MKUU wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema, ameunda timu ya watu wanne itakayofuatilia malipo ya fidia ya ardhi kwa ajili ya wananchi walioondolewa katika eneo la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam.
Timu hiyo imeundwa juzi wakati wa mkutano wa Mkuu huyo wa Wilaya na wananchi hao. Mjema amesema timu hiyo itahusika pia kufuatilia ulipwaji wa viwanja.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Mjema amesema ataunda timu nyingine ya watu sita itakayochunguza tuhuma zilizotolewa na wakazi hao dhidi ya maofisa waliodaiwa kuwa si waaminifu, wanaodaiwa kujilimbikizia viwanja na kuwagawia wasiostahili.
Mjema aliamua kuunda timu ya kufuatilia malipo hayo ya fidia baada ya maelezo ya Mhandisi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), William Shechambo mkutanoni hapo kutowaridhisha wananchi, kutokana na kutoonesha lini watalipwa fidia na kupewa viwanja.
“Nitaunda timu ya uchunguzi ya watu sita, yoyote atakayebainika kujinufaisha tutamchukulia hatua kwa mujibu wa sheria na timu hii itapaswa kunipa ripoti kabla ya Desemba 30, mwaka huu,” alisema.
Awali, wananchi hao waliwasilisha malalamiko yao mbele ya Mjema na maofisa wengine waliokuwepo kwenye mkutano huo ambao walidai kuwa hawafahamu hatma ya maeneo yao yaliyochukuliwa na TAA kwa ajili ya utanuzi wa kiwanja.
Wananchi hao kutoka katika mitaa ya Kipunguni, Kigilagila na Pugu Kinyamwezi walidai kuwa hawajalipwa fidia kama walivyoahidiwa na Serikali.
“Mkuu wa Wilaya tunaomba kupewa viwanja vyetu kwa kuwa tunapata shida sana, pia tumeingia kwenye mgogoro sisi kwa sisi,” alisema mmoja wa wananchi hao aitwaye Gaudensia Pascal aliyedai kuwa nyumba zake tatu zilibomolewa kupisha mradi wa upanuzi wa uwanja huo wa ndege na kwamba sasa ameingia kwenye mgogoro na wanaye akituhumiwa kuuza eneo la nyumba zao