Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, January Makamba
SIKU chache baada ya Tanzania kusherehekea maadhimisho ya miaka 52 ya Muungano, Serikali imesema, hali ya muungano huo ni imara na inazidi kuimarika kila kukicha.
Aidha, imebainisha kuwa hadi sasa imeshughulikia kero za Muungano tisa kwa kuzipatia ufumbuzi wa kudumu na imejipanga kushughulikia kero nyingine zilizobaki ikiwemo ya mafuta na gesiasili na usajili wa vyombo vya moto.

Akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha wa 2016/17, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, January Makamba, aliwataka watanzania kujivunia muungano huo kwa kuwa ndio alama halisi ya watanzania duniani kote.
Alitaja sababu za kuimarika kwa muungano huo kuwa ni pamoja na jitihada za Watanzania wenyewe na serikali katika kuhakikisha Muungano huo unadumu na kushughulikia ipasavyo kero za Muungano.
Alisema kati ya changamoto kubwa iliyoukabili muungano huo ni pamoja na ushiriki wa Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika Mashariki lakini tayari visiwa hivyo vimeanza kushirikishwa kikamilifu hasa baada ya kuwasilisha miradi yake kadhaa katika jumuiya hiyo.
Alisema Zanzibar iliwasilisha miradi yake ya uwanja wa ndege wa Karume, Pemba na Abeid Amani Karume ambayo kupitia Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imesaini mkataba na Serikali ya Tanzania kwa ajili ya kuimarisha sekta ya uchukuzi visiwani humo.
Alitaja changamoto zilizobakia kuwa ni mafuta na gesiasilia, usajili wa vyombo vya moto, hisa za Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar zilizokuwa katika bodi ya sarafu ya Afrika Mashariki na mgawanyo wa faida ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Akizungumzia mgawanyo wa mapato hayo, January alisema katika mwaka huu wa fedha, wizara yake ilipeleka Zanzibar jumla ya Sh bilioni 27.5 hadi kufikia Machi mwaka huu kama mgawo wa fedha kwa Serikali ya Zanzibar.
Alisema fedha hizo ni kwa ajili ya mishahara ambazo ni Sh bilioni 14, faida ya BoT Sh milioni 621.9, na gawio la misaada ya kibajeti Sh bilioni 9.974.
Alisema katika kuhakikisha pande zote za muungano zinanufaika programu ya maendeleo ya pamoja, Serikali imejipanga kufuatilia utekelezaji wa programu hiyo inayojumuisha Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF III).
Alisema katika kuhakikisha Muungano huo unadumu zaidi kwa vizazi vijavyo, serikali imeanzisha programu maalumu ya elimu kuhusu umuhimu wa Muungano hasa kwa vijana.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mohamed Mchengerwa alisema pamoja na hali ya muungano kuendelea kuimarika, Serikali bado ina wajibu wa kutoa elimu ya Muungano kwa wananchi ili wauthamini, kuupenda na kuulinda.
Hata hivyo, alisema wakati kamati hiyo ikipitia miradi ya maendeleo iliyopo chini ya wizara hiyo ya Muungano, ilibaini kuwa ujenzi wa jengo la ofisi ya makamu wa rais Dar es Salaam limejengwa chini ya kiwango.