MAAFA zaidi yameripotiwa katika janga la tetemeko la ardhi, lililotokea juzi mkoani Kagera, ambapo imeripotiwa idadi ya vifo kuongezeka na kufikia watu 16, huku wengine 253 wakijeruhiwa na kusababisha simanzi na masikitiko kwa familia nyingi. Katika tukio hilo, pia nyumba 840 za makazi zimeanguka, nyumba 1,264 zimepata nyufa kubwa na majengo 44 ya taasisi mbalimbali zikiwemo shule yameanguka.
Tukio hilo limemfanya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kulazimika kufanya ziara ya ghafla ya kuwatembelea waathirika wa tetemeko hilo, ambalo limedaiwa kusababisha tafrani pia katika nchi jirani za ukanda wa Afrika Mashariki za Kenya na Rwanda.
Katika hatua nyingine, Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela kilichopo eneo la Tengeru, mkoani Arusha kimeeleza mpango wa kuanza kufunga vifaa vitakavyotoa ishara ya matukio ya matetemeko ya ardhi kabla majanga hayo kutokea.
Katika mradi huo maalumu chini ya Kitengo cha Utafiti wa Miamba na Volcano, chuo hicho kitashirikiana na taasisi mbalimbali za elimu ya juu zilizopo Ulaya na Marekani, hasa Chuo Kikuu cha Glasgow kilichopo Scotland, kwa mujibu wa Makamu Mkuu wa taasisi hiyo, Profesa Burton Mwamila. Ziara ya Waziri Mkuu
Akitoa taarifa kwa Waziri Mkuu jana katika Uwanja wa Kaitaba ulioko mjini Bukoba ambapo umeandaliwa maalumu kwa ajili ya kuaga miili ya watu waliopoteza maisha katika tukio hilo la kusikitisha, Mkuu wa Mkoa, Meja Jenerali mstaafu Salum Kijuu alisema tukio hilo ni la kwanza kutokea mkoani humo na kwamba limeleta madhara makubwa kwa wananchi na kuacha majonzi makubwa.
Kijuu alisema mpaka taarifa inaandaliwa watu 16 waliripotiwa kupoteza maisha na kusababisha majeruhi 253, huku 170 wakiwa wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo na 83 wakitibiwa na kuruhusiwa.
Alisema pia tetemeko hilo limesababisha nyumba 840 za makazi kuanguka, nyumba 1,264 kupata nyufa kubwa na majengo 44 ya taasisi mbalimbali zikiwemo shule kuanguka.
Alisema tetemeko hilo lenye ukubwa wa alama 5.7 uliopimwa kwa kipimo cha Ritcher cha kisayansi cha kupima matetemeko, limeleta madhara makubwa ambapo Serikali ya Mkoa inaendelea kutathmini kwa kina athari zaidi zilizosababishwa na tetemeko hilo na pia uharibifu uliojitokeza kisha kupeleka katika Ofisi ya Waziri Mkuu waone jinsi ya kusaidia.
Alisema hatua zilizochukuliwa na mkoa mpaka sasa ni kuwaokoa na kuwapeleka watu hospitali kwa ajili ya matibabu na kuwapatia makazi ya muda baadhi ya wananchi wenye nyumba zilizoathirika, wakati mipango mingine ikiandaliwa.
Taarifa hiyo ya Mkuu wa Mkoa, ilimfanya Waziri Mkuu kueleza masikitiko yake na serikali kutokana na janga hilo na kutoa salamu za pole kwa wananchi waliopatwa na madhara na kuwatembelea wagonjwa waliolazwa katika Hospitali ya Mkoa na pia maeneo yote yaliyoathirika.
"Leo si siku nzuri kwetu, nimekuja kumwakilisha Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye anawapa pole sana wana Kagera wote na Watanzania kwa ujumla. Pia Makamu wa Rais anawapa pole kwa msiba huu mkubwa, lengo la safari yangu ni kuja kuwapa pole, tukio hili ni kubwa na halijawahi kutokea Tanzania, tumekuwa tukisikia kutoka mataifa ya nje lakini leo limetupata nchini kwetu," alisema Majaliwa.
Aliwasihi na kuwataka wananchi kuwa wavumilivu, kuonesha umoja na ushirikiano, lakini pia kujitokeza kuwafariji wenzao wakati wote wa majonzi, huku akisema Watanzania kwa miaka mingi wamekuwa wakishuhudia mitikisiko midogo, lakini juzi tumeshuhudia mtikisiko mkubwa kabisa ambao umeleta madhara makubwa kwetu.
"Mpaka sasa hatuna uhakika mtikisiko huu utakuwa endelevu kwa kiasi gani, nataka niwahakikishie Watanzania wote, Serikali tunafanya mawasiliano na taasisi zenye uwezo wa kubaini mtikisiko huu ili tuweze kujua jambo hili litakuwa endelevu kwa kiasi gani na kuona dalili na ukubwa wake utakuwaje ili tujipange katika kutoa elimu lakini pia tahadhari pindi jambo kama hili linapoweza kutokea au tunapoona viashiria au dalili za jambo hili," alisema Waziri Mkuu.
Alisema kuwa Mkuu wa Mkoa katika taarifa yake alimweleza kwamba tathmini inaendelea na kwamba ameiagiza Kamati ya Maafa ya Ofisi ya Waziri Mkuu kufika mkoani Kagera mara moja na kuzunguka mkoa mzima kwa kushirikiana na uongozi wa mkoa kwa lengo la kufanya tathmini ya jumla.
