Kaimu Mkurugenzi wa TBS, Egid Mubofu
KUTOKANA na kuwepo kwa habari kuhusu uzalishaji usiokidhi ubora wa unga wa dona na sembe katika baadhi ya maeneo nchini, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limetaka wazalishaji wa bidhaa hizo, kuzingatia taratibu zilizowekwa na mamlaka husika katika uzalishaji wake.

Gazeti hili wiki iliyopita liliandika habari za kina kuhusu uzalishaji wa unga wa dona na sembe katika maeneo kadhaa nchini, ambao unaonekana kuwa na ubora hafifu, hatua ambayo imeibua mjadala mkali.
Kwa upande wake, Umoja wa Wamiliki na Wazalishaji wa Sembe (UWAWASE), umesisitiza kuwa unga unaozalishwa katika eneo la Tandale jijini Dar es Salaam, unazingatia kiwango cha juu cha ubora.
Katika habari ya Jumamosi iliyopita, gazeti hili lilifafanua kuhusu utata katika mazingira ya uzalishaji wake, ikidaiwa kutozingatia taratibu stahiki, hasa kwa wazalishaji kushindwa kufuata kanuni zinazotakiwa.
Akizungumza na gazeti hili juzi, Kaimu Mkurugenzi wa TBS, Egid Mubofu aliwataka wazalishaji hao badala ya kulalamika, wazingatie taratibu zinazotakiwa .
Alisema kuwa bidhaa za unga wa mahindi ni moja ya bidhaa za lazima kuidhinishwa na TBS, kabla ya kuingia sokoni. Aliongeza kuwa kiwango kinachotakiwa kutumiwa katika kupima ubora wa unga wa sembe ni TZS 328: 2014.
Kaimu huyo aliongeza kuwa kwa sasa ofisi yake, inaendelea na utaratibu wa kutoa semina kwa wazalishaji hao wa kati na kuwataka wazalishaji kutopuuza mafunzo hayo.
Kwa upande wake, Umoja wa Wamiliki na Wazalishaji wa Sembe (UWAWASE) chini ya Mwenyekiti wake, Oscar Munisi akizungumza kwa niaba ya wazalisha sembe 210 waliopo Manzese na Tandale, alisema changamoto kubwa si ubora, bali ni uzalishaji kufanyika katika eneo ambalo ni makazi ya watu.
Aliweka wazi kuwa Umoja huo umenunua eneo nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, litakalokuwa ni Kijiji cha Wazalishaji Sembe, kama njia ya kuboresha zaidi uzalishaji wake.
Alisema, uamuzi huo ni kutokana na ushauri uliotolewa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TDFA) uliowataka kuhakikisha kuwa wanatafuta eneo rafiki kwa uzalishaji huo wa bidhaa za chakula.
Mwenyekiti wa Kamati ndogo ya Nidhamu katika umoja huo, William Siga aliweka wazi kuwa wakati wa msimu wa mahindi mwezi wa Juni na Julai, wanapata magunia 300 hadi 400 ya mahindi ambayo wanayaosha, kuyachuja na uchafu na ndipo wanasaga.
Umoja huo uliiomba serikali kutambua nafasi yao katika kuzalisha sembe na dona na kutoa ajira kwa vijana wengi, iwasaidie miundombinu bora zaidi ya uzalishaji wa bidhaa hizo, hasa katika kuendeleza eneo lao la Kiluvya ili hatimaye wazalishe sembe na dona kiufasaha, kama inavyoshauriwa na TFDA.
Msemaji wa TFDA, Gaudensia Simwanza akizungumzia uzalishwaji huo, alisema kuwa ofisi yake inafanya juhudi kubwa katika kutengeneza mazingira bora zaidi na rafiki kwa wazalishaji hao na kisha wanawapa semina za mara kwa mara.