Kaimu Katibu Tawala mkoani Mwanza, Projestus Rubanzibwa, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Mwanza, kwenye kikao cha Utambulisho wa Mradi wa kuongeza Ujuzi na Idadi ya Wakunga katika maeneo ya Vijijini katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na Kanda ya Magharibi, kilichofanyika hii leo Jijini Mwanza.


Amesisitiza kwamba Wakuu wa Vyuo vya vya Ukunga nchini wanao wajibu wa kuhakikisha kwamba wanatoa mafunzo bora kwa wahitimu wa vyuo hivyo ili watakapohitimu masomo yao waweze kusaidia kutoa huduma bora afya.

Mradi wa kuongeza Ujuzi na Idadi ya Wakunga katika maeneo ya Vijijini, unatekelezwa na Shirika la Jhpiego kwa kushirikiana na Taasisi ya Wakunga nchini Canada, Shirika la Amref, Serikari ya Canada, Taasisi ya Wakunga Tanzania na Wizara ya Afya nchini, lengo likiwa ni kuboresha huduma za afya kwa akina mama na mtoto ili kutokomeza vifo vitokanavyo na uzazi maeneo ya Vijijini nchini.
Na BMG
Kaimu Mganga Mkuu mkoa wa Mwanza, Dr.Silas Wambura, akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu mkoa wa Mwanza, ambapo amesema mkoa wa Mwanza unakabiriwa na upungufu mkubwa wa idadi wa wakunga pamoja na vifaa tiba hali ambayo inasababisha kuwepo kwa vifo vya akina mama na watoto.
Dr.Dustan Bishanga ambaye ni Mkurugenzi wa huduma za Mama na Mtoto Shirika la Jhpiego, amesema lengo la mradi huo ni kuhakikisha unaongeza Ujuzi na Idadi ya Wakunga maeneo ya Vijijini hapa nchini ambapo wahitimu wa masomo ya Sayansi katika maeneo hayo watakuwa wakipewa ufadhiri wa masomo kwa makubaliano ya kurudi kwenye maeneo yao ili kutoa huduma za afya. Mradi huo unatarajiwa kufikia tamati mwaka 2021.
Kikao cha Utambulisho wa Mradi wa kuongeza ujuzi na idadi ya Wakunga katika maeneo ya Vijijini mikoa ya Kanda ya Ziwa na Kanda ya Magharibi kilichofanyika hii leo Jijini Mwanza.
Dr.Dustan Bishanga ambaye ni Mkurugenzi wa huduma za Mama na Mtoto Shirika la Jhpiego, akizungumza na wanahabari kwenye kikao hicho.
Martha Rimoy ambaye ni Mratibu wa Taifa wa Chama cha Wakunga Tanzania (TAMA), amesema bado maeneo mengi nchini yanakabiloiwa na upungufu wa Wakunga kutokana na idadi ya Wakunga wanaohitimu vyuoni kutoendana na idadi ya ujenzi wa Zahanati na Vituo vya Afya huku wengine pia wakishindwa kwenda kufanya kazi maeneo ya Vijijini kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mazingira duni.
Gustav Moyo ambaye ni Mkurugenzi wa huduma za Uuguzi na Ukunga, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, amesema hali ya upungufu wa Wakunga nchini hususani maeneo ya Vijijini si nzuri hivyo Serikali inatumia jitihada mbalimbali ikiwemo kuhamasisha wanafunzi kusoma masomo ya Sayansi ili kutatua changamoto hiyo. 

Amesema asilimia kubwa ya mikoa ya Kanda ya Ziwa inakabiliwa na upungufu huo na kwamba Serikali itakuwa ikitolea kipaumbele kwenye mikoa hiyo pindi inapotoa ajira kwa Wakunga.
Kikao hicho kimewajumuisha wadau mbalimbali wa afya wakiwemo Wakunga, Waganga Wakuu wa Wilaya na Maafisa Elimu ambao watakuwa na wajibu wa kuwahamasisha wanafunzi kusoma masomo ya Sayansi ili kuongeza idadi ya Wakunga.
Wadau wa afya kutoka Mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Geita, Tabora, Kigoma na Mara wameshiriki kwenye kikao hicho.