Follow us: Subscribe via RSS Feed Connect on YouTube Connect on YouTube
Maganga One Blog kwa habari za kitaifa,kimataifa,burudani na michezo kila siku. Tutumie habari na matukio yoyote kwa email yetu ya magangaone@gmail.com

Nov 8, 2016

Buriani Samuel Sitta

TAIFA la Tanzania limempoteza kiongozi mzalendo na mwadilifu, Spika wa Bunge mstaafu, Samuel John Sitta (73) aliyejipambanua kuwa Spika wa Kasi na Viwango. Sitta amefariki dunia usiku wa kuamkia jana katika Hospitali ya Technical University of Munich nchini Ujerumani, alikokuwa akipatiwa matibabu. Sitta alikuwa akipatiwa matibabu nchini Ujerumani na alipoelekwa huko mwishoni mwa mwezi Septemba.

Wakati anaondoka nchini familia ilithibitisha kuwa mwanasiasa huyo, alikuwa anasumbuliwa na maradhi ya miguu. Sitta ambaye aliwahi kuzushiwa habari za kifo mwezi uliopita, zilianza kusambaa jana asubuhi kwenye mitandao ya kijamii na baadaye familia ya mwanasiasa huyo ikathibitisha kutokea kwa msiba huo kupitia kituo kimoja cha redio.
Mtoto wa marehemu, Benjamin Sitta alizungumza na baadhi ya vituo vya redio na kuthibitisha kifo cha baba yake.
Alisema baba yake alienda Ujerumani kutibiwa maradhi ya saratani ya tezi dume ambayo yalikuwa yanamsumbua kwa muda mrefu.
“Alienda nje kwa ajili ya kupambana na maradhi hayo, kwa bahati mbaya saratani hiyo ilienea sana ikaanza kuathiri hadi viungo vingine ikiwemo miguu. Yote ni mapenzi ya Mungu kwani ilipofika saa saba usiku kwa saa za Ujerumani na huku ilikuwa ni saa 10 alfajiri, mzee alifariki dunia. Mke wake Margaret yuko Ujerumani tukipata taarifa zingine tutaendelea kuwajulisha,” alisema Benjamin.
Baadaye Ikulu ilitoa taarifa kuonesha kuwa Rais John Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Spika wa Bunge, Job Ndugai kuhusu kifo cha mwanasiasa huyo nguli.
Taarifa hiyo ya Ikulu ndiyo iliyoupa umma uthibitisho wa kifo cha Sitta.
Lakini,bungeni ambako Sitta alikuwa Spika kuanzia mwaka 2005 hadi 2010, akisoma taarifa ya iliyotolewa na Spika wa Bunge, Job Ndugai, Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu alisema Bunge limepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha Spika wa Bunge la Tisa aliyefariki saa 7:50 usiku kwa saa za Ujerumani (saa 09:50 alfajiri nchini) wa kuamkia jana katika Hospitali ya Technical University of Munich alipokuwa anatibiwa.
Zungu alisema Sitta aliondoka nchini Novemba 3, mwaka huu na kwenda nchini humo kwa ajili ya matibabu ambayo Bunge lilikuwa likigharamia. Zungu alisema Bunge linatoa pole kwa familia hususan Mbunge wa Urambo, Margaret Sitta (CCM) ambaye ni mke wa marehemu.
Hali ilivyo nyumbani kwake Baada ya kuthibitishwa kwa habari za kifo ha mwanasiasa huyo, gazeti hili lilienda nyumbani wake na kukuta maandalizi ya kupokea mwili wa Sitta yakiwa yanaendelea kufanywa na wanafamilia.
Miongoni mwa maandalizi hayo ni kutundika mahema pamoja na viti ambavyo vitatumiwa na waombolezaji watakaofika kwenye makazi yake hayo yaliyoko Mtaa wa Manzese, Masaki, mkabala na ofisi za Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wakimbizi (UNHCR).
Baadhi ya wanasiasa waliokuwepo nyumbani hapo ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhan Madabida, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na Mbunge wa zamani wa Tabora Mjini, Ismail Aden Rage. Hata hivyo, Madabida alisema kwamba taarifa za lini mwili utawasili pamoja na taratibu zingine zote zitakuwa zinatolewa na Ofisi ya Bunge.
Mama yake amlilia, Urambo yazizima
Maandalizi ya mwanasiasa mkongwe wilayani Urambo mkoani Tabora, Sitta yanaendelea huku ndugu na jamaa wa karibu wakiendelea kuwasili wilayani humo. Akizungumza na gazeti hili nyumbani kwa marehemu mjini hapa jana, mdogo wake Peter Sitta alisema maandalizi yanaendelea huku wakiendelea kusubiri taarifa za ratiba kutoka kwa Kamati ya Bunge iliyoundwa kuratibu.
Mama mzazi wa Sitta, Hajjat Zuwena Saidi Fundikira akizungumza kwa masikitiko huku akibubujikwa na machozi, alisema hana cha kusema zaidi ya kulia.
Mama huyo ni wa ukoo wa Chifu Fundikira wa mkoani humo.
