Msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema hakuna mgogoro wowote katika mchakato wa kukabidhi kijiti cha Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho kutoka kwa Mwenyekiti wa sasa Jakaya Kikwete kwenda kwa Rais John Magufuli.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Msemaji wa CCM Taifa, Christopher ole Sendeka ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) ilieleza taarifa hizo zinazushwa na baadhi ya vyombo vya habari visivyozingatia maadili ya taaluma ya uandishi wa habari.

“Baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vinatoa taarifa potofu kuhusu mchakato wa Mwenyekiti wa sasa wa CCM Dk Jakaya Kikwete kukabidhi kijiti cha uongozi wa CCM kwa Rais John Pombe Magufuli kama ilivyo mila na desturi ya CCM. “Yamekuwapo madai eti Mwenyekiti amekataa au anachelewesha kukabidhi kijiti.
Habari hiyo si kweli kabisa na ni kinyume chake, kwani Dk Kikwete amekuwa akisisitiza kukabidhi madaraka mapema iwezekanavyo. “Kwa ajili hiyo kwenye kikao cha Mei 3, 2016 alikataa kusiongezwe ajenda nyingine ambazo zitalazimisha Mkutano Mkuu Maalumu kuchelewa kufanyika kwa sababu ya kukamilisha maandalizi ya ajenda hizo na alisisitiza ajenda iwe moja tu,” ilieleza taarifa hiyo ya CCM.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Ole Sendeka, dhamira ya kufanyika Mkutano Mkuu Maalum Juni, 2016 iko pale pale na kwamba kilichoelezwa kwenye kikao ni kutaka kukamilisha utaratibu wa kupata fedha za kugharimia mkutano huo.
“Taratibu zikikamilika tarehe itapangwa. Mipango ya kutafuta pesa inaendelea na ikikamilika tarehe itatangazwa,” alisema Msemaji huyo wa CCM Taifa. Aliwataka wana-CCM wasihamanike wala kubabaishwa na taarifa za upotoshaji zinazofanywa na watu wenye nia mbaya na chama hicho, akisema watu hao ni wale ambao wamekuwa wakiiombea mabaya CCM bila ya mafanikio.
“Pia tunapenda kukanusha madai ati kuwa Mwenyekiti Kikwete aliwatahadharisha wajumbe wa Kamati Kuu kuhusu ukimya wa Edward Lowassa. Hakuna wakati wowote kauli kama hiyo aliitoa. Ni uzushi mtupu. Jina la Ndugu Lowassa halikutajwa kabisa,” alisema.
Katika hatua nyingine Ole Sendeka alikanusha madai ya kufanyika mkutano baina ya Mwenyekiti Kikwete, Rais Magufuli, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan na Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana, kuhusu uchaguzi wa Katibu wa Kamati ya Wabunge wa CCM.