Mkuu wa tume ya kupambana na rushwa Kenya (EACC) Philip Kinisu, amejiuzulu siku moja baada ya kamati ya bunge kupendekeza afutwe kazi kwa sababu ya muingiliano ya maslahi.
EACC ilikuwa inatakiwa ifanye uchunguzi kuhusu tuhuma za ufisadi katika Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) ambayo hufadhiliwa na serikali.

Lakini kampuni ambayo inamilikiwa na Bw Kinisu inadaiwa kushiriki katika shughuli za kibiashara na NYS.
Wabunge walikuwa wamemuomba Rais Uhuru Kenyatta aunde jopo la kumchunguza, na kuamua iwapo anafaa kufutwa kazi.
Bw Kinisu, ambaye ni mwenyekiti wa zamani ya kampuni ya wahasibu ya PwC Afrika aliteuliwa kuongoza tume hiyo Novemba mwaka jana.
Amesisitiza kwamba hana hatia na kusema badala yake watu wanafaa kuangazia "ufisadi".
Kuondoka kwake kutamfanya kuwa mkuu wa tume ya kupambana na rushwa Kenya aliyehudumu kwa kipindi kifupi zaidi.
Watangulizi wake wawili waliondolewa kazini baada ya kukabiliwa na tuhuma na shutuma, zikiwemo kutowajibika kazini.