WIZARA ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imemtangaza mwandishi wa habari mwandamizi, Hassan Abbas kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Assah Mwambene aliyehamishiwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Akizungumza jana Dar es Salaam, Waziri wa wizara hiyo, Nape Nnauye alisema kabla ya uteuzi huo, Abbas alikuwa Meneja Habari na Mawasiliano katika Ofisi ya Rais inayosimamia utekelezaji wa Programu ya Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
“Mkurugenzi huyu amechaguliwa baada ya kufanyika kwa mchakato kwa mujibu wa sheria za Utumishi wa Umma,” alisema Nape na kumshukuru aliyekuwa akikaimu nafasi hiyo, Zamaradi Kawawa ambaye alifanya kazi zake kwa uadilifu na kujituma kwa kusimamia majukumu yote ya idara kwa ukamilifu.
Alitoa mwito kwa vyombo vya habari na wadau wa habari kutoa ushirikiano wa kutosha kwa mkurugenzi huyo atakapokuwa akitekeleza majukumu yake kama Msemaji wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari. Aidha, Nnauye ameendelea kuvisisitiza vyombo vya habari kufuata sheria zilizopo japo zina upungufu.
“Hakuna uhuru usio na mipaka, ni lazima kufuata taratibu na sheria zilizopo hatutavumilia chombo chochote kinachoripoti uchochezi na sisi tutajitahidi kuharakisha miswada ya habar ili tuwe na sheria nzuri,” alisisitiza Nape.
Akizungumza baada ya kutambulishwa, Abbas alishukuru kwa uteuzi huo na kuahidi kuleta mabadiliko katika idara hiyo.
“Nimepokea uteuzi na ninaahidi kufanya kazi ninachohitaji kwenu na kwa Watanzania ni ushirikiano na mimi naahidi kutoa ushirikiano, mtegemee mabadiliko makubwa,” alisema.