“Nilipokea taarifa hizi kutoka kwa mwanangu Peter John Sitta baada ya kufika nyumbani huku akilia na baada ya kunyamaza ndipo alinieleza kuwa kuna msiba,” alisema na kuongeza kuwa kamwe hatamsahau mtoto wake kwani bila ya Samuel yeye asingeijua ibada ya hija, kwani alimpenda katika maisha yake.
Anavyokumbukwa kwenye siasa
Sitta akiwa Spika wa Bunge la Tisa atakumbukwa kwa kuweka misingi ya Bunge imara la kuisimamia serikali kwa maslahi ya taifa wakati.
Alilielekeza Bunge kufanya kazi yake ya kuisimamia serikali kikamilifu na wananchi wakaanza kuona nguvu za mhimili huo wa dola. Ni Sitta ndiye aliwezesha Bunge kupata uwezo wa kujitegemea.
Alisimamia mhimili huo wa dola na hivyo kutokuwa rahisi kuingiliwa na mihimili mingine ya dola ambayo ni Serikali na Mahakama.
Chini ya falsafa yake ya Kasi na Viwango, Sitta pia anaelezwa kuwa ni spika aliyetetea maslahi ya wabunge na kufanya yakaboreshwa katika kipindi chake.
Wabunge wanaamini kuwa ndiye alikuwa nguzo ya wao kupata maslahi mazuri. Akiwa Spika, Sitta alijipambanua kupambana na ufisadi jambo ambalo lilimjengea heshima kubwa kwa jamii.
Aliunda tume ya kuchunguza ufisadi dhidi ya kampuni ya kufua umeme ya Richmond ambayo baada ya kukamilisha kazi yake ilisababisha aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kujiuzulu.
Akiwa Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Sitta atakumbukwa kwa kusimama kidete kuhakikisha kwamba Bunge hilo ambalo lilisusiwa na wapinzani, linakamilisha kazi ya kuandika rasimu ya Katiba mpya na kupitishwa na Bunge hilo.
Inaelezwa kuwa Katiba imekamilika kwa asilimia 85. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alimuelezea Sitta kuwa "alikuwa jasiri, alikuwa na uwezo wa kusimamia anayoyaamini, mzalendo, amefanya mageuzi bungeni na kila alipofanya kazi ameacha alama. Katiba imekamilika kwa asilimia 85 na imebaki kupitishwa tu na hiyo ni kutokana na nguvu yake (Sitta).”
Wasifu wake
Samuel John Sitta alizaliwa Desemba 18, 1942 wilayani Urambo Mkoa wa Tabora. Alisoma Shule ya Msingi Urambo kati ya mwaka 1950 – 1953, kisha alikwenda Wilaya ya Sikonge mwaka 1954 - 1957 na kuendelea na masomo ya kati katika Shule ya Sikonge Middle School. Baadaye mwaka 1958 – 1963 alianza masomo ya sekondari Shule ya Wavulana Tabora yaani Tabora Boys kidato cha I – IV na cha V – VI.
Baada ya kuhitimu masomo ya sekondari, Sitta alijiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kusomea Shahada ya Sheria (LLB) mwaka 1964 na kuhitimu mwaka 1971. Utumishi wa umma Sitta aliajiriwa na Kampuni ya Mafuta ya CALTEX OIL kama Meneja wa Tawi (1967 – 1969) na mwaka 1969 – 1975 aliajiriwa na Shirika la Maendeleo la Taifa kama Katibu na Mkurugenzi wa Utawala.
Baadaye mwaka 1976 Sitta aliamua kujiendeleza kielimu katika masuala ya Usimamizi nchini Uswisi kwenye Chuo Kikuu cha IMEDE ambako alihitimu Stashahada ya Juu ya Usimamizi mwaka huo 1976.
Maisha katika siasa
Enzi za chama kimoja 1975 – 1995, Sitta alikuwa Mbunge wa Jimbo la Urambo (kabla halijagawanywa na kuwa Urambo Magharibi na Mashariki) na pia alifanikiwa kuwa waziri kwa nyakati tofauti. Kwa mfano, wakati wa kipindi cha mwisho cha Mzee Mwinyi, Sitta alikuwa Waziri za Katiba na Sheria.
Mwaka 1995, Sitta alipambana na Jacob Msina wa NCCR Mageuzi.
Msina alishinda ubunge huo na kumweka kando mwanasiasa huyo.
Sitta alirudi tena kwenye jukwaa la siasa mwaka 2005 kwenye Uchaguzi Mkuu alishinda ubunge na kuteuliwa na CCM kugombea uspika wa Bunge la Tanzania na akaliongoza Bunge la Tisa aliloliita Bunge la Kasi na Viwango kwa mafanikio na changamoto nyingi.
Mwaka 2010, Sitta alishiriki tena uchaguzi Urambo Mashariki akawashinda wapinzani wake na akateuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa Waziri wa Wizara ya Afrika Mashariki na baadaye alihamishiwa katika Wizara ya Uchukuzi na Mawasiliano.
Aliwania nafasi ya Spika bila mafanikio. Mwaka 2014, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba aliloliongoza hadi kupatikana kwa rasimu ya Katiba Pendekezwa ya Bunge.

Share this article :

0 Maoni:

 
Maganga One Blog © Copyright 2017. All Rights Reserved.

Powered by Maganga One.
Back to TOP