Mwanamke wa Marekani aliye na asili ya Kisomali ni mwanamke wa kwanza kushindana katika shindano la malkia wa urembo wa Minnesota akiwa amejifunika mwili wake wote.

Halima Aden alifuzu katika nusu fainali ya shindano hilo la malkia wa urembo wikendi iliopita akiwa amevalia hijab.
Pia alivalia nguo iliomfinika mwili wake wote kwa jina burkini wakati wa shindano la uogeleaji.
Gazeti la Minneapolis Star limeripoti kwamba nguo ya kuogelea aliyovaa bi Aden ilikuwa tofauti na zile za wenzake 44 wengi wao ambao walivalia bikini.
Kabla ya shindano hilo, mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 19 aliambia kituo cha habari cha Mineapolis kwamba shindano hilo la malkia wa urembo lilikuwa jukwaa zuri la kuuonyesha ulimwengu yeye ni nani.
Mapema mwezi huu mkimbizi mmoja mwenye asili ya Kisomali aliweka historia baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge wa kwanza wa Marekani mwenye asili ya Kisomali.
IIhan Omar mwenye umri wa miaka 34, ambaye huvalia hijab ,alichaguliwa kuhudumu katika bunge la jimbo la Minnesota .