Wabunge bungeni dodoma.
WABUNGE wanaopinga kiinua mgongo chao wanachopata baada ya miaka mitano kutozwa kodi, wamenyooshewa vidole na kuambiwa wanakwepa majukumu yao ya kuwajibika na kujiaibisha kwa wananchi.
Miongoni mwa watu waliozungumzia kitendo hicho, wamesema wabunge wanaopinga kukatwa kodi, wanajiaibisha kwa wananchi;
ambao licha ya wengi kuwa na kipato cha chini, wanalipa kodi. Katika kuunga mkono mapendekezo hayo ya serikali kukata kodi kiinua mgongo cha wabunge, yaliyomo kwenye hotuba ya bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2016/17 , baadhi ya watu wamekwenda mbali na kushauri pia ruzuku za vyama vya siasa zianze kukatwa kodi kwa ajili ya kuongeza mapato.
Wabunge wajipime Wamesema wabunge wana wajibu wa kujipima kama michango yao kwa Watanzania na serikali inaishia kuongea bungeni au pia uchangiaji wa kodi, ambazo kila Mtanzania anachangia kulingana na nafasi yake. Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, watu wa kada mbalimbali walisema kila mwananchi bila kujali wadhifa wake, analo jukumu la kuchangia pato la taifa kwa kulipa kodi.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana alisema jukumu la raia mwema ni kulipa kodi kusaidia serikali yake . Alisema wabunge ni miongoni mwa raia hao, ambao wanapaswa kutambua kwamba hawapaswi kukwepa jukumu hilo. “Mbunge ni kama raia wengine ambao wanatakiwa kuchangia nchi yao; Tena kiongozi mwenye sifa ni yule anayechangia nchi yake, anatembea kifua mbele kwa kuchangia, wewe mbunge usiyechangia ni kiongozi wa aina gani?” Alihoji Dk Bana.
Ruzuku za vyama Aidha, Dk Bana alisema pamoja na wabunge kukatwa kodi, serikali iangalie pia namna ya kukata kodi katika ruzuku ambazo vyama vya siasa hupata ambavyo kwa sasa hawakatwi. “Serikali pia iangalie namna ya kukata kodi katika vyama hivi ambavyo kazi yao kubwa fedha hizo ni kuandaa mikutano ambayo ni vurugu tupu na kesi mahakamani kila kukicha,” alisema Dk Bana.
Hata hivyo, mhadhiri huyo wa chuo kikuu alisema, wabunge wanachotakiwa kufanya, ni kuomba majadiliano na serikali kiasi ambacho wanaona kinapaswa kukatwa kwenye kiinua mgongo chao. Alisema si sahihi kukataa kukatwa kodi wakati Watanzania wa hali ya chini wanakatwa kodi. Alisisitiza kuwa wabunge wanapaswa kujipima kuwa michango yao kwa Watanzania na serikali ni michango yao ya maneno bungeni au pia katika kodi ambazo kila Mtanzania anapaswa kulipa nao wanachangia.
Alishauri wabunge waelimishwe juu ya suala hilo huku akisisitiza kuwa ni jambo lisilowezekana kwa wanasiasa hao ambao hupanga mambo mbalimbali ikiwemo sheria za kodi, wakati wao wenyewe hawataki kuzitii. “Huu utakuwa ni uongozi mbovu ambao wabunge wanauonesha, hii ni mipango ya serikali katika kukusanya kodi hivyo na wabunge wanapaswa kushirikiana na serikali kuwaletea wananchi maendeleo ambayo yanapatikana baada ya kukusanywa kodi,” alisema Bana na kupongeza serikali kwa hatua hiyo.
Wanajiaibisha Kwa upande wake, Mhadhini wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Kitila Mkumbo alisema wabunge wanapaswa kutambua kwamba serikali imepania kukusanya kodi hivyo hawapaswi kukataa au kupingana nayo. Mkumbo ambaye pia ni Mshauri wa Chama cha ACT Wazalendo, alisema wabunge wanaopinga kukatwa kodi wanajiaibisha kwa wananchi kwani wananchi wa kipato cha chini wanalipa kodi.
“Katika kujenga nchi mchango wako unakuwa katika kulipa kodi na mfano huo unatakiwa kuoneshwa na viongozi wenyewe ambao ni pamoja na wabunge,” alisema Mkumbo.
Alisema anaamini wapo wabunge wazalendo ambao watasimamia katika misingi inayofaa na kupongeza hatua ya serikali kukusanya kodi katika eneo hilo. Mkazi wa Kigamboni, jijini Dar es Salaam John Abenja alisema wabunge hawana haja ya kulalamika kwani wanalipwa fedha nyingi kuliko watu wa hali ya chini ambao wanakatwa kodi bila kuwa na malalamiko.
