Rais John Magufuli akimjulia hali mke wake, Mama Janeth Magufuli aliyelazwa wodi ya Sewa Haji katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, jijini Dar es Salaam jana. (Picha na Ikulu).
RAIS John Magufuli jana aliwatembelea na kuwajulia hali wagonjwa waliolazwa katika wodi ya Sewahaji iliyopo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam jana akiwemo mkewe, Mama Janeth Magufuli na Waziri na Balozi mstaafu wa Tanzania, Omar Ramadhan Mapuri.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, Rais Magufuli aliwatembelea wagonjwa hao mara baada ya kuwaongoza mamia ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam katika kuaga mwili wa aliyekuwa Waziri na Mbunge wa Mufindi Kaskazini, Joseph Mungai kwenye Viwanja vya Karimjee.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, baadhi ya wagonjwa waliolazwa katika wodi hiyo walimshukuru Rais Magufuli kwa hatua zilizochukuliwa na serikali kuboresha hospitali hiyo na wamebainisha kuwa licha ya kuboreshwa kwa mazingira ya hospitali pia wanapata huduma nzuri kutoka kwa madaktari na wauguzi.
Aidha, jana asubuhi, Rais Magufuli alikutana na kufanya mazungumzo na Mfadhili wa Taasisi ya Gatsby Tanzania, Lord Sir David Sansburg na kumhakikishia kuwa serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za kuendeleza kilimo, wajasiriamali na viwanda ambazo zinafanywa na taasisi hiyo.
Rais Magufuli alisema atafurahi kuona taasisi hiyo ambayo imekuwa ikiwasaidia wakulima wa pamba na chai kupata mbegu bora na kusindika mazao yao, inapiga hatua zaidi kwa kuanzisha viwanda vya nguo na kwamba serikali ipo tayari kuunga mkono juhudi hizo.