|
TETEMEKO la ukubwa wa mtikisiko wa kipimo cha Ritcher 5.7 limetokea katika mikoa mitatu nchini na watu zaidi ya 10 wamekufa na wengine 120 wamejeruhiwa huku majengo mengi yakibomoka.
Mikoa iliyoripotiwa kuathiriwa kwa tetemeko hilo ni Kagera, Mwanza na Mara. Pia tetemeko hilo limeukumba mji wa Kampala na Rakai nchini Uganda jana saa 9.27 alasiri.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi alisema tetemeko hilo limetokea saa tisa alasiri na zaidi ya watu 10 wamekufa.
Awali, akizungumza kwa simu kutoka jiijini Dar es Salaam, Kamanda Ollomi alisema watu wanane walikufa na baadaye alisema idadi hiyo iliongezeka na kwamba alipata taarifa kutoka hospitali ya mkoa kuwa wamepokea miili ya watu 10 na wameihifadhi.
Alisema tisa kati ya waliokufa ni wakazi wa Manispaa ya Bukoba na mmoja ni mkazi wa wilayani Karagwe.
Kamanda alisema miongoni mwa majeruhi wamo wanafunzi 15 wa Shule ya Sekondari ya Wavulana Ihungo na wapo katika hospitali ya mkoa wanaendelea kupatiwa huduma. Alisema bado vikosi vya uokoaji likiwemo Jeshi la Polisi na Zimamoto vinaendelea na uokoaji.
Alisema watu waliojeruhiwa na waliokufa wamedondokewa na kuta, vifusi na vyombo vya ndani.
Alisema wengine walikufa kwa mshituko unaosababishwa na shinikizo la damu na nyumba zaidi ya 40 zimeathirika.
“Ni kweli tetemeko la ardhi limetokea na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali za watu, vifo pamoja na majeruhi na bado tunaendelea kupokea taarifa zaidi,” alisema Kamanda Ollomi na kuongeza kuwa mpaka jana jioni walikuwa wakiendelea kupokea taarifa kutoka sehemu mbalimbali za mkoa huo kuhusu vifo na majeruhi.
Wakala wa Jiolojia waelezea ukubwa wake
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), Profesa Abdulkarim Mruma alisema tetemeko hilo ni kubwa kwa nusu ya kipimo cha juu cha Ritcher10 na limezidi kipimo cha chini cha ukubwa wa Ritcher tatu. Alisema limezidi lililotokea Dodoma hivi karibuni.
Profesa Mruma alisema tetemeko hilo limetokea katika mpaka wa Tanzania na Uganda, kilometa 47 kaskazini mwa Bukoba mkoani Kagera na sababu ni mpasuko wa ardhi katika Bonde la Ufa la magharibi karibu kabisa na Ziwa Victoria .
Amewataka wananchi kuchukua tahadhari kwani kwa kawaida linapotokea tetemeko kubwa kama hilo hufuatiwa na matetemeko madogo na ardhi hutulia baada ya siku mbili mpaka tatu. “Kwa wakati huu ili kuepuka madhara zaidi, litakapotokea watoke nje ya nyumba na kukaa mbali na miti kwenye uwanja wa wazi na wanaoendesha magari waache mara moja,” alisema Profesa Mruma.
Alisema kwa sasa wataalamu katika kituo chao cha kupimia matetemeko cha Geita wanaendelea kupata takwimu zaidi kutokana na kuwa mpasuko wa tetemeko hilo umekuwa karibu sana na ziwa Victoria na baadaye watatoa taarifa kuhusu tukio hilo kwa undani.
Waathirika wazungumza
Baadhi ya watu walioathirika kwa tetemeko hilo mkoani Kagera walilieleza gazeti hili kuwa maeneo yalioathirika zaidi mkoani humo ni Bukoba Vijijini katika Kata ya Lubale, Kitongoji cha Migala, ambapo baadhi ya nyumba zimebomoka na kupata nyufa. Pia katika Wilaya ya Muleba ni Kata ya Buganguzi.
“Tulikuwa kwenye tafrija, tukasikia nyumba nzima inatetemeka. Tulidhani ni umeme umepata hitilafu, tukakimbia nje,” alisema Berena Nkalomba, mkazi wa Kata ya Buganguzi wilayani Muleba aliyesema pia kuwa nyumba kadhaa kijijini kwao Buhanga, zimepata nyufa na nyingine kubomoka kabisa katika kata hiyo.
