sera zao mbovu zinazoidhalilisha Zanzibar yao kupitia sanduku la kura tarehe 25 Oktoba, 2015. Watawala waovu wa CCM wakaamua kutumia mabavu na uvunjwaji wa katiba na sheria kuyapindua maamuzi ya Wazanzibari, kwa sababu tu maamuzi hayo yalikuwa ni ya kuwakataa watawala hao.
Kwa miezi mitano kuanzia Oktoba 2015 hadi Machi 2016, watawala waovu wa CCM wakawaingiza wananchi watulivu na wanaopenda amani wa Zanzibar katika idhilali na hilaki kubwa kwa kuwazuilia haki zao za msingi za binadamu ili wasiweze kuonesha hisia zao dhidi ya watawala. Kwa namna ya pekee na ya ustaraabu wa hali ya juu na wa kupigiwa mfano, wananchi wa Zanzibar wakaisubiri tarehe 20 Machi, 2016 na wakapeleka ujumbe wao kwa watawala hao na kwa dunia nzima kwa njia za amani za kuususia uchafuzi ulioitishwa siku hiyo. Hali halisi iliyoonekana na kila aliyetaka kuona ni kwamba zaidi ya asilimia 80 ya Wazanzibari hawakwenda kupiga kura siku hiyo ili kuonesha hisia zao na kuthibitisha tena maamuzi yao ya tarehe 25 Oktoba, 2015.
Kituo cha televisheni cha ITV kilichokuwa kikirusha matangazo ya moja kwa moja kutoka katika mikoa mitano ya Unguja na Pemba kilionesha vile vilivyoitwa vituo vya kupigia kura vikiwa havina watu kabisa au vikiwa na watu wachache sana. Walipowahoji wale walioitwa maofisa uchaguzi na walioitwa mawakala kila mmoja alikuwa akija na majibu yake na takwimu zake zinazopingana na za mwenzake. Vituo vya televisheni vya kimataifa hasa kile cha Al-Jazeera na CCTV ya China vilionesha na kuripoti vituo vikiwa vitupu. Hata televisheni ya watawala ya ZBC ilikuwa ikipata kigugumizi kuonesha hali ilivyokuwa katika vile vilivyoitwa vituo vya kupigia kura hadi kuamua kukatisha matangazo ya moja kwa moja. Magazeti ya Tanzania na ya nje ya nchi yaliripoti na kuchapisha picha zilizoonesha kususiwa kwa uchafuzi huo ulioitishwa na watawala wakidhani wanajihalalishia haramu yao. Mitandao ya kijamii nayo ilijaa maelezo na vielelezo kutoka watu na taasisi za kimataifa zinazoheshimika vikionesha hali halisi ilivyokuwa na ujasiri wa Wazanzibari wa kuususia uchafuzi huo. Na hatimaye nchi 16 zikatoa taarifa yao tarehe 21 Machi, 2016 wakieleza kwamba uchaguzi huo haukuwa wa kuheshimika kwa sababu haukuwa shirikishi na wala haukuwakilisha matakwa ya wapiga kura wa Zanzibar.
Nitumie fursa hii kwa mara nyengine tena kuwapongeza wananchi wote wa Zanzibar kwa ujasiri, uzalendo na ari kubwa walioionesha kwa kuitikia kwa kiasi kikubwa wito wa chama chao cha CUF wa kuwataka wasishiriki katika uhuni na ubakaji wa demokrasia uliopewa jina la uchaguzi wa marudio wa tarehe 20 Machi, 2016, na hivyo kuudhihirishia ulimwengu kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) hakina ridhaa ya wananchi wa Zanzibar.
Naungana na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF kuwapongeza waliokuwa wagombea wenzangu wa CUF kwa nafasi za Uwakilishi na Udiwani kwa kusimama na wananchi wa Zanzibar na kutoshiriki katika uchaguzi huo haramu na batili wa marudio, jambo ambalo limethibitisha kwamba hawapo kwa ajili ya kutaka nafasi na vyeo binafsi bali wanachotaka ni kuleta mabadiliko ya kweli kwa maslahi ya watu wote wa Zanzibar.
Pongezi zangu za dhati kabisa zinakwenda kwa wagombea Urais, Uwakilishi na Udiwani wa vyama vyengine vya upinzani ambavyo ni NRA, DEMOKRASIA MAKINI, SAU, UMD, JAHAZI ASILIA, CHAUMMA, UPDP, DP, na ACT-WAZALENDO, na vile vinavyoshirikiana kupitia UKAWA ambavyo ni CHADEMA, NCCR na NLD kwa kuungana pamoja na Wazanzibari kutetea demokrasia yao.
