WASTANI wa Sh milioni mbili zinatumika kumtibu majeruhi mmoja wa pikipiki, jambo ambalo limezifanya hospitali zinazowapokea majeruhi hao, kuzidiwa na gharama hizo za matibabu.
Madaktari kutoka Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) wamesema kwamba kwa sasa kila siku, wanapokea wastani wa majeruhi kati ya 50 na 60, jambo ambalo linaiwia vigumu taasisi hiyo kutoa huduma za uhakika kwa majeruhi hao.
Gharama hizo zinatokana na vyuma vinavyotumika kuwatibu majeruhi wa mifupa mirefu kuagizwa nje ya nchi, jambo ambalo linaelezwa na madaktari kwamba kutokana na idadi ya majeruhi kuongezeka kila siku, inailazimu MOI kukabiliwa na upungufu wa vifaa hivyo.
Kutokana na kuongezeka kwa majeruhi hao wa bodaboda, Jumuiya ya Madaktari Wakristo (TCMA) wametumia mkutano wao wa mwaka uliomalizika juzi, kujadili jambo hilo na kueleza kuwa ajali zinazotokana na bodaboda ni janga la taifa kutokana na kuziongezea gharama za upasuaji hospitali.
Kwa hali hiyo, wameziomba mamlaka za masuala ya usalama barabarani, kuhakikisha zinatunga sheria kali zitakazowabana wapanda na waendesha bodaboda ili kuepusha taifa kuwa na walemavu wengi wa ajali za vyombo hivyo vya usafiri.
Madaktari kutoka MOI katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam, walisema taasisi hiyo kwa sasa imelemewa na majeruhi wa bodaboda, jambo ambalo linafanya vifaa na miundombinu ya taasisi hiyo, kutotosheleza mahitaji na hivyo kufanya gharama zinazotolewa kwa majeruhi hao kuwa hafifu.
Madaktari hao katika mkutano wao wa mwaka wa 79 ambao ulimalizika juzi kwenye ukumbi wa AMECEA, Dar es Salaam, waliwaita wadau mbalimbali wakiwemo madereva wa bodaboda, Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), polisi wa Usalama Barabarani, madaktari, maofisa wa Shirika la Afya Duniani (WHO) na waandishi wa habari, kujadili namna gani taifa linaweza kupunguza ajali za bodaboda.
Rais wa TCMA, Dk Isaya Tosiri alisema wamelazimika kutumia mkutano huo kujadili ajali zinazotokana na bodaboda kwa sababu hospitali ambako wanafanya kazi madaktari hao Wakristo zimelemewa kutokana na kupokea majeruhi wengi wa pikipiki.
"Kwa kweli hospitali zetu za makanisa zinapokea sana majeruhi wengi wa bodaboda, kila daktari aliyeko hapa analalamika kuongezeka kwa majeruhi huku hospitali zetu hazina uwezo wa kuhimili ongezeko hili, ndio maana tunasema ni janga la taifa ni lazima wadau watafute suluhisho," alisema Dk Tosiri.
Daktari Bingwa wa Hospitali ya Rufaa ya Nkinga, Yohana Masota iliyoko mkoani Tabora alisema katika hospitali yake wanapokea wastani wa majeruhi 10 kila siku ambao wanatokana na ajali za pikipiki jambo ambalo linafanya hospitali hiyo kuwa na mzigo wa kutibu majeruhi.
"Naamini kwamba ajali nyingi zinatokana na madereva hawa kutokuwa na uelewa wa sheria za barabarani ndio maana wanapata ajali mara kwa mara, ni lazima hatua zichukuliwe maana hospitali zetu zinalemewa," alisema Dk Masota.
Daktari Bingwa wa MOI, Victoria Munthali amesema zamani kabla ya kuruhusiwa kwa bodaboda kubeba abiria wa biashara, taasisi yake ilikuwa inapokea majeruhi wasiozidi watano kwa siku na siku ambako kuna ajali ya basi waliweza kupokea wastani wa majeruhi 10 kwa siku.
"Lakini siku hizi tunapokea wastani wa majeruhi kati ya 50 na 60 kwa siku, miundombinu ni ile ile hivyo uwezo wetu wa kuwahudumia unakuwa mdogo," amesema Dk Munthali.
Ameongeza kuwa hata vifaa kama vyuma, ambavyo ndivyo vinavyotumika kuwatibu majeruhi wa mifupa mirefu, kifaa cha gharama za chini kinauzwa dola za Marekani 70 (takribani Sh 147,000)
"Kwa wale ambao wanavunjika mgongo 'screw' zinazotumika kuwatibu ya gharama za chini ni dola za Marekani 200 (sawa na Sh 420,000).
Dk Boniface Respicious ambaye ni daktari bingwa wa mifupa wa MOI, alisema gharama za kumtibu majeruhi mmoja wa ajali ya bodaboda ni Sh milioni 2 jambo ambalo limefanya hospitali nyingi kulemewa na mzigo wa majeruhi.
Amependekeza kuanzishwe mfuko maalumu wa majeruhi kama ilivyo kwa mifuko mingine ya umeme vijijini (Rea) ambao utasaidia kutibiwa kwa majeruhi wa ajali za bodaboda na magari.
Alisema fedha za mfuko huo zikatwe wakati mmiliki wa gari au bodaboda anapoenda kukata leseni ya matumizi ya barabarani kama inavyofanyika sasa kwa Zimamoto.
"Hizi kampuni za bima hazisaidii lolote kwenye matibabu wakati wanachukua fedha nyingi, nadhani ukianzishwa mfuko wa majeruhi utaisaidia serikali kuwa na fedha za kutosha za kutibu majeruhi na itasaidia kupunguza mzigo ulioko kwenye hospitali zetu," alisema Dk Respicious.
Alisema kwa sasa huduma za kuwatibu majeruhi zimedorora katika hospitali nyingi kutokana na kukosa fedha za kununulia vifaa pamoja na dawa kutokana na ongezeko la majeruhi wa bodaboda.
Mkurugenzi wa Huduma za Afya, Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii, Dk Josphine Ballati alisema vifo vinavyotokana na ajali za bodaboda ni nyingi kuzidi vifo vinavyosababishwa na baadhi ya magonjwa.
"Huu ni ugonjwa mwingine ambao taifa letu limepata, lazima tutafute suluhisho."
Alionya kuwa kama taifa halitachukua hatua, miaka 20 ijayo nguvu kazi nyingi za taifa watakuwa ni walemavu kutokana na usafiri wa bodaboda kutumiwa na watu wengi. Alisema pia hatua zichukuliwe, kuhakikisha zinalipunguzia gharama taifa kuwatibu majeruhi hao.
Mkurugenzi wa Barabara wa Sumatra, Johansen Kahatano alisema imekuwa ngumu kuwadhibiti madereva wa bodaboda kwa sababu vijana wengi wanaofanya biashara hiyo ni wale ambao walikuwa na tabia za ajabu huko nyuma.
"Hawa ni vigumu kujifunza na kama wakijifunza ni ngumu kuelewa," alisema Kahatano na kusisitiza kuwa serikali inafanya jitihada kufanya usafiri huo baadaye uwe na heshima na kupunguza matatizo ya sasa.
|
0 Comments