Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
SASA ni dhahiri kuwa azimio lililotangazwa miaka 43 iliyopita la kubadili makao makuu ya nchi kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma limepata kasi mpya, baada ya kusuasua kwa muda mrefu kufuatia hatua ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kutangaza kuhamia mjini hapa Septemba mwaka huu.

Waziri Mkuu pia aliwataka mawaziri wake wahakikishe wanahamia mjini hapa mara moja. Jumamosi iliyopita wakati akitoa hotuba ya shukrani baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais John Magufuli alitangaza kuwa kabla ya kumalizika kwa awamu ya kwanza ya muhula wake wa uongozi wa nchi mwaka 2020, atakuwa amehamia Dodoma.
Rais Magufuli alisisitiza tena kauli hiyo jana wakati akizungumza katika sherehe za Siku ya Mashujaa mjini hapa, lakini Waziri Mkuu Majaliwa akaonesha mfano akiwa msimamizi mkuu wa Serikali kuwa atahamishia ofisi yake mkoani humu ifikapo Septemba mwaka huu.
“Jana nilimwita Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu na kumwambia akamilishe matengenezo kwenye nyumba yangu kwa sababu ninataka kuhamia Dodoma ifikapo Septemba,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa kwa kauli iliyopokelewa kwa shangwe na wananchi wa Dodoma waliohudhuria sherehe hizo.
Majaliwa alisema kuwa akishatangulia mawaziri wote na naibu mawaziri nao watamfuata. Alisema ameagiza wizara zote, kuhamia mara moja Dodoma kutoka Dar es Salaam na kwamba huo ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Magufuli.
“Mawaziri wana nyumba na pia wana ofisi ndogo Dodoma, naagiza wahame mara moja Dar es Salaam kuja Dodoma. Kwa upande wangu nimeshaagiza nyumba yangu ikamilishwe ili nihamie mwezi Septemba. Nikitangulia mawaziri wote watanifuata,” alisema Majaliwa.
Alimuahidi Rais Magufuli kuwa atasimamia utekelezaji wa mpango wa Serikali kuhamia Dodoma kwa nguvu zake zote.
“Utekelezaji wa suala hili nitaufanya haraka. Huu ni mwanzo wa makao makuu kuhamia Dodoma,” alisema na kuwataka wakazi wa Dodoma kuanza kuwekeza katika mambo mbalimbali.
Alisema jambo la kwanza ni kuhakikisha mji wa Dodoma unakuwa kisiwa cha amani na pili kuwekeza kwenye ujenzi wa hoteli kubwa za kisasa zikiwemo za kitalii, nyumba na mazingira bora ya biashara.
Alisema Dodoma ikiwa makao makuu, watu wengi watakuja kuwekeza, hivyo wakazi wa Dodoma wawe wa kwanza kutumia fursa hiyo.
Rais Magufuli alieleza kuwa Serikali yake imeshatimiza miezi minane na sasa imebakiza miaka minne na miezi minne, hivyo aliwahakikishia Watanzania na wakazi wa Dodoma kuwa katika muda huo uliosalia kumaliza miaka mitano, atahakikisha Serikali yote inahamia Dodoma na alitaka viongozi wengine waache kutafuta visingizio.
Alisema kwa sasa mji wa Dodoma una miundombinu inayoweza kuhudumia ofisi nyingi za Serikali na una huduma mbalimbali za kijamii. Mathalani, alisema tayari Serikali inaendelea na ukarabati na upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Dodoma ili kuwezesha hata ndege kubwa, aina ya Boeing kuweza kutua.
“Watani zangu Wagogo tembeeni kifua mbele. Ahadi ni deni na ahadi ni lazima tutaitimiza bila kuchelewa. Tuliahidi wakati wa kampeni na sasa tumeanza kutekeleza,” alisema Magufuli.
Akizungumza katika sherehe hizo, Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi au Mzee Ruksa alisema Watanzania walikubali kuhamishia makao makuu Dodoma, lakini mpango huo umechelewa kutekelezwa. “Tumekawia vya kutosha kuhamia Dodoma. Sasa ndoto za Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kuifanya Dodoma kuwa makao makuu ya nchi inatimia. Tuhamie Dodoma tuachane na maneno maneno,” alisema Mwinyi.
Waziri Mkuu mstaafu, John Malecela alisema anamshukuru Rais Magufuli kwa kutangaza kuhamia Dodoma na kwamba katika maisha yake, kauli hiyo ya Rais imempa amani na furaha ya kupindukia moyoni na kuufanya moyo wake uchemke.
“Tunakushukuru sana Mheshimiwa Rais Magufuli kwa matamshi yako kwenye Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi na pia hapa kwenye maadhimisho ya Mashujaa kwamba wewe na Serikali yako mtahamia Dodoma,” alisema na kumuahidi Rais Magufuli kwamba wakazi wa Dodoma watakuwa naye bega kwa bega kumsaidia atekeleze azma yake hiyo.
Alisema, “Kwa sisi Wagogo Rais ni mtani wetu. Mimi kama mwenyeji, kwa niaba ya wenzangu, tunasema asante sana, karibu sana na tutakuwa nawe bega kwa bega,” alisema Malecela ambaye mara kadhaa alitumia lugha ya asili ya kabila lake, Kigogo.
Baadhi ya wananchi wa Dodoma waliohojiwa, walisema Rais Magufuli ametoa kauli hadharani kuonesha azma yake ya kuhamia Dodoma.
Mmoja wao ambaye ni Katibu wa wafanyabiashara ndogo mkoani hapa, John Tambala aliishauri Serikali kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya wafanyabiashara ndogo ili wasisambae mitaani kufanya biashara katika maeneo yasiyoruhusiwa.
Alisema kwa kufanya hivyo, kutawezesha wakazi wa Dodoma kufaidi uwepo wa makao makuu ya nchi.
Shehe wa Jumuiya ya Wahamadiya mjini Dodoma, Barshat Butt alisema wazo la kuhamia Dodoma lilitolewa na Rais wa Awamu ya Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere, lakini lilichelewa kutekelezwa na Rais Magufuli ameanza kulitekeleza kwa vitendo.