Follow us: Subscribe via RSS Feed Connect on YouTube Connect on YouTube
Maganga One Blog kwa habari za kitaifa,kimataifa,burudani na michezo kila siku. Tutumie habari na matukio yoyote kwa email yetu ya magangaone@gmail.com

Nov 11, 2016

Bunge lampa heshima adhimu Sitta

SPIKA mstaafu wa Bunge, Samuel Sitta (73) leo ataagwa ndani ya Bunge la Tanzania mjini Dodoma kabla ya kusafirishwa kwenda Urambo mkoani Tabora kwa maziko, ikiwa ni historia kwa kiongozi kuagwa ndani ya Bunge hilo.
Jana, Bunge lililazimika kutengua kanuni kuwezesha kumpa heshima za kipekee Sitta aliyekuwa Spika wa Bunge la 10 kuanzia mwaka 2005 hadi 2010 ambaye leo mwili wake utaingizwa ndani ya Ukumbi wa Bunge kuagwa kwa heshima na wabunge ambao baadhi yao alikuwa nao katika Bunge hilo la Tanzania.

Sitta aliyewahi kuwa pia Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, alifariki usiku wa kuamkia Jumatatu katika Hospitali ya Technical University ya mjini Munich, Ujerumani ambako alikuwa amelazwa akitibiwa saratani ya tezi dume. Alizaliwa Desemba 18, 1942 mjini Urambo.
Mwili wa Sitta uliwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Julius Nyerere (JNIA) jana saa tisa alasiri ukitokea nchini Ujerumani ambako alienda kwa matibabu. Ulipokewa na baadhi ya viongozi wa serikali, viongozi wastaafu, viongozi wa vyama vya siasa pamoja wananchi waliofika uwanjani hapo.
Kwa hatua hiyo ya kutengua kanuni, Mkutano wa Tano wa Bunge la 11 utakuwa umetengua kanuni zake kwa mara ya pili; awali kanuni zilitenguliwa juzi Jumanne ili kusitisha shughuli za Bunge baada ya kifo cha Sitta kutangazwa.
Spika wa Bunge, Job Ndugai jana kwa mujibu wa utaratibu na kanuni za Bunge, alimuomba Waziri, Ofisi ya Rais, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama kutengua kanuni ili kuruhusu shughuli za kumuaga Sitta zifanyike ndani ya Ukumbi wa Bunge kwa heshima ya kiongozi huyo.
“Nitaomba Waziri wa Nchi asimame ili kutengua baadhi ya kanuni ili haya yawezekane,” alisema Ndugai baada ya kuwaeleza wabunge kitakachofanyika leo. Jenista alisimama na kabla ya kutengua kanuni alisema hatua hiyo inafanyika ili kuruhusu shughuli za leo zifanyike kwa matakwa ya kikanuni. “Kwa kuwa Bunge limepata msiba na kwa kuwa Bunge limepanga kumuenzi na kumuaga katika ukumbi wa Bunge, kuna kanuni zitapaswa kutenguliwa,” alisema Jenista.
Kanuni zilizotenguliwa ni ya 139 (1) inayohusu wageni wanaoingia Ukumbi wa Bunge kwamba wataketi maeneo maalumu ya wageni na si katika ukumbi wenyewe na kanuni ya 143 (e)-(f) kuhusu mpangilio wa Bunge wa kukaa, uliowekwa kwa namna ya baadhi ya watu.
“Kanuni hizo zitenguliwe ili kuruhusu ndugu wa karibu wasiozidi 12 waingie kushiriki tukio hilo na kuhusu kanuni ya 143 mpangilio wa ukaaji bungeni utenguliwe ili jeneza liingizwe ndani ya ukumbi na kuwekwa sehemu iliyoandaliwa mbele,” alitoa hoja na wabunge wote kuiunga mkono.
Ndugai alimwelezea Sitta ambaye akiongoza Bunge alijipambanua kwa falsafa yake ya Kasi na Viwango, aliyeanzisha matangazo ya mubashara (live) katika Bunge la 10 na kuwaeleza wabunge kuwa, leo shughuli ya kumuaga itakuwa mubashara.
Akielezea utaratibu wa leo, Ndugai alisema wataupokea mwili wa Sitta saa 8 mchana kwenye Uwanja wa Ndege wa Dodoma.
“Kutakuwa na kikao maalumu cha Bunge saa 8:30 mchana tuwe tumekaa kwa kikao hicho maalumu cha Bunge ambacho hakijawahi kutokea,” alisema Spika Ndugai na kuongeza kuwa wabunge watapata nafasi ya kutoa salamu za rambirambi na heshima za mwisho ingawa jeneza halitafunuliwa.
Alisema baada ya shughuli hizo bungeni, mwili utasafirishwa kwenda Urambo kwa maziko na wabunge 10 akiwemo Spika watakwenda katika maziko na wataondoka Jumamosi. Alisema Tume ya Huduma za Bunge itateua wabunge kwa uwakilishi wa vyama.
“Tunampa heshima za kipekee sana mzee wetu, tutaupokea mwili na tutauingiza ndani ya ukumbi hapo mbele ya kiti, baada ya hapo kutakuwa na ratiba. Baadhi watatoa maneno mafupi kwa uwiano kama ilivyo kawaida ya Bunge letu. Tutaongozwa na Waziri Mkuu na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe,” alisema.
