VIONGOZI wa dini mkoani Kagera wameishauri serikali kushirikisha wananchi katika mchakato mzima wa kutathmini madhara, yaliyotokana na tetemeko la ardhi mkoani humo kwani mpaka sasa baadhi ya maeneo, hayajafikiwa na kufanyiwa tathmini, huku wakiomba misaada kwa waathirika iharakishwe.

Walitoa kauli yao jana wakati wakizungumza na gazeti hili katika maeneo mbalimbali ya nyumba za ibada, yaliyoathirika kutokana tetemeko hilo la Jumamosi wiki iliyopita ambalo lilisababisha vifo vya watu 17 na kuacha wengine majeruhi zaidi ya 200 na kubomoa nyumba zaidi ya 1,000.
Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Bukoba, Methodius Kilaini alisema wanapaswa kufanya tathmini mbili, kwanza ni ile ya haraka na kuwatafutia watu maeneo ya kulala kama vile mahema, chakula na dawa.
Ya pili kufanya tathmini ya kuhusu majengo na kutafuta njia ya kupata vifaa vya ujenzi ili kujenga majengo au nyumba imara.
Kilaini, Askofu KKKT, Pentekoste wanena “Sisi kama viongozi wa dini hatujaona watu wanakuja kufanya tathmini katika makanisa yetu yaliyoathirika, nyumba za mapadri wanalala zimeanguka, wakitaka tathmini ifanikiwe na kutoa majibu ya uhakika watushirikishe sisi jamii watu wanataabika sasa mvua inakuja watu wanalala nje, wengine hawafikiwi na wakiendelea hivyo bila kushirikisha jamii hali hiyo itachukua muda mrefu huku watu wakiendelea kuathirika,” alisema Askofu Kilaini.
“Sisi tumepata hasara kubwa kutokana na hili janga, kanisa letu la Ihungo limeharibika kabisa na kuanguka, nyumba ya kihistoria iliyojengwa mwaka 1940 iliyokuwa ikitumiwa na mapadri katika kanisa hilo la Ihungo imeanguka kabisa kwa hiyo lazima tujenge upya. Kanisa la kihistoria ambalo ni la kwanza mkoani Kagera lililojengwa mwaka 1892 na ndio chimbuko la dini yetu hapa Bukoba pia limeharibika kabisa, tunahitaji msaada wa haraka kulikarabati pia nyumba za mapadre pia zimeharibika kabisa,” aliongeza Kilaini.
Alisema mpaka sasa mapadri wa sehemu hizo mbili, wanalala kwenye magari, lakini jitihada za haraka zinafanyika za kuwajengea banda la kujihifadhi wakati wakitafuta ufumbuzi wa kujenga makanisa hayo mawili haraka kwani waumini wanasalia nje na hakuna mtu yeyote au taasisi waliofika kutathmini kuhusu majanga yaliyowapata.
“Kwa sasa tuna kikao kuna kamati imetoka Baraza la Maaskofu (TEC) ili kuona tunafanya nini kunusuru watu pia makanisa yetu mengine kumi yamepata nyufa kubwa,” alisema Kilaini na kuiiomba serikali, wafadhili mbalimbali kuwakumbuka wananchi wa Kagera walioathirika kwa kuwaletea misaada ya haraka hasa mahema ili wajikinge na mvua na baridi, hili ni janga limemgusa kila mmoja.
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Magharibi, Abedinego Keshomshahara katika tathmini ya mwanzo waliyoifanya, wamegundua makanisa 10 kati ya 248 yamepata nyufa kubwa, nyumba tatu za wachungaji zimepata nyufa, nyumba tano za wainjilisti zimepata nyufa, na nyumba za watenda kazi wao 25 pia zimeharibika, na hadi sasa hawajafanyiwa tathmini yoyote.
“Lakini hatuwezi kuilaumu serikali, hili tukio ni la ghafla kwani kila mtu anakimbia huku na huku kuona ni vipi watawasaidia waliothirika tunategemea tathmini kubwa itakuwa kwenye majumuisho ila la muhimu wananchi washirikishwe ili kutoa takwimu sahihi kwani wao ndio waathirika,” alisema Askofu Keshomshahara.
Naye Mwenyekiti wa Makanisa ya Kipentekoste, Mchungaji Edward Crodward alisema tetemeko limeathiri makanisa mengi ila hawajamaliza kufanya tathmini, ingawa tathmini ya mwanzo wamebaini makanisa saba yamepata nyufa kubwa.
