Serikali ya Burkina Faso imepiga marufuku usafirishwaji wa ngozi ya punda kwenda Asia kwa lengo la kuwalinda wanyama hao ambao wanasaidia familia nyingi katika shughuli za kilimo hasa vijijini.

Ingawa biashara hiyo ya ngozi ya Punda imekuwa ikiingiza dola nyingi za kimarekani kwa mwaka katika taifa hilo, lakini Serikali hiyo imetoa marufuku hiyo jana na kueleza kuwa punda wamekua wakipungua miaka ya hivi karibuni kutokana na kusafirishwa kwenda Asia ambapo usafirashwaji umeongezeka mara 18 zaidi kwa kipindi cha januari hadi disemba mwaka jana. Takwimu rasmi zinaonesha miezi sita ya kwanza ni karibu ngozi elfu sitini na tano za punda zimesafirishwa Asia mashariki hususani China.
Ongezeko la mahitaji hayo kumesababisha soko la ndani kuongeza bei ya punda kutoka dola nne hadi dola 30. Katika wiki za hivi karibuni wakazi wa karibu na mji mkuu wa Ougadougou wamepekua bucha la punda lilifunguliwa na kampuni ya kichina wakipinga harufu iliyokua inatoka katika bucha hilo.

Punda ni maarufu sana katika maeneo mengi barani Afrika hususani vijijini ambapo wanatumika katika shughuli za kilimo na usafiri, hawana gharama kubwa na wanadumu kwa muda mrefu zaidi ya wanyama wengine.