Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa inafanya uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazowahusu  wafanyabiashara wa sukari nchini kwa kuficha
bidhaa hiyo ili  kusababisha upungufu
katika soko na hivyo kuleta usumbufu kwa jamii ya watanzania wanaohitaji bidhaa
hiyo kwa matumizi jambo ambalo limesababisha kupanda kwa bei hadi kufikia
shilingi elfu nne kwa kilo moja ya sukari. 


 Taasisi imeanza uchunguzi dhidi ya Tuhuma hizi
kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi na tayari tumeweza kutembelea Maghala ya
mfanyabiasha Haruni Daudi Zacharia ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Al-Naeem
yaliyoko Mbagala na Tabata ambaye ni miongoni mwa wafanyabiashara wakubwa
nchini wa sukari na anayetuhumiwa kuficha bidhaa hii. 


Mnamo tarehe 05 Mei, 2016
timu ya uchunguzi ilitembelea maghala ya Tabata na kubaini uwepo wa sukari
yenye jumla ya tani 4,579.2 iliyonunuliwa toka Kiwanda cha Kilombero Sugar
Company. 


Aidha uchunguzi ulibaini kuwepo kwa njama za dhati za kutouza kwa
sukari kulikofanywa na mfanyabiashara huyu kwani hata sehemu ya Maghala ilipo
sukari hapa kuwepo dalili za upakiaji wa sukari na baada ya kufika Kitumbini
tulibaini uwepo wa wananchi wengi waliokuwa wakihitaji bidhaa hiyo na wachache
sana waliweza kuuziwa tena kwa kiwango kidogo sana kuliko mahitaji yao. 


Wananchi wengi walikosa huduma hiyo licha ya ukweli kwamba sukari ilikuwepo. 

Uchunguzi uliofanyika umebaini kuwepo
kwa mikakati ya dhati iliyokuwa ikifanywa na mfanyabiasha huyu kwa kununua
sukari yote toka viwanda vya ndani na kisha kuihifadhi na kuuza bidhaa hiyo
kidogo kidogo kwa wastani wa tani 250 kwa siku wakati alikuwa na uwezo wa kuuza
zaidi jambo lililochangia uhaba wa sukari katika soko. Kuficha bidhaa ni kosa
la uhujumu uchumi na ni  kinyume na Aya
ya 3 Jedwali la kwanza Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura ya 200 [Chapisho la Mwaka
2002]. Serikali haitavumilia hujuma za namna hii na itachukua hatua kali dhidi
ya mfanyabiashara yeyote ataekwenda kinyume na sheria hii. 


Kuanzia sasa TAKUKURU inatoa wito kwa
wafanyabiashara wote wa sukari kuacha vitendo vya kuficha sukari na vyombo vya
uchunguzi vinafuatilia kote nchini na yeyote atakayebainika kufanya hujuma hizo
atakabiliwa na mkondo wa Sheria. 


VALENTINO MLOWOLA

 MKURUGENZI MKUU WA TAASISI 

YA KUZUIA NA
KUPAMBANA NA RUSHWA 



7 MEI, 2016