BUNGE limeelezwa kuwa Rais John Magufuli hajavunja sheria yoyote kwa kuzuia siasa za hovyo, iliyotafsiriwa kuwa amefuta siasa nchini, bali kwa kufanya hivyo ameiheshimu, ameihifadhi na kuilinda Katiba ya nchi.
Aidha, wanasiasa na watu wengine wanaodhani Rais amevunja sheria, wameshauriwa kwenda mahakamani au kudai majadiliano na Rais.

Hayo yalisemwa juzi jioni mjini Dodoma na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe alipokuwa anahitimisha mjadala wa Muswada wa Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa wa Mwaka 2016, aliouwasilisha bungeni na kujadiliwa kwa siku mbili mfululizo.
Mwakyembe alilazimika kuyasema hayo baada ya wabunge wa kambi ya upinzani, kuwashambulia waziri huyo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju kuwa hawaungi mkono muswada uliowasilishwa bungeni kwa kuwa una nia ovu.
“Dk Mwakyembe huyu huyu ndiye aliyetetea kauli ya Rais Magufuli ya kuzuia mikutano ya hadhara wakati anajua inakubalika kikatiba,” alisema Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema aliyeungwa mkono na Mbunge wa Momba, David Silinde na Mchungaji Peter Msigwa wa Iringa, wote wa Chadema.
Akijibu, Dk Mwakyembe alisema ni vyema wakaacha kuingilia utendaji wa Rais Magufuli na wasaidizi wake, kwani hawana mamlaka hiyo na kwamba kama wanadhani wanaonewa, wana njia ya kutafuta haki kupitia Mahakama.
“Mimi sikujua mkuki kwa nguruwe binadamu mchungu, jana mliongea nikawasikiliza tulieni na mimi leo niwaeleze na nijibu hoja zenu,” alisema na kuongeza kuwa hawezi kubishana nao kwani anatilia mashaka usafi wao katika siasa, kwani walizunguka nchi nzima kumtangaza Edward Lowassa kuwa ni fisadi, lakini alipohamia kwao akageuka `malaika’ wanayemlamba nyayo zake.
Baada ya kauli hizo, alisisitiza Rais Magufuli hajavunja, sheria wala Katiba katika kupeleka muswada huo, bali alichokifanya ni kuzuia siasa za shari zisisambaratishe taifa.
Waziri huyo alisema alitegemea busara ya chama chochote kwenda mahakamani au kufanya majadiliano na serikali, Mwanasheria Mkuu au waziri mhusika, lakini hakuna mtu yeyote aliyekwenda mpaka Muswada huo unaletwa bungeni kupitishwa.
Kauli kama ya Mwakyembe ilitolewa pia na Mwanasheria Mkuu, George Masaju aliyehoji ni kifungu gani cha Katiba kilichokiukwa na Rais na kutaka wanaoamini wako sahihi, ni vyema wakafuata mkondo wa Sheria na kwenda kushitaki mahakamani.