WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye amesema hatolivalia njuga suala la vazi la Taifa bali atawaachia Watanzania kuamua wenyewe aina ya vazi walitakalo.
Nape alitoa msimamo huo mjini hapa juzi wakati akijibu hoja ya Ofisa Utamaduni wa wilaya ya Mkalama, Lunzegere Kilala katika kikao cha pamoja baina yake na waandishi wa habari na wadau mbalimbali wa michezo mkoani hapa.
Alisema ni kweli alikuta mjadala wa kutafuta aina ya vazi la taifa ukiendelea lakini alipouliza ni nchi gani imewahi kuendesha mchakato kama huo ili naye akajifunze, hakupata jibu lolote.
“Hivi mjadala wa vazi la Wamaasai ulifanyika wapi?” Alihoji Nape na kujiridhisha kuwa iwapo mjadala huo utaruhusiwa kuendelea, ukweli ni kwamba hatimaye vazi hilo litakuwa ni kwa ajili ya viongozi tu. “Mimi nachelea kuendeleza mjadala huo maana vazi la taifa halivaliwi kwa kutungiwa sheria bali ni hiari na mapenzi ya mvaaji mwenyewe,” alisema.
“Nadhani tuwaache Watanzania wajiamulie wenyewe maana tukilitungia sheria vazi la Taifa litageuka kuwa sare kama ilivyo kwa wanafunzi au wanajeshi jambo ambalo si jema hata kidogo”.
Alisisitiza umuhimu wa kulinda utamaduni na akasema kuwa Taifa lisilo na utamaduni wake hukosa mwelekeo.
“Kila mkoa uwe na kituo chake kwa ajili ya kuhifadhi tamaduni za mkoa husika kama ambavyo Mwanza wamefanya kwenye kituo cha Bujora”.
Akachekesha kwa kuhoji, “Kama uvaaji wake utakuwa ni kwa amri kama magwanda ha jeshi au ni hiari?”
Aliongeza: “Si rahisi kupata vazi la taifa, tutajikuta tunapata vazi la viongozi na si la taifa”. Hivyo, kwa kauli yake huo mchakato umefikia ukomo wake.
Aidha, alihimiza suala la sanaa kufanywa kuwa shughuli inayoliingizia Taifa kipato na hivyo kukuza uchumi badala ya kuwa ni burudani tu.
Waziri Nape alikuwa kwenye ziara ya mikoa ya Kagera, Mara, Shinyanga, Tabora na Singida ili kusikia na kujionea changamoto mbalimbali zinazokabili watendaji, wafanyakazi, waandishi wa habari na wadau wa Wizara hiyo
0 Comments