Akielezea zaidi alisema baada ya hapo wabunge watatoka nje ya lango kuu, watakakokaa kwa muda mfupi.
“Tutabeba jeneza kwa kushirikiana. Tumepewa saa mbili tu. Tutafanya kumpa heshima kubwa Mzee Sitta. Viongozi wetu wa kitaifa watapewa heshima zote hizo kwa kuletwa bungeni ambako ndiko nyumba ya Watanzania wote ilipo,” alisema Ndugai.
Alisema kabla ya kutoka nje, Waziri Mkuu atatoa hotuba ya kuahirisha Bunge, lakini Spika hatawahoji wabunge mpaka shughuli ya kumuaga Sitta iishe na wakiutoa mwili nje na kumaliza, ndipo atawahoji.
“Tunataka hii shughuli iingie kwenye shughuli za Bunge,” alisema Ndugai.
Jijini Dar es Salaam, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan jana amewaongoza baadhi ya wakazi wa jiji hilo kupokea mwili wa Sitta na kueleza kuwa taifa limempoteza mshauri muhimu. Samia alisema Sitta alikuwa kiongozi mahiri ambaye alikuwa haamini kwenye kushindwa.
Makamu huyo wa Rais ambaye alifanya kazi na Sitta kwenye Bunge Maalumu la Katiba, alisema Bunge hilo lilikuwa na changamoto nyingi, lakini siku zote Sitta alimtia moyo kwamba hawatashindwa.
“Taifa tumempoteza mshauri, ni mtu ambaye hakuamini kushindwa, kwake yeye nilijifunza uvumilivu na kusimamia mambo kwa kiwango cha juu,” alisema Samia na kuongeza kuwa kuwa Sitta alikuwa kaka kwake, mshauri na kwamba hakuchoka kutoa ushauri katika mambo ambayo yeye aliona hayana ufumbuzi. “
Aliniamini akiwa ananiachia niongoze Bunge nyakati za jioni na yeye akawa anampumzika nyumbani kwake, kulipotokea changamoto nilipoenda kumweleza, kwa ushauri wake nilijikuta naona kwamba jambo hilo sio changamoto tena,” alisema Samia aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge hilo, Sitta akiwa Mwenyekiti.
Mwili wa marehemu uliwasili uwanjani hapo huku ukiwa unasindikizwa na Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Philip Marmo pamoja na mke wa marehemu, Margaret Sitta.
Baadhi ya viongozi waliofika uwanja wa ndege kupokea mwili huo pamoja na Samia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Augustine Mahiga, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, Spika mstaafu Pius Msekwa na Mwenyekiti wa CUF Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba.
Shughuli ya kupokea mwili wa Sitta ilifanyika katika uwanja wa ndege wa zamani ambako ulibebwa kwa gari la Jeshi na baadaye askari wa Polisi walibeba jeneza lake na kulipitisha mbele ya Makamu wa Rais kama ishara ya kupokewa kwa mwili huo kwa taratibu zote za serikali.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, jana mwili huo ulipelekwa nyumbani kwake Masaki jijini Dar es Salaam na leo asubuhi utapelekwa Viwanja vya Karimjee kwa ajili ya kuwapa nafasi wananchi na viongozi wa serikali kutoa heshima zao za mwisho kuanzia saa 1.30 asubuhi.
Mchana utapelekwa JNIA kwa ajili ya kusafirishwa kuelekea mkoani Dodoma na utawasili mkoani humo saa 8 mchana. Utapelekwa katika Viwanja vya Bunge ambapo salamu mbalimbali zitatolewa na Spika, Waziri Mkuu, Kambi Rasmi ya Upinzani na viongozi wa Mkoa wa Dodoma. Kisha wabunge watatoa heshima za mwisho.
Jioni mwili wa Sitta utapelekwa Uwanja wa Ndege wa Dodoma kwa ajili ya kusafirishwa kwenda Urambo mkoani Tabora kwa ajili ya maziko. Utawasili Uwanja wa Ndege wa Tabora saa 10 jioni na baadaye kusafirishwa kwenda nyumbani kwake Urambo ambako utawasili saa 12 jioni.
Waombolezaji wilayani Urambo na maeneo mengine watatoa heshima za mwisho kesho kuanzia asubuhi na maziko yanatarajia kufanyika saa tisa alasiri kuhitimisha miaka 73 na ushee ya maisha ya mmoja wa wanasiasa waadilifu na wazalendo nchini Tanzania aliyeifanyia mengi mema ya kukumbukwa.
Imeandikwa na Gloria Tesha, Dodoma na Shadrack Sagati, Dar.

Share this article :

0 Maoni:

 
Maganga One Blog © Copyright 2017. All Rights Reserved.

Powered by Maganga One.
Back to TOP