SUALA la uuzwaji wa hisa za Shirika la Usafiri la Jiji la Dar es Salaam (UDA), limeibuka tena bungeni baada ya Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) kutaka suala hilo liundiwe Kamati Teule ya Bunge.
Pamoja na suala hilo la UDA kuibuliwa na Mdee, pia wabunge wengi wameitaka serikali kuongeza fedha Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ili itekeleze majukumu yake vizuri zaidi.

Mdee aliyeeleza historia ya UDA na namna linavyozingirwa na ukakasi, alisema atawasilisha hoja binafsi bungeni kuomba kuundwe kamati hiyo Teule ya Bunge kuchunguza suala hilo.
Wakati Mdee akieleza hayo, Waziri wa Nchi, Ofis ya Rais, Tamisemi, George Simbachawene, alisema bungeni kuwa serikali imekwenda hatua kwa hatua kuhusu UDA kwa kushirikiana na Kamati ya Bunge ya Serikali za Mitaa (LAAC) na tayari kamati hiyo imeagiza taarifa fulani ili kukamilisha suala hilo na kamati italeta taarifa bungeni.
Mdee alikuwa akichangia taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ya kuanzia Juni 30, 2014 hadi Juni 30, 2015 pamoja na ile ya Serikali za Mitaa (LAAC), ya mwaka 2013/14 na 14/15, jana bungeni mjini hapa.
Alisema yeye ni mjumbe wa Baraza la Madiwani wa Jiji la Dar es Salaam na baada ya kuona suala la UDA limeingizwa bungeni na mambo yanayohusiana na jiji yakitajwa na baadhi ya hoja kutaka Jiji livunjwe kutokana na kashfa ya kiwanda cha nyama, baadhi wanasahau kwamba yanayotokea sasa katika shirika hilo yalianza wakati wa CCM ikiliongoza Jiji hilo.
Alisema sasa wakati Ukawa wapo kwa wingi katika Jiji, wanataka kusafisha masuala yote ya ufisadi katika Jiji.
“Nimesikia zile bilioni tano alizolipa Simon Group zinataka zipangiwe matumizi, naomba niwaambie sisi kama Jiji tunatambua mamlaka yetu, sasa kama hatujitambui na serikali inataka kuingilia sisi tunatambua mamlaka yetu,” alisema Mdee.
Ili kuondoa mzizi wa fitina kwa sababu CAG amefanya kazi na Takukuru wamefanya kazi, naliomba Bunge kupitia kanuni ya 120 tuunde kamati teule ili suala hili lifanyiwe uchunguzi tujue kinagaubaga tujue mbivu zipi na mbichi ni zipi.
Simbachawene jana jioni bungeni alisema LAAC imewaagiza taarifa kuhusu UDA na suala hilo halipaswi kuletwa tena bungeni kwa sasa kwa kuwa tayari kuna hatua imefanyika na wabunge wanapaswa kusubiri taarifa hiyo italetwa bungeni.
Katika taarifa yake, LAAC imesema ofisi ya CAG inahitaji kuongezewa fedha kwa kuwa ilishindwa kutembelea miradi mingi kutokana na bajeti finyu.
Mwenyekiti wa LAAC, Vedasto Ngombale Mwiru alisema ofisi ya CAG ilishindwa kutembelea baadhi ya halmashauri kuthibitisha majibu ya hoja mbalimbali za ukaguzi.
Aliitaja Halmashauri ya Korogwe kuwa ni mojawapo. Alishauri bajeti iongezwe ikiwa majawabu ya hoja za serikali za mitaa zinatakiwa kuleta tija. Mbunge wa Moshi Mjini, Jafar Michael (Chadema ) alisema mwaka huu wa fedha (2016/17) watu wanaona madudu maana CAG hajawekewa fedha za kutosha kwenye ukaguzi na inawezekana akafika wilaya 10 tu maana fedha hana.
“Miradi mingi inategemea fedha Serikali Kuu lakini fedha haziendi, halmashauri ziwe na data base, (kanzi data) “ alisema mbunge huyo.
Mbunge wa Viti Maalumu, Conchesta Rwamlaza (Chadema) alisema kama fedha hazitapelekwa katika halmashauri kwa namna ilivyo, itaua hizo halmashauri na kutaka pia kuwa kitengo cha CAG, serikali ikiimarishe.
Mbunge wa Nanyamba Abdallah Chikota (CCM) alizungumzia pia suala la CAG na kutaka fedha zaidi apewe kumuwezesha kufanya kazi kubwa zaidi ya aliyofanya katika taarifa iliyozifikia kamati za Bunge za LAAC na PAC.