WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesema serikali imelipa Sh trilioni 1.2 kwa makandarasi wenye madeni yao ya nyuma na mapya.
Ameagiza makandarasi hao kurejea haraka katika maeneo ya ujenzi wa miradi ya barabara na madaraja na kuanza kazi hizo kwa kasi, wasiotekeleza watanyang’anywa zabuni zao na kutopewa zabuni nyingine tena nchini.

Amesema Serikali ya Awamu ya Tano, itahakikisha barabara zote zinazojengwa katika kiwango cha lami, zinakamilishwa kwa muda uliowekwa na katika ubora wa hali ya juu, hivyo makandarasi wote walipewa zabuni kufanya kazi zao kwa kasi ya ‘Hapa Kazi Tu’ na si vinginevyo.
Profesa Mbarawa alitoa kauli hiyo juzi wakati alipofanya ziara ya kushitukiza katika mradi wa ujenzi wa barabara ya Magole- Turiani kwa kiwango cha lami pamoja na daraja kubwa la Divue ambalo ujenzi wake ulisimama tangu Septemba 2014 hadi ulipoanza tena Juni mwaka huu.
Akiwa katika ukaguzi huo, alimtaka mkandarasi wa Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) kutoka China, kuongeza kasi ya ujenzi wa barabara Magole- Turiani yenye urefu wa kilometa 48.6 kutokana na udhaifu aliouonesha katika ujenzi wake, ama sivyo serikali itamnyang’anya kandarasi hiyo.
Awali, Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Mkoa wa Morogoro (Tanroads), Godwin Andalwisye akitoa taarifa kwa waziri, alisema mradi wa barabara ya Magole- Turiani yenye urefu wa kilometa 48.6 ni sehemu ya utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya Magole- Turiani- Mziha yenye urefu wa kilometa 88.6 kwa kiwango cha lami.