Rais wa wa Tanzania Dkt John Magufuli amelitaka jeshi la polisi nchini pamoja na ofisi ya mwendesha mashitaka kujirekebisha katika utenda kazi na kujiepusha na kashfa.
Amesema taarifa zinaonesha jeshi la polisi limekuwa likihusishwa na matumizi mabaya ya fedha hali inayoongeza ukubwa wa matatizo yanayokwamisha utendaji wake wa kazi.

Akiongea alipokuwa akifungua kikao cha kazi cha makamanda wa polisi wa mikoa, mawakili wafawidhi wa serikali wa mikoa na wakuu wa upelelezi wa Mikoa na Vikosi, Dodoma ametoa mfano wa taarifa za matumizi mabaya ya fedha zinazotolewa kwa ajili ya kununulia vifaa na sare za askari.
Aidha, amezungumzia mikataba yenye mashaka inayotiwa saini kati ya polisi na wawekezaji akisema baadhi ya mambo yanayoongeza hali ngumu ya utendaji kazi kwa jeshi hilo.
“Nimesema lazima nizungumze kwa uwazi, nisiposema kwa uwazi nitajisikia vibaya nikimaliza mkutano huu, nataka muelewe na muelewe ukweli direction (njia) ninayoitaka mimi.”
Dkt. Magufuli pia amelitaka jeshi la polisi kujiepusha na kashfa ambazo zimekuwa zikisemwa dhidi yake, ikiwemo maafisa wa polisi kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya na kuazimisha silaha kwa wahalifu wa ujambazi.
Kuhusu Ofisi ya Mwendesha Mashitaka, amesema amekuwa akisikitishwa sana na vitendo vya serikali kushindwa katika kesi nyingi mahakamani licha ya kuwa na wanasheria mahiri.
"Niwaombe mawakili na polisi wanaohusika na upelelezi mtangulize maslahi ya nchi mbele, kwa sababu kumekuwa na usemi kwa baadhi ya wapelelezi na mawakili wachache, nasema wachache, panapokuwa na kesi inayohusiana na pesa pesa, wana misemo yao wanasema dili limepatikana,” amesema.
“Na saa nyingine kesi inapopelekwa mahakamani wana-collude (wanakula njama) mawakili wa serikali na mawakili wanaomtetea mhalifu, na wanapo-collude (wanapokula njama pamoja) siku zote serikali inashindwa.”