Mgombea wa chama cha Democratic nchini Marekani Bi Hillary Clinton amesema hakuficha taarifa za kuugua homa ya mapafu kwa kuwa hakudhani kama litakuwa jambo kubwa na la kusumbua.
Amekuwa akikosolewa kwa kushindwa kutoa taarifa zake mapema mpaka pale alipokaribia kuanguka mbele ya hadhara katika siku ya kumbukumbu ya shambulizi la Septemba 11.
Akihojiwa na shirika la habari la CNN, Bi Clinton amesema kuwa hakufuata vyema kile anachokiita ushauri wa madaktari wake wa kupumzika kwa siku tano baada ya kufanyiwa vipimo siku ya Ijumaa.
Timu yake ya kampeni imesema kuwa hana tatizo lolote la kiafya isipokuwa homa ya mapafu na kuongeza kuwa taarifa zaidi juu ya uimara wa afya yake zitatolewa.

Bi Clinton amesema kuwa hakufuata vyema ushauri wa madaktari wake kumpumzika siku tano
Image captionBi Clinton amesema kuwa hakufuata vyema ushauri wa madaktari wake kumpumzika siku tano

Mpinzani wake wa chama cha Republican Donald Trump,amesema kuwa anatumai Bi Clinton atapona hivi karibuni,na kuongeza kuwa ugonjwa wa mgombea huyo ni tatizo katika mbio za urais.
Trump amesema kuwa ofisi yake itatoa taarifa yake ya kiafya wiki hii.
Bi Clinton alionekana kudhoofu kiafya siku ya kukumbukumbu ya watu waliofariki katika shambulio la Septemba 11,ambapo aliondoka katika eneo hilo kwa msaada maalum wa walinzi wake.