Alisema baada ya tathmini hiyo, utaratibu utafuatwa kwani serikali haiwezi kuwatupa mkono wananchi hao, pia alitumia fursa hiyo kuwaambia wafiwa kuwa Watanzania nchini kote wako pamoja nao katika janga hilo.
Akielezea mkasa huo, majeruhi Happines Apolinary ambaye ni mkazi wa kata ya Buyekera aliyelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Kagera kwa kuumia kichwani na mgongoni, alisema alishtuka kusikia mtikisiko mkubwa wakati akiwa ndani ya nyumba yake na ghafla aliangukiwa na kuta na kumsababishia majeraha. Pamoja na kueleza kuumia vibaya kutokana na tukio hilo, Happines aliwashukuru wafanyakazi wa Hospitali ya Mkoa wa Kagera kwa huduma nzuri waliyompatia tangu juzi alipofikishwa hospitalini hapo.
Majeruhi mwingine, Paulina Spilian aliyelazwa hospitalini hapo akiwa amejeruhiwa miguu alisema akiwa ndani ya nyumba yake ghafla alisikia mtikisiko mkubwa ulioambatana na kishindo cha kuanguka kwa kuta za nyumba na akiwa katika harakati za kutaka kukimbia nje aliangukiwa na ukuta miguuni.
Majeruhi huyo aliiomba Serikali kuwasaidia kwa kuwajengea nyumba na pia kuwapa elimu kuhusiana na matukio kama hayo ili waweze kujiokoa baada ya kuona dalili au viashiria tofauti na ilivyotokea juzi.
Advela Respicius ambaye ni mama wa marehemu, Verdiana Respicius aliyekufa baada ya kufunikwa na kifusi cha nyumba, akizungumza kwa niaba ya familia za wafiwa wa tukio hilo, alitoa shukrani kwa serikali kwa kutoa majeneza, sanda na usafiri wa kuwapeleka marehemu hao mpaka vijijini kwa ajili ya maziko.
Vifaa vya kutabiri kufungwa Wakati hofu ikiwa bado imetawala kutokana na tukio hilo hasa kutokana na wananchi wa Kagera kueleza kutofahamu lolote kabla ya kutokea kwa tetemeko kutokana na kutopewa taarifa zozote na mamlaka za serikali, Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela kilichopo eneo la Tengeru, mkoani Arusha kimesema kinatarajia kuanza kufunga vifaa vitakavyotoa ishara ya matukio ya matetemeko ya ardhi kabla majanga hayo kutokea.
Katika mradi huo maalumu chini ya Kitengo cha Utafiti wa Miamba na Volcano, chuo hicho kitashirikiana na taasisi mbalimbali za elimu ya juu zilizopo Ulaya na Marekani, lakini hasa Chuo Kikuu cha Glasgow kilichopo Scotland, kwa mujibu wa Makamu Mkuu wa taasisi hiyo, Profesa Burton Mwamila.
Katika mradi huo wa kwanza nchini unaolenga kutoa utabiri wa matukio ya matetemeko na ulipukaji wa volcano nchini, vifaa maalumu vitakavyokuwa vinapima uwezekano wa kutokea majanga hayo, vitafungwa katika maeneo nyeti kama milima, vilima na sehemu ambazo huwa na volcano hai.
Mtaalamu wa miamba ambaye pia ni Mkuu wa Taasisi ya 'Eco Science' inayoshughulika na utafiti wa miamba pamoja na milipuko ya volcano, Dk Ben Beeckmans amefafanua kuwa 'Mlima wa Mungu' (Oldonyo Lengai) uliopo eneo la Ngaresero, wilayani Ngorongoro ndio chanzo kikubwa cha matetemeko ya ardhi katika eneo lote la Afrika Mashariki. Mlima huo wenye volkano hai pia umekuwa ukilipuka mara kwa mara na tukio la mwisho lilirekodiwa mwaka 2007.
Vifaa hivyo vya kutabiri matetemeko ya ardhi vitafungwa kuzunguka eneo la mlima huo, Ziwa Natron, Mlima Meru na hata Mlima Kilimanjaro pamoja na maeneo mengine nchini.
Lakini hatua hiyo si kwamba imetokana na matukio ya tetemeko yaliyoyakumba maeneo mengi ya nchi juzi bali ni mpango uliobuniwa na wataalamu mapema mwaka huu na kwamba kilichobaki ni utekelezaji tu.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST), Karimu Meshaki alisema atatoa taarifa rasmi kuhusu maendeleo ya mpango huo wiki hii.
Hivi karibuni Serikali ilijenga maabara kubwa kabisa ya utafiti wa kisayansi katika Chuo cha Nelson Mandela, Arusha ambayo ilizinduliwa miezi miwili iliyopita.
Serikali ya India pia ilitoa mchango wake kwa kukipatia chuo hicho kompyuta kubwa na yenye uwezo mkubwa zaidi nchini ijulikanayo kama 'Param Kilimanjaro,' ambayo pamoja na shughuli nyingine pia inatarajiwa kutumika katika tafiti za miamba, gesi asilia na pia kwenye huu mradi mpya wa kufuatilia matukio ya tetemeko la ardhi na milipuko ya volkano.
|
0 Comments