Kauli ya Shehe wa Mkoa Shehe wa Mkoa, Haruna Kichwabuta alitaja athari walizozipata kutokana na tetemeko hilo kuwa ni misikiti mitatu mikubwa iliyoko Manispaa ya Bukoba, imeanguka kabisa na kusababisha kuifunga na hivyo waumini kuswalia nje, misikiti mingine minne imepata nyufa kubwa, ofisi mbili za Bakwata zimepata nyufa na miundombinu ya vyoo kuharibika.
Kichwabuta anashauri ifanyike tathmini ya kina bila kubagua wala kutazama taasisi fulani ili kufanikisha kazi hiyo na kusaidia kwani wote wanahitaji msaada wa haraka.
Wakati huo huo, wadau mbalimbali wameendelea kutoa misaada, na Serikali ya China imetoa vifaa mbalimbali yakiwemo madawa, nguo, maji na blangeti, Ubalozi wa Kuwait ukiwakilishwa na Shirika la African Muslim wamekabidhi msaada wa Sh milioni 22 zikiwa Sh milioni 12 taslimu na vifaa vya ujenzi na chakula vya Sh milioni 11, Serikali ya Zanzibar imekabidhi Sh milioni 50 na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Dayosisi ya Kaskazini Magharibi ikitoa msaada wa chakula kwa waathirika hao.
Wabunge wachanga milioni 85.5
Mjini Dodoma, wabunge wamekusanya Sh 85,580,000 ili kusaidia waathirika wa tetemeko la ardhi lililotokea mwishoni mwa wiki iliyopita mkoani Kagera. Michango hiyo imetokana na uamuzi wa wabunge kuridhia kuchangia posho zao za siku moja kila mmoja.
Hayo yalithibitishwa bungeni jana na Spika wa Bunge, Job Ndugai alipokuwa akitoa taarifa za michango ya wabunge wa Bunge ambao kwa ujumla idadi yao ni 389.
Wabunge hao, kwa kauli moja Jumanne wiki hii waliguswa na kuridhia kutolipwa posho ya siku, kiasi cha Sh 220,000 kila mmoja ili zisaidie waathirika wa tetemeko hilo lililosababisha vifo vya watu 17 na kujeruhi zaidi ya watu 252.
Mashirika ya umma yatoa zaidi ya mil 800/- Jijini Dar es Salaam, zaidi ya Sh milioni 800 zimechangishwa kutoka mashirika mbalimbali ya umma na taasisi za serikali kupitia harambee maalumu ya kuchangia waathirika wa tetemeko la ardhi lililotokea hivi karibuni mkoani Kagera.
Katika harambee hiyo iliyoongozwa na Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru, pia baadhi ya mashirika yaliahidi kutoa mchango wao kwa njia ya misaada ya kitaalamu kama vile wataalamu wa masuala ya ujenzi, wataalamu wa jiolojia na mazingira.
Akizungumza katika mkutano maalumu, ulioandaliwa na ofisi ya Hazina kwa ajili ya harambee hiyo Dar es Salaam jana, Mafuru alisema kutokana na maafa makubwa yaliyosababishwa na tetemeko hilo kwa wakazi wa Kagera ni jukumu la Watanzania wote kuungana na kutoa msaada kwa waathirika.
Aliyaomba mashirika hayo kuwasiliana na makatibu wakuu wao kupitia wizara walizopo ili kuangalia namna ya kupunguza matumizi yao na kuchangia waathirika hao wa tetemeko.
Katika michango hiyo iliyofikia zaidi ya Sh milioni 800, Kampuni ya Tanzania Standard Newspapers (TSN) wachapishaji wa magazeti ya Daily News, HabariLeo, HabariLeo Jumapili, Sunday News na SpotiLeo walichangia jumla ya Sh milioni tano pamoja na matangazo bure kuhusu maafa hayo ya Kagera kwa siku 30.
Meneja Uhusiano wa TSN, Badra Masoud aliyemwakilisha Mhariri Mtendaji wa kampuni hii Dk Jim Yonazi, alisema pia Kampuni ya TSN ilirusha moja kwa moja mkutano huo wa harambee kupitia tovuti za Daily News na HabariLeo.
Shirika la Habari la Utangazaji Tanzania (TBC), nalo lilichangia kiasi cha Sh milioni tano kutoa matangazo bure yanayohusu maafa hayo na kurusha mkutano huo wa harambee ya kuchangia waathirika hao moja kwa moja.
Baadhi ya kampuni, mashirika na taasisi nyingine za umma zilizochangia katika harambee hiyo ni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) (milioni 60), Benki Kuu ya Tanzania (BoT) (milioni 50), Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) (milioni 50) na Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB) (milioni 25).