CCM WANAPENDA NAMBA LAKINI HAWAJUI HESABU
Jambo moja ambalo CCM wamejifedhehesha wenyewe ni lile la kutangaza kile walichokiita matokeo ya uchafuzi wao bila ya kuzingatia kwamba takwimu zina sifa moja, huwa hazisemi uongo. Vijana wana msemo wao siku hizi; wanasema CCM wanapenda namba lakini hawajui hesabu. Matokeo ya tarehe 20 Machi, 2016 waliyoyatangaza ni kwamba eti jumla ya watu waliopiga kura walikuwa 341,865 na kwamba Dk. Ali Mohamed Shein eti alipata kura 299,982 sawa na asilimia 91.4.
Takwimu za uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015 zilionesha kwamba jumla ya wananchi waliojitokeza kupiga kura walikuwa ni 402,354 na Dk. Ali Mohamed Shein alipata kura 182,011 sawa na asilimia 46.28.
Wakati huo huo kwa uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzaia, wapiga kura kwa upande wa Zanzibar walikuwa 417,882 ambapo mgombea wa CCM, Dk. John Pombe Magufuli alipata kura 194,317 sawa na asilimia 46.5.
Kwa hivyo, kwa kutumia takwimu hizi, mtu anapochukua takwimu hizi na kulinganisha wapiga kura 402,354 waliojitokeza tarehe 25 Oktoba, 2015 na wale wanaodai eti walijitokeza tarehe 20 Machi kwamba ni 341,865 watawala wa CCM walichotaka kutuaminisha ni kwamba tofauti ya waliokuwa hawakujitokeza kupiga kura ilikuwa ni 60,489 tu. Suala la kujiuliza ni kwamba iwapo hilo ni kweli kwa nini vituo vionekane vitupu kabisa tarehe 20 Machi, 2016?
Lakini kwa upande mwengine, mtu anapokosa hata tahayuri na kudai Dk. Ali Mohamed Shein amepata kura 299,982 anachotaka kutwambia ni kwamba ndani ya miezi mitano ya idhilali na mateso aliyowapatisha Wazanzibari ameweza kuongeza kura 117,971.
Kufedheheka kwa CCM kunakuja zaidi kwamba walisahau kwamba waliyakubali matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa tarehe 25 Oktoba 2015 kwa upande wa Zanzibar ambapo kama tulivyokwisha onesha waliopiga kura walikuwa wengi zaidi wakiwa ni 417,882 (na hilo ungetegemea lingeinufaisha CCM) na bado mgombea wa CCM akapata kura 194,317 sawa na asilimia 46.5. Kwa kutumia idadi waliyotangaza ya kura 299,982 walizompa Dk. Shein wanataka kutwambia kwamba yeye amepata kura 105,665 zaidi kuliko Dr. Magufuli kwa Zanzibar.
Kama takwimu zao zingekuwa sahihi ina maana pia wapiga kura waliomuunga mkono mgombea wa CUF ambao hawakwenda kupiga kura ni 60,489 tu (sawa na asilimia 15 tu). Hivi nani utamdanganya kwamba Maalim Seif Sharif Hamad anaungwa mkono na asilimia 15 tu ya wapiga kura wa Zanzibar? Nani utamdanganya kwamba ndani ya miezi mitano, CCM imeongeza kura 105,665 zaidi ya alizopata mgombea wake Dk. Magufuli kwa upande wa Zanzibar?
Kutokana na ubabe na kiburi cha utawala walicho nacho CCM, wameishia kujifedhehesha kwa takwimu zao za kupika wenyewe. Ndiyo vijana wakasema, CCM wanapenda namba lakini hawajui hesabu.
NINI MWELEKEO WA CUF NA WAZANZIBARI BAADA YA UBAKAJI HUU WA DEMOKRASIA?
Wazanzibari walio wengi wamekuwa wakituuliza nini mwelekeo wa CUF baada ya ubakaji huu wa demokrasia? Wanatuuliza viongozi wao na hasa mimi tunatokaje katika hali hii ambayo imedumu miaka nenda miaka rudi kila pale Zanzibar inapofanya uchaguzi?
Kabla sijalieleza hilo, nataka niweke wazi leo kwamba tulipofanya uamuzi wa kuususia uchaguzi haramu na batili wa tarehe 20 Machi, 2016 tuliamua kusimama juu ya uamuzi unaoheshimu misingi ya kikatiba ambayo watu wa Zanzibar tumeamua ndiyo inapaswa iongoze na iendeshe nchi yetu. Tulijua kwamba uamuzi huo utakuwa na athari kwa CUF na kwa Zanzibar lakini tulijua na tuliamini pia kwamba athari hiyo haiwezi kuwa kubwa zaidi kuliko gharama ya kuikanyaga Katiba na Sheria za nchi yetu na gharama za kupiga teke demokrasia, haki za binadamu na utawala wa sheria.
