KAMPENI ya kubomoa nyumba ili barabara zipite, imeitikiwa vyema na wananchi wa mitaa ya Sechelela na Amani iliyopo Manispaa ya Dodoma.
Mwitikio huo uliopokewa kwa maneno na vitendo, utawezesha nyumba takribani 70 zilizo katika maeneo ya barabara, kubomolewa na hivyo kupisha ujenzi wa barabara hizo.

Diwani wa Kata hiyo, Juma Mazengo (CCM) alisema, nyumba 70 zenye familia 2,000 zilizokuwa zimejengwa katika mitaa ya Sechelela na Amani, zimekubali kupisha ujenzi wa barabara ili wananchi wapate huduma za kijamii.
Mazengo alisema watu wote waliobomolewa nyumba zao, wametafutiwa maeneo mengine ili kupisha kutengeneza vizuri barabara hizo ili wakazi wa maeneo hayo waweze kupatiwa huduma zinazofanikishwa na uwapo wa barabara bila shida. Huduma hizo ni pamoja na magari ya zimamoto, wagonjwa na hata mabasi.
“Wakati mama akiwa mjamzito na gari inatakiwa iende hadi mlangoni ikamchukue huwa ni tatizo kubwa. Kwa hakika huduma za kijamii kufika katika maeneo haya ilikuwa ni ngumu, tulikaa vikao na kukubalina kubomoa hizi nyumba ili tuweze kupata barabara,” alisema Mazengo.
Idadi kubwa ya wanawake katika mitaa hiyo walipongeza hatua hiyo ambao walisema ni ukombozi kwa jamii kwani kukosekana kwa barabara ilikuwa ni mojawapo ya kero iliyowanyima raha hasa unapofika wakati wa kujifungua.
Wakizungumza na waandishi wa habari jana wakati wa kubomoa nyumba ili barabara zipite, kina mama hao walisema wamekuwa wakipa taabu wakati wa kujifungua kutokana na gari kushindwa kuingia katika maeneo wanayoishi.
Mmoja wa wanawake hao, Amina Issa alisema wakati akiwa na mimba ya mtoto wa pili, ilikuwa hekaheka kutokana na gari kushindwa kuingia katika eneo hilo, hali ambayo ilimlazimu mume wake kumbeba mpaka katika barabara kuu ili kupata usafiri.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Sechelela, Norbat Pangasero alisema wametumia elimu zaidi kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kupata huduma za kijamii ili wapate maendeleo.