Wengine waliochangia ni Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) (milioni 20), Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) (milioni 20), Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) (milioni 20), Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) (milioni 15), Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) (milioni 10) na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya NHIF (milioni 10).
Aidha taasisi, mashirika na kampuni nyingine za umma zilizochangia katika harambee hiyo ni Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) (milioni 10), Benki ya Posta Tanzania (TPB) (milioni 10), Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) (milioni 10), Wakala wa Majengo Tanzania (milioni 10) na Mamlaka ya Udhibiti wa Bima Tanzania (milioni 10).
Nyingine zilizochangia Sh milioni tano ni ofisi ya Msajili wa Hazina, Bodi ya Tumbaku (TTB), Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi na Huduma (VETA), Bodi ya Usajili wa Makandarasi na Chuo cha Bahari (DMI). Udsm, MSD, DIT, JKT kutoa utaalamu Aidha, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilisema kimetoa mchango wa kupeleka wataalamu wake wa masuala ya jiolojia mkoani Kagera ambao pamoja na kuendelea na utafiti kupitia kituo cha kufuatilia matetemeko kilichopo mkoani Geita, pia watafungua kituo mkoani Kagera kufuatilia zaidi hali ya matetemeko.
Kwa upande wa Bohari ya Dawa Tanzania (MSD) yenyewe imeahidi kusambaza dawa kwa waathirika hao zenye thamani ya Sh milioni 30, Chuo cha DIT kiliahidi kutoa msaada wa kitaalamu zaidi katika maeneo yaliyoathirika na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) nalo litatoa askari wake kwa ajili ya ujenzi.
Mapema wiki hii, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, pia aliitisha harambee ya wafanyabiashara kwa ajili ya kuchangia waathirika hao wa tetemeko na jumla ya Sh bilioni 1.4 ziliahidiwa kutolewa pamoja na misaada ya ujenzi wa taasisi mbalimbali ikiwemo shule zilizoathirika.
Aidha, serikali ilisema inalichukulia suala hilo kwa ukubwa wake na ndio maana, Rais John Magufuli aliahirisha safari ya kikazi Lusaka, Zambia kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais wa nchi hiyo, Edgar Lungu.
Wajenzi waombwa vifaa Nayo Idara ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu imeomba viwanda vinavyozalisha vifaa vya ujenzi, watoe msaada wa kuzalisha vifaa maalumu vyenye nembo Kagera na bei ndogo, ili vikawezeshe waathirika wa tetemeko Bukoba wajenge nyumba zao haraka.
Akizungumza jana jijini Arusha, Mkurugenzi Idara ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Brigedia Jenerali Mbazi Msuya katika mafunzo ya siku mbili ya wanahabari, mashirika yasiyo ya kiserikali na Asasi za Kiraia ya kuwajengea uwezo masuala ya maafa, alisema vifaa hivyo vizalishwe ndani ya miaka miwili.
Alisema kama bati au mfuko wa saruji ni vyema kuandikwa jina Kagera ili usiuzwe kokote ni huko na bei iwe ndogo, lakini sio hivyo tu ni vifaa vyote vya ujenzi vya Kagera. Aliomba wazalishaji washushe bei ya vifaa hivyo iwe chini na wasisingizie kodi ili kusaidia waathirika hao.
Aidha, alisema mpaka jana wagonjwa waliopo wodini 53 kati yao 21 wameshaonwa na madaktari bingwa kutoka China na baadhi watafanyiwa upasuaji.
Mwinyi kuongoza matembezi Naye Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi kesho ataongoza matembezi ya hiari ya kilometa tano, kuchangisha fedha kuwasaidia wananchi walioathirika na tetemeko la ardhi lililotokea mwishoni mwa wiki iliyopita mkoani Kagera.
Matembezi hayo yaliyoandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, yatashirikisha jumuiya ya wanadiplomasia, mawaziri, makatibu wakuu pamoja na wananchi.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mindi Kasiga alisema matembezi hayo yataanza saa 12 asubuhi katika Bwalo la Maofisa wa Polisi Oysterbay.
Kasiga alisema kiingilio katika matembezi hayo ni Sh 10,000, lakini wananchi wa kawaida wanaalikwa kuingia kwa fedha yoyote waliyonayo.
Alisema wanahamasisha kampuni, benki na taasisi mbalimbali kujitokeza kuchangia. Fedha zitakazopatikana zitapelekwa katika akaunti iliyofunguliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Imeandikwa na Angela Sebastian (Bukoba), Veronica Mheta (Arusha), Eric Anthony (Dodoma) na Theopista Nsanzugwanko na Halima Mlacha (Dar).