AJALI na kero zinazosababishwa na usafiri wa bodaboda sasa umefika kikomo, hii ni kutokana na mageuzi makubwa yanayofanywa na Serikali kwa kushirikiana na madereva wa vyombo hivyo vya usafiri. Miongoni mwa mageuzi hayo ni kuandaa kanzi data maalumu kwa ajili ya kuwasajili madereva wote wa bodaboda ambao watapewa namba ya utambulisho.

Namba hiyo pamoja na jina la dereva ndio watakuwa kwenye kanzi data hiyo. Madereva pia watalazimika kuvaa sare muda wote wawapo kazini na namba yake ya utambulisho itakuwa kwenye hiyo sare.
Hiyo ni kurahisisha dereva huyo wa bodaboda kufahamika kirahisi pale atakapofanya kosa ili asiweze kuwakimbia polisi kama inavyofanyika sasa.
Abiria kabla ya kubebwa na bodaboda kupitia simu yake ya mkononi ataweza kuhakiki uhalali wa dereva wa bodaboda aliyemkodi kwa kutumia namba yake ya simu ya mkononi. Atafanya uhakiki huo kwa kuingiza namba iliyoko kwenye sare na matokeo yake ataletewa jina na picha ya dereva aliyemkodi.
"Lengo la kufanya hivyo ni kuondokana na vitendo vya baadhi ya madereva wenzetu kuwafanyia vitendo vya kihuni abiria wao ikiwemo kuwaibia. Lakini pia tunataka kila dereva apitia mafunzo ya udereva na awe na leseni yake.
"Lengo la kuleta mageuzi hayo ni kutaka kuhalalisha usafiri wa bodaboda ili uwe rasmi, lakini pia uwe wa heshima kuliko ilivyo sasa. Uzinduzi rasmi wa mfumo huu mpya utafanyika Oktoba 18 mwaka huu," amesema Mwenyekiti wa Umoja wa Madereva wa Bodaboda mkoani Dar es Salaam, Michael Masawe.
Masawe alikuwa akizungumza mwishoni mwa wiki kwenye Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Jumuiya ya Madaktari wanaofanya kazi katika hospitali za makanisa ya Kikristo (TCMA). Katika mkutano huo suala la ajali za bodaboda lilijadiliwa kwa kina na madaktari hao.
Masawe pia alisema hatua hiyo itapunguza madereva wa bodaboda kutumika kwenye vitendo vya ujambazi.
Mageuzi hayo ya usafiri wa bodaboda yanafanywa kwa ushirikiano kati ya Chama cha Bodaboda mkoani Dar es Salaam, Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), Kikosi cha Polisi cha Usalalama Barabarani kwa kushirikiana na manispaa tatu za jijini Dar es Salaam.
Masawe alisema katika mageuzi hayo, kila kijiwe au kikundi kitasajiliwa rasmi kwenye manispaa husika na kwenye kanzi data na itakuwa inaonesha idadi ya madereva waliopo kwenye kijiwe hicho na majina yao. Pia alisema kila kijiwe kitakuwa na viongozi ambao watahakikisha taratibu mpya zilizoandaliwa zinatekelezwa na madereva wote.
"Kazi ya kiongozi ni kuhakikisha madereva wote wako kwenye sare zenye namba na pia amevaa mavazi yote yanayotakiwa wakati wa kuendesha bodaboda," alisema Masawe na kuongeza kuwa hakuna dereva wa bodaboda ambaye ataruhusiwa kuvaa ndala au makubadhi.
Mkurugenzi wa Barabara wa Sumatra, Johansen Kahatano alisema mpango huo wanaoufanya kwa kushirikiana na Chama cha Bodaboda mkoani Dar es Salaam uko katika hatua za mwisho kukamilika na sasa kuna baadhi ya mambo yako katika hatua za mwisho. Alisema wanaanzia Dar es Salaam na baadaye mpango huo utapelekwa pia mikoani.
Alisema wanakamilisha kusajili vituo vya bodaboda vyote vya jijini Dar es Salaam pamoja na kuandaa kanzi data ya vituo vyote vya bodaboda ili asiwemo dereva ambaye watamwacha nje ya mfumo huo ambao unalenga pia kuhakikisha kila dereva anapitia mafunzo na kupatiwa leseni.
"Dereva ambaye atajifanya mjanja na akashindwa kujisajili kwenye vikundi kazi ambayo tunaifanya kwa sasa, huyo hataruhusiwa kuendesha pikipiki, tunamshauri akatafute kazi nyingine," alisema Kahatano.
Mkuu wa Usalama Barabarani mkoa wa Temeke, Mrakibu Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Solomon Mwangamilo alisema trafiki wanalazimika kuwakamata bodaboda kwa kutumia nguvu kwa vile hawataki kusimama pale wanaposimamishwa.
"Kama polisi wasingekuwa wanafanya hiki kinachoitwa harrasment (nguvu) nadhani hali ingekuwa mbaya zaidi, sisi tunafanya ukamataji kutokana na usalama wao," alisema ASP Mwangamilo.
Mwangamilo alisema ni vizuri mfumo huo wa usafiri ubadilike, kwani ilivyo sasa ni bodaboda wenyewe wanawalazimisha polisi wawakamate kwa nguvu kwani hawataki kutii hata kama kuna msafara wa kiongozi.