ASKARI wawili waliofukuzwa kazi na Jeshi la Polisi mkoani Mbeya wamepandishwa kizimbani jana katika Mahakama ya Mkoa wa Mbeya wakikabiliwa na jumla ya mashitaka 13 waliyoyatenda dhidi ya wanafunzi wa kidato cha nne likiwamo la kuwaingilia kimwili kwa nguvu.
Waliopandishwa kizimbani ni Konstebo Petro Magana aliyekuwa wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) Mbeya na Konstebo Lucas Ng’weina wa Wilaya ya Kipolisi Mbalizi.

Katika kesi namba 147 ya mwaka 2016, ilidaiwa na Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Catherine Paul mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Mbeya, Zawadi Laizer kuwa washitakiwa walitenda makosa hayo Novemba 4, mwaka huu saa tano usiku katika Shule ya Sekondari Isuto iliyopo wilayani Mbeya.
Mwendesha Mashitaka aliiambia mahakama hiyo kuwa katika shitaka la kwanza la kosa la udhalilishaji wa hali ya juu linalomkabili Konstebo Petro pekee, siku ya tukio mshitakiwa alijaribu kumwingilia kimwili mwanafunzi (jina linahifadhiwa) mwenye umri wa miaka 14 huku pia akimdhalilisha mwanafunzi huyo jambo ambalo ni kinyume cha sheria Kifungu namba 138 A cha Kanuni ya Adhabu.
Alisema kwa shitaka la pili la kosa la udhalilishaji wa hali ya juu pia linalomkabili Konstebo Lucas peke yake, siku ya tukio mshitakiwa alijaribu kumwingilia kimwili mwanafunzi (jina linahifadhiwa) mwenye umri wa miaka 16 na kisha kumdhalilisha jambo ambalo pia ni kinyume cha sheria Kifungu namba 138 A cha Kanuni ya Adhabu.
Mwendesha Mashitaka huyo wa Serikali alizidi kubainisha kuwa mashitaka mengine yote kuanzia shitaka namba tatu hadi 13 yanayohusu shambulio yanawakabili washitakiwa wote wawili kwani kwa pamoja waliwashambulia wanafunzi 11 wa kidato cha nne kwa kuwachapa viboko sehemu mbalimbali za miili yao jambo ambalo ni kinyume cha Sheria Kifungu cha 240 cha Kanuni ya Adhabu.
Aliwataja wanafunzi walioshambuliwa na askari hao kuwa ni Neema Mabalanjo, Vicky Mwaya, Tumpe Jonas, Ombeni Tuonee, Lutabite Landa, Jane Msukulu, Zulfa Julius, Atupole Boniface, Betha Joseph, Blandina Mwaigaga na Zainabu Leonard.
Hakimu Mkazi Laizer aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 14, huku akisema dhamana kwa washitakiwa wote wawili iko wazi kwa masharti ya kila mmoja kutosafiri nje ya Mkoa wa Mbeya bila idhini ya mahakama hiyo na pia kila mshitakiwa kuleta mdhamini mmoja ambaye ni mtumishi wa umma ambaye ataweka dhamana ya malikauli isiyopungua thamani ya Sh milioni saba.
Hadi kesi hiyo inaahirishwa mahakamani hapo washitakiwa wote ambao kwa pamoja wanatetewa na Wakili wa Kujitegemea, Josephat Kazeula walishindwa kutimiza masharti ya dhamana na kutakiwa kurudishwa rumande.