Tulipima na tukatafakari kwa kina na kuona ni kheri kumeza machungu ya athari binafsi kwetu lakini tusimame kidete na kifua mbele katika kutetea maamuzi ya watu wa Zanzibar waliyoyafanya tarehe 25 Oktoba, 2015, na pia kulinda misingi ya Katiba na Sheria za nchi yetu na misingi ya demokrasia na haki za watu. Tuliona hayo ni kheri kwa huko twendako badala ya kushiriki katika haramu ya ubakaji wa demokrasia na matumizi ya nguvu za kijeshi kulazimisha watawala wasio na ridhaa ya watu. Tulifanya maamuzi yale pia kwa lengo la kuepusha shari katika nchi yetu. Leo Wazanzibari na dunia nzima ni mashahidi kwamba uamuzi ule ulikuwa sahihi na wa busara. Maana mateso na vitisho walivyokumbana navyo Wazanzibari wakati tumewaachia uchaguzi ule watawala waovu peke yao vilikuwa vya kiasi kile kilichoshuhudiwa. Je, tungeliamua kushiriki na kusimama kulinda na kutetea ushindi wetu hali ingekuwaje? Bila shaka nchi ingetumbukia katika machafuko ambayo watawala waovu walikuwa tayari yatokee kuliko kuridhia maamuzi halali ya wananchi wa Zanzibar.
Maamuzi yale yamethibitika pia kwamba ni sahihi kwa jinsi watu wa Zanzibar walivyoudharau na kuupuuza uchaguzi haramu na batili wa tarehe 20 Machi, 2016. Watawala waovu wa CCM waliwadharau watu wa Zanzibar na watu wa Zanzibar wakaamua kuwadharau wao tarehe 20 Machi 2016.
Kwa upande mwengine, uamuzi tuliouchukua na kuusimamia pia ni uamuzi uliosimama juu ya misingi ya heshima na misingi ya utu wa watu, ambayo yalikuwa ndiyo malengo sahihi ya Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, Hayati Mzee Abeid Amani Karume, malengo sahihi ya Chama cha Afro Shirazi na malengo sahihi ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964.
Kwa hakika, uamuzi wa kuupuuza na kuudharau uchafuzi wa tarehe 20 Machi, 2016 ni ushindi mwengine wa Zanzibar katika historia yake ya kisiasa.
Nimalizie sasa kwa kujibu hoja ya ni upi mwelekeo wa CUF na wa Wazanzibari baada ya ubakaji huu wa wazi wa demokrasia na haki za watu wa Zanzibar?
Kwanza, nirudie na kusisitiza msimamo wetu kwamba hatukubaliani na ubakaji wa demokrasia na haki za watu wa Zanzibar uliofanywa na watawala waovu wakisaidiwa na vyombo vya dola. Kwa msingi huo, Wazanzibari wataendelea kuipinga serikali isiyo na ridhaa ya watu kwa kutumia njia za amani, za kidemokrsia na zinazoendana na misingi ya Katiba na Sheria za nchi yetu.
Jana kumetangazwa kile kilichoitwa ni Baraza la Mawaziri. Msimamo wetu uko pale pale. Kama tusivyomtambua aliyelitangaza Baraza hilo, vivyo hivyo hatulitambui Baraza lake la Mawaziri.
Kwa hakika, kwa sababu msingi wa watawala waliojinyakulia madaraka ni kupitia uvunjwaji wa Katiba, kila kinachofuata kimekuwa kikiendeleza uvunjwaji wa Katiba. Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kupitia Marekebisho ya 10 ya mwaka 2010, Ibara ya 9 (1) inalazimisha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa na muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Ibara za 39, 39A na 42 za Katiba zimeeleza namna Serikali hiyo ya Umoja wa Kitaifa itakavyoundwa. Masharti yote hayo yanaendelea kuvunjwa na mtawala aliyeamua kuyapiga teke maamuzi ya Wazanzibari na kujiweka madarakani kwa nguvu. Kwa hivyo, Serikali yake haiwezi kuwa Serikali inayokwenda na Katiba. Kwa ufupi, si Serikali halali kwa mujibu wa Katiba.
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF katika kikao chake cha tarehe 2 – 3 Aprili, 2016 lilipitisha maazimio yafuatayo miongoni mwa maazimio yake:
“Azimio Nam. 9:
Haliyatambui matokeo ya uchaguzi huo haramu na batili, na kwa msingi huo halimtambui Dk. Ali Mohamed Shein kuwa Rais wa Zanzibar, haliwatambui waliotangazwa kuwa Wawakilishi na wala haliwatambui waliotangazwa kuwa Madiwani. Baraza Kuu linaungana na wananchi wa Zanzibar waliokataa kuwapa uhalali watu hao na kwa hivyo halitoitambua Serikali, Manispaa na Halmashauri za Wilaya zitakazoundwa na watu hao. CUF haitoshirikiana na Serikali itakayoundwa kwa sababu ni kinyume na Katiba ya Zanzibar, kinyume na Sheria ya Uchaguzi na haikutokana na ridhaa ya watu. Kwa vyovyote vile, Serikali itakayoundwa haitakidhi matakwa ya Katiba ya Zanzibar na hivyo CUF haitoshiriki kwenye uvunjaji wa Katiba ambayo inaeleza kwa uwazi kabisa namna ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.
