Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Alphayo Kidata
 akizungumza na waandishi wa habari (Hawapo pichani) kuhusu mwenendo wa
makusanyo ya mapato nchini kulia ni Kamishna wa kodi za ndani Bw. Yusufu
Salum.(Picha na Raymond Mushumbusi MAELEZO)



Na Raymond Mushumbusi MAELEZO

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewakamata zaidi wafanyabiashara 300 kwa kosa la kutotumia mashine za (Electronic Fiscal Devices) EFD’S katika biashara zao.

Akizungumzia na waandishi wa habari Jijini Dare s Salaam, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) Alphayo Kidata amesema mamlaka yake imefanya uchunguzi wa kina na kuwabaini wafanyabiashara hao katika maeneo mbalimbali nchini wakikiuka agizo la kuwa na mashine hizo.

“ Tumeshaanza kuwapeleka mahakamani wafanyabiashara ambao wanakwepa kulipa kodi kwa kuuza bidhaa bila risiti na pia tumetaifisha bidhaa mbalimbali zilizoingizwa nchini kwa njia ya magendo na kukwepa kodi “ Alisema Kidata.

Kamishna Kidata amefafanua kuwa mamlaka haitowavumilia wafanyabiashara wanaoikosesha mapato Serikali kwa kuuza na kutoa huduma bila risiti za EFD’s kwa makusudi na hasa wale wafanyabiashara wanaouza kazi za wasanii bila stempu za kodi pamoja na wafanyabiashara wanaojihusisha na magendo.

Vilevile amefafanua kuwa, kwa wafanyabiashara waliopelekwa mahakamani mara baada ya kumalizika kwa kesi zao na kupewa adhabu ya kulipa faini, wakibainika tena kurudia makosa hayo adhabu kali zaidi zitachukuliwa dhidi yao ikiwemo kifungo cha miaka mitatu jela kwa kukaidi agizo la Serikali.

Aidha, Mamlaka imetoza faini ya Shillingi Mil 746 kwa wafanyabiashara waliokutwa na makosa mbalimbali yakiwemo kutotumia mashine za kielotroniki za EFD’s , kuingiza bidhaa kimagendo na kuuza kazi za wasanii bila ya stempu ya kodi.

Mamlaka inatoa wito kwa wananchi wote kuwa mabalozi wa kodi na kichocheo cha ukusanyaji wa mapato kwakutimiza wajibu wao wa kudai risiti wanaponunua bidhaa au kupatiwa huduma mbalimbali.