ASILIMIA 96 ya Watanzania wanakubali utendaji wa Rais John Magufuli tangu alipoingia madarakani Novemba mwaka jana, huku asilimia 69 wakikubaliana na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano, hususan uondoaji wafanyakazi hewa huku elimu kuwa bure ikikubaliwa kwa asilimia 67 na asilimia 61 ikikubali kusimamishwa kazi kwa watumishi wa umma (kutumbuliwa kwa majipu).

Wakati asilimia 96 ya Watanzania wakikubali utendaji kazi wa Rais Magufuli tangu aingie Ikulu ya Magogoni, Dar es Salaam, Novemba 5, mwaka jana, asilimia 78 wanawakubali wenyeviti wa mitaa na kijiji, asilimia 74 wakikubali utendaji wa madiwani na wabunge wakiwa wa mwisho kwa kukubalika kwa asilimia 68.
Matokeo haya yametolewa na Taasisi ya Twaweza kwenye utafiti uitwao Rais wa Watu? Tathmini na matarajio ya wananchi kwa Serikali ya Awamu ya Tano.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze, muhtasari huo unatokana na takwimu kutoka Sauti za Wananchi, ambao ni utafiti wa kwanza barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaotumia simu za mkononi. Matokeo haya yanatokana na takwimu zilizokusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,813 kutoka maeneo yote Tanzania Bara (Zanzibar haihusiki kwenye matokeo haya) kati ya Juni 4 na 20, mwaka huu.
Aidha, wadau wameshauri ripoti hiyo kufanyiwa kazi zaidi, lakini pia wakibainisha kuwa ni taarifa inayotoa taarifa kama ni yapi ya kufanyiwa kazi zaidi kwa mustakabali wa Taifa.
Kuhusu wananchi kama wanawafahamu wawakilishi wao, Eyakuze alibainisha kuwa asilimia 98 ya wananchi wanafahamu utendaji wa Rais wao, asilimia 96 ikiwa ni kufahamu ofisa mtendaji wa kijiji, asilimia 92 kwa diwani na mbunge na asilimia 21 kwa mkurugenzi mtendaji wa wilaya.
Kuhusu wananchi kuwa na taarifa kiasi gani katika masuala ya siasa, alisema asilimia 61 ya wananchi hawana taarifa huku wenye nazo wakiwa ni asilimia nne tu.
Alisema wananchi waliohojiwa walisema (kwa nyakati tofauti) kuwa wana uzoefu wa kukutana na watendaji wa ngazi kama vile ofisa mtendaji lakini wachache wakiwa wanakutana na wabunge wa majimbo yao.
“Pale ambapo wananchi wameongea na viongozi wao, asilimia kubwa walizungumzia masuala ya kijamii badala ya masuala binafsi ama ya kitaifa,” alisema Eyakuze na kuongeza kuwa mara nyingi kukutana huko hutokea kwenye mikutano ya umma, majumbani au maofisini mwa viongozi wa ngazi ya kijiji na kata.
Mtendaji huyo alisema wananchi wengi wanasema Serikali ya Awamu ya Tano imeleta maboresho kwenye huduma nyingi za umma ikiongozwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuboresha huduma zake, huduma kuwa nzuri shuleni, vituo vya Polisi, mahakamani, vituo vya afya na mamlaka za maji.
Alisisitiza kuwa takwimu hizo zinaonesha mitazamo na maoni ya wananchi kuhusu huduma za umma na siyo lazima ikawa ndiyo hali halisi ya mabadiliko kwenye huduma hizo.
Akiizungumzia ripoti hiyo, Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), wachapishaji wa magazeti ya Daily News, HabariLeo, Sunday News, HabariLeo Jumapili na SpotiLeo, Dk Jim Yonaz alisema taarifa hiyo inaonesha kuwa wananchi hawana jambo wanalosema ni baya.
Alisema ripoti inatoa taarifa kwamba ni yapi ya kufanyiwa kazi na inatoa fursa kwa watendaji waliochaguliwa na Rais Magufuli kuhakikisha wanakubalika kama yeye mwenyewe alivyokubalika kulingana na ripoti.