“Azimio Nam. 10:
Linawataka wananchi wote wa Zanzibar kutumia njia za amani, za kikatiba na kisheria ambazo zimewahi kutumika katika nchi nyingine duniani kuwakataa watawala waovu na wasio na ridhaa ya watu waliojiweka madarakani kwa kutumia nguvu na ubakaji wa demokrasia kwa kutoipa ushirikiano Serikali itakayoundwa na watawala hao.”
Baada ya maazimio hayo ya Baraza Kuu, kinachofuata sasa ni utekelezaji wake. Hivi sasa tunapanga mikakati madhubuti ya utekelezaji wa maazimio hayo kwa kutumia njia za amani, za kidemokrasia na za kikatiba ili kutufikisha kwenye malengo yetu ya kuona maamuzi ya watu wa Zanzibar yanaheshimiwa.
Nina hakika kabisa kuwa mikakati tunayoipanga itazaa hatua ambazo zitaibana Serikali haramu na hatimaye itasalimu amri kwa wananchi wa Zanzibar ambayo kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ndiyo wenye mamlaka ya kuiweka madarakani Serikali wanayoitaka. Katika dunia ya leo, hatuwezi kuongozwa na watawala ambao hawakupewa mamlaka na watu wenyewe.
Pili, naipongeza na kuishukuru jumuiya ya kimataifa na washirika wa maendeleo kwa msimamo waliochukua wa kukataa kubariki ubakaji huo wa demokrasia na haki za watu wa Zanzibar na kukataa kushiriki katika uapishwaji wa mtu asiye na ridhaa ya wapiga kura wa Zanzibar. Napongeza hatua ambazo wameanza kuzichukua dhidi ya Serikali za CCM ambazo ndizo zilizosimamia ubakaji huo wa demokrasia na haki za watu. Natoa wito kwao kuchukua hatua kali zaidi dhidi ya watawala hawa waovu zikiwemo kuwawekea vikwazo vya kusafiri, kufuatilia akaunti zao za fedha nje ya nchi na hatua za kuchunguza matendo yao ya uhalifu dhidi ya binadamu. Wananchi waliodhulumiwa haki zao wanaziunga mkono hatua hizo wakiamini kwamba CCM ni lazima iwajibishwe kwa matendo yake maovu dhidi yao.
Nitumie fursa hii kwa mara nyengine tena kuwataka wananchi wa Zanzibar kudumisha amani ya nchi yetu na umoja wa watu wetu. Nikiwa kiongozi wao ninayewapenda na ambaye nimejitolea kuwatumikia katika umri wangu wote siwezi kuwaongoza kuelekea kwenye fujo na ghasia au vitendo vitakavyopelekea kuiharibu nchi yetu na kuathiri watu wetu. Nina imani kabisa kwamba njia tunayoifuata ni njia ya haki; na haki siku zote itashinda.
Mwaka 2009, mimi na mwenzangu, Dk. Amani Abeid Karume, tuliwaongoza Wazanzibari katika Maridhiano yaliyoashiria mwanzo wa ujenzi wa mahusiano mapya baina ya watu wema wa Zanzibar kwa kuzika siasa za ubaguzi, utengano, chuki, hasama na fujo na badala yake kusimamisha siasa za maelewano, umoja, upendo, mshikamano na udugu katika jamii yetu. Tulitegemea kuanzia pale tungeendelea mbele kwa kuchukua hatua za kuyaimarisha maridhiano yetu na kuyazamisha zaidi kwenye nyoyo za Wazanzibari. Binafsi nasikitishwa na kuhuzunishwa sana kuona watawala waovu wasiowatakia mema watu wa nchi hii wameturudisha tulikotoka kwa maslahi yao binafsi. Natoa wito kwa Wazanzibari wenzangu kuwa tukatae kurudishwa kwenye siasa zile za ubaguzi, utengano, chuki, hasama na fujo na kila mmoja afanye lile liliomo katika uwezo wake kuendeleza maelewano, umoja, upendo, mshikamano na udugu katika jamii yetu.
Wazanzibari tumeamua kuisimamisha tena Zanzibar yetu na Zanzibar itasimama tena Inshallah. Hilo sina wasiwasi nalo kama kiongozi wa Wazanzibari waliyenipa ridhaa yao.
HATIMAYE TUTASHINDA.
WANANCHI JASIRI NA SHUPAVU WA ZANZIBAR WATASHINDA.
Ahsanteni sana.