Mkazi mwingine wa Bukoba Vijijini, Kata ya Lubale, Mbelwa Jonathan, alisema, “Tulikimbia kutoka nje, nyumba yangu imebomoka upande.” “Hata wazee wanasema hawajawahi kushuhudia tetemeko la namna hii. Sisi tuliona vitu ndani ya nyumba vinadondoka, tukakimbilia kwenye uwanja. Tumeshuhudia nyumba zikibomoka na watu wakikimbizwa katika hospitali ya mkoa,” alisema Novert Tayebwa, mkazi wa Kashai, Bukoba Mjini.
“Ilikuwa mida ya saa tisa na nusu nikiwa nimelala ndani ndipo nikasikia mtikisiko kwa bahati mbaya nilikuwa peke yangu na nilikuwa nimejifungia ndani, lakini namshukuru Mungu maana niliweza kufungua mlango na kutoka salama,” alisema Kashura wa Bukoba Mjini.
Mkazi mwingine wa Kashai, Specioza Lukamba alisema nyumba yake pamoja na baadhi ya majirani zake wameathiriwa na tetemeko hilo. “Hapa nilipo tupo nje ya nyumba zetu…mimi nilikuwa bafuni naoga nje ya nyumba yangu, nikasikia mtetemeko, nikatoka mbio…yaani ilikuwa hali mbaya. Nyumba yangu imeharibika upande mmoja pamoja na vitu vyangu kuharibika,” alieleza Lukamba.
Kauli ya Mkuu wa Mkoa
Naye Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kagera ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Deodatus Kinawilo alisema tetemeko hilo limetokea mkoa mzima ila taarifa walizopata ni za Manispaa ya Bukoba na kifo kimoja cha Karagwe ambapo taarifa za wilaya nyingine bado zinafuatiliwa.
Aliwashauri wananchi kuwapeleka waliopata majeraha katika zahanati zilizoko karibu nao ili wapatiwe huduma kwani dawa zimeletwa za kutosha ingawa mwanzo ziliisha na Serikali ya Mkoa ililazimika kuagiza katika Duka la dawa la MK la mtu binafsi.
Mwanza
Mkoani Mwanza, Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Ahmed Msangi aliliambia gazeti hili jana kwa simu kuwa tetemeko hilo lilipita kwa muda mchache wa kama sekunde mbili na mpaka jana jioni, hawakuwa na taarifa zozote za madhara kwa binadamu wala mali.
“Hapa kwetu tetemeko limepita tu na mpaka sasa bado sijapata taarifa kama kuna amdhara makubwa yametokea bali, limetutikisa tu,” alisema Kamanda Msangi.
Mara
Taarifa kutoka mkoani Mara, zilieleza kuwa wilayani Bunda taarifa zinaeleza kuwa, tetemeko hilo limetikisa kwa sekunde mbili na hakuna madhara kwa binadamu wala majengo isipokuwa lilisababisha taharuki kwa baadhi ya watu.
Taarifa kutoka wilayani Musoma zinaeleza kuwa tetemeko lilitikisa maeneo ya mji kwa sekunde kadhaa na nyumba moja iliyopo Musoma Mjini ilipata ufa na hakuna madhara kwa binadamu.
Mitandao ya kijamii
Baadhi ya taarifa zilizosambaa katika mitandao ya kijamii zilieleza kuwa tetemeko hilo lina ukubwa wa magnitude 5.7 na limetokea umbali wa kilometa 40 kutoka mji wa Rakai, Uganda saa 9:27 alasiri na muda huo lilitikisa Bukoba na maeneo mengine ya Mwanza na Mara.
Magufuli aomboleza
Katika taarifa ya Ikulu jana, Rais Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Salim Kijuu kutokana na vifo vya watu kadhaa vilivyotokea kutokana na tetemeko hilo la ardhi katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Katika salamu hizo, Rais Magufuli ameeleza kushitushwa na taarifa za tukio hilo lililosababisha idadi kubwa ya watu kupoteza maisha, wengine kujeruhiwa pamoja na uharibifu wa mali. Amesema anaungana na familia zote zilizopoteza ndugu, jamaa na marafiki na anawaombea marehemu wapumzishwe mahali pema peponi. Amina.
“Kupitia kwako Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Mstaafu Salum Mustafa Kijuu na wakuu wa mikoa jirani yako iliyokumbwa na tukio hilo, natoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wote waliopoteza jamaa zao na nawaombea kwa Mwenyezi Mungu awape moyo wa subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu,” alisema Rais Magufuli na kuwaombea wote walioumia katika tetemeko hilo wapone haraka.
Imeandikwa na Theopista Nsanzugwanko, Gloria Tesha, Stella Nyemenohi (Dar es Salaam) na Angela Sebastian, Bukoba.
0 Comments