SHERIA inakuja itakayowadhibiti wanaume waliozoea kula njama na wathamini ili washushe ama kupandisha thamani ya mali za wanandoa kwa nia ya kuwapunja akinamama katika mgawanyo wa mali za wanandoa.
Iwapo Muswada wa Sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini ya mwaka 2016 utapitishwa, moja ya kazi yake itakuwa kuwadhibiti baadhi ya wathamini waliozoea kula njama na wanaume hao ili kushusha ama kupandisha thamani ya mali za wanandoa nia ikiwa kuwapunja wanawake katika mgao wa mali za wanandoa.
Akitoa hotuba yake Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi wakati akiwasilisha Muswada wa Sheria ya Uthamini na Usajili Wathamini Mwaka 2016 alisema dawa ya wanaume waliozoea kudhulumu wanawake mali za wanandoa imepatikana.
“Tena hapa nataka wanawake mnisikilize sana, sasa Sheria hii itawadhibiti baadhi ya wathamini waliozoea kufanya mchezo huu wa kula njama na wanaume, jambo ambalo limekuwa likisababisha migogoro mingi katika familia na jamii,” alisema.
Akiunga mkono kipengele hicho, Mbunge wa Viti Maalumu, Sophia Simba (CCM), alisema kumekuwepo na migogoro mingi linapokuja suala la kugawana mali wanandoa baba na mama na kwamba wanawake wamekuwa wakionewa zaidi kwani kuna wathamini wasiokuwa waaminifu wanaocheza ‘deal’ na akinababa kuwadhulumu wanawake.
“Kuna haja ya akinamama kuelimishwa na kufahamu kuhusu sheria hizi… nawaomba wabunge wenzangu wanawake tutoke tukawaelimishe wanawake wenzetu ili wasidhulumiwe,” alisema.
Mbunge wa Ushetu, Eliasi Kuandikwa (CCM), alisema sheria hiyo itaondoa pia migogoro ya mirathi ikiwa ni pamoja na kuchukua muda mrefu lakini sasa itakuwa rahisi mali kufanyiwa uthamini haraka na mirathi kutoka hasa inayohusiana na mali.
Kwa mujibu wa Lukuvi, sheria hiyo pia imelenga kuwaondolea mateso, kero na migogoro wananchi wanaothaminiwa mali zao na kuchelewa kulipwa fidia kwa kuweka ukomo wa muda ambao fidia lazima ilipwe pamoja na kuwadhibiti wawekezaji wote kulipa fidia kwa wakati.
Hii itapunguza migogoro ya fidia ambayo imekuwa kero kubwa kwa wananchi ambao ardhi yao imekuwa ikichukuliwa kwa ahadi ya kulipwa fidia na hailipwi kwa wakati; itawachuja na kuwaondoa sokoni wathamini wote ambao hawana sifa, matapeli na wadanganyifu ambao muda mrefu wamekuwa wakilitia hasara Taifa.
Hata wale wathamini waliozoea kufanya uthamini wa kifisadi kushusha thamani ya mali kwa madhumuni ya kukwepa kodi stahili na waliozoea kuongeza thamani wafidiwa hewa katika jedwali la fidia sheria hiyo sasa inakwenda kuwadhibiti kwani serikali imekuwa ikipata hasara kubwa.
Waziri Lukuvi alibainisha pia chini ya sheria hiyo, wathamini watakuwa chini ya usajili unaoeleweka na itakuwa rahisi kuwawajibisha wathamini wote watakaokiuka maadili ya kitaaluma, kutoa adhabu kwa wathamini wanaokiuka sheria ikiwa ni pamoja na kifungo gerezani, faini kali, kusimamishwa au kufutiwa usajili.
|
0 Comments