“Sasa hawa ni viongozi wa aina gani? Wao wanalipwa fedha nyingi wanakataa kukatwa kodi wakati sisi walala hoi tunakatwa kodi bila kupata pa kulalamikia,” alisema Abenja ambaye ni mwendesha bodaboda. Alitoa mfano wa walimu ambao ni miongoni mwa watumishi wenye mishahara midogo kuwa wamekuwa wakikatwa kodi na hawalalamiki, kama ambavyo imejitokeza kwa wabunge.
Alisema kama sasa serikali imeona eneo hilo (kiinua mgongo cha wabunge), lilikuwa halikusanyi kodi, ni vizuri wabunge wawe sehemu ya kuchangia kodi kwa kuacha kutoa visingizio. Wafananishwa wanyonyaji Mwingine aliyezungumza na mwandishi ni Mwalimu, Mselenga Nungu aliyesema kitendo cha wabunge kutotaka maslahi yao yaguswe wakati wengine yanaguswa, ni unyonyaji kwa wananchi wa kawaida.
“Mfano mimi ni mwalimu mpaka nastaafu ni miaka 20 ijayo kiinua mgongo changu kitakatwa kodi, na mshahara wangu unakatwa kodi, kwanza nilikuwa sijui kama wabunge walikuwa hawakatwi kodi huu ni unyonyaji,” alisema Nungu. Alisema ni uonevu kwa wananchi wa kawaida ambao wanalipa kodi. Alisisitiza kwamba, kila pato inapaswa kiwe chanzo cha mapato kwa maendeleo ya taifa bila kubagua makundi.
Kwa upande wake, aliyewahi kuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, David Kafulila alisema serikali haitapata kodi katika mwaka wa fedha 2016/2017 kwani hakuna mbunge anayepata kiinua mgongo mpaka mwisho wa Bunge hilo mwaka 2020. “Hii kuijadili inakuwa haina maana kwa sababu hakuna fedha ambayo serikali itaikusanya kwa mwaka huu wa fedha kwa sababu wabunge watalipwa kiinua mgongo mwaka 2020 na malipo hayo yanastahili kodi kisheria lakini kisiasa Serikali inaogopa wabunge,” alisema Kafulila.
Wakati baadhi ya wabunge walikaririwa hivi karibuni wakilalamikia mapendekezo hayo ya kukatwa kodi kwenye kiinua mgongo, Mbunge wa Kigoma Mjini, Kabwe Zitto amepongeza serikali kwa hatua hiyo. Zitto alikwenda mbali na kushauri serikali itoze kodi pia kwenye posho za wabunge, akisema wanapokea kiasi kikubwa cha posho kwa shughuli mbalimbali wanazofanya, ikiwekwa kando Sh 220,000 ya kikao kimoja cha Bunge wanachohudhuria.
Akizungumza katika mdahalo wa uchambuzi wa bajeti ya serikali ya mwaka 2016/17 ulioandaliwa na Kampuni ya Ukaguzi wa Hesabu ya KPMG hivi karibuni, Zitto alisema wabunge wakikatwa kodi kwenye posho hizo mapato ya nchi yataongezeka. Kwa mujibu wa Zitto, kwa mwaka, wabunge hupokea posho ya Sh milioni 40 ambayo ikizidishwa kwa miaka mitano ni zaidi ya Sh milioni 200 huku kiinua mgongo kikiwa Sh milioni 172.
Wanaopinga kodi Baadhi ya wabunge waliopinga kiinua mgongo kukatwa kodi, walisema uamuzi huo si sahihi kwa kuwa utaminya maslahi yao na unalenga kuwasukuma kuwa ombaomba baada ya kustaafu kazi hiyo. Kamati ya Bunge ya Bajeti kupitia kwa Mwenyekiti wake, Hawa Ghasia ilipendekeza kuwa iwapo hakuna marekebisho yatakayofanywa na serikali kuhusu kodi hiyo, tozo ya namna hiyo iguse pia viongozi wote wa kisiasa kuleta usawa katika maslahi.
Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM) pia alipinga akisema serikali haiwatakii mema. Alisema fedha za wabunge huishia kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo na kuombwa na wananchi wanaopatwa matatizo majimboni mwao. Mbunge wa Sikonge, Joseph Kakunda (CCM), alisema, Ofisi ya Mbunge ni taasisi inayojitegemea na kwamba fedha zinazoonekana nyingi si za mbunge, bali ni za jamii.
Pia Kambi ya Upinzani Bungeni ilisema serikali haijawataja Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya katika kundi la wanaopaswa kutozwa kodi ya kiinua mgongo, badala yake imewabana wabunge pekee. Mbunge wa Mkinga (CCM), Dastan Kitandula alishawishi wabunge kutoidhinisha bajeti ya serikali kwa kile alichosema, ikiwa ushauri wa Kamati ya Bajeti utapuuzwa.
Katika hatua nyingine, Bunge linaendelea leo, ambapo baada ya maswali na majibu wabunge wataendelea kuchambua mapendekezo ya Bajeti ya Serikali na kutoa maoni kuhusu Mpango wa Serikali wa 2016/2017.