Dk James Mataragio
BODI ya Wakurugenzi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) imemsimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Dk James Mataragio.
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya shirika hilo na wadau mbalimbali wa masuala ya mafuta na gesi, zimeeleza kuwa kusimamishwa kazi kunatokana na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu (CAG) ya mwaka jana iliyoeleza kuwa, TPDC ilikiuka taratibu za manunuzi ya umma kwa kuipa upendeleo kampuni ya Marekani kutafiti mafuta na gesi katika maeneo ya kaskazini na magharibi mwa Ziwa Tanganyika, Songosongo, Mandawa na Eyasi.

“Shirika kwa sasa si salama, kwani mkurugenzi amepewa barua kutoka kwa mwenyekiti wa bodi kusimamishwa kazi kuanzia jana (Jumatano) kutokana na ripoti ya ukaguzi,” alisema mmoja wa watoa taarifa.
Hata hivyo, mpaka jana jioni hakukuwa na taarifa rasmi kuhusu kusimamishwa kazi kwa mkurugenzi huyo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa alipoulizwa kuhusu hatua hiyo, alisema anafahamu suala la kusimamishwa kazi kwa Dk Mataragio, lakini akaongeza kuwa, maelezo zaidi kuhusu maamuzi hayo anayo Mwenyekiti wa Bodi ya shirika hilo, Profesa Sufian Bukurura.
Hata hivyo, Mwenyekiti huyo alipotafutwa kwa simu kutoa taarifa rasmi za kusimamishwa kazi kwa mkurugenzi huyo, hakupatikana kwani mara zote simu yake ilisema inatumika.
                    Chanzo cha habari hizi ni kutoka habari leo.