Balozi Tuvako Manongi (kushoto) akizungumza na Rais wa Mahakama ya ICC, Jaji Slivia Fernandez de Gumendi.
RAIS wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC), Jaji Slivia Fernandez de Gumendi, amekutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi.
Katika mazungumzo hayo ya Jaji Gumendi na Balozi Manongi, Rais wa ICC aliishukuru Tanzania kwa hotuba yake iliyotolewa na Balozi siku ya Jumatatu wakati Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, lilipopokea na kujadili Ripoti ya ICC.

Kwa mujibu wa Gumendi, hotuba hiyo ya Tanzania ilikuwa yenye uwiano (balanced) na pia ilitoa ushauri au mapendekezo ya namna gani Mahakama hiyo, inavyoweza kuboresha uhusiano na wanachama wake kwa mujibu wa Mkataba wa Roma.
“Nilikusikiliza kwa makini sana wakati ulipokuwa unatoa hotuba yako, nilinukuu kila hoja ulizokuwa unazizungumza. Hotuba ya Tanzania ilikuwa yenye uwiano (balanced) na ningependa kuitumia fursa hii kuishukuru Tanzania kwa hilo,” alisema.
Rais huyo wa ICC alikiri kwamba anadhani ni wakati muafaka kwa wadau wa pande mbili, kukaa na kuzungumza kama ambayo Tanzania na wanachama wengine wameshauri, hasa kutokana na kile alichosema kwamba kila nchi imekuwa na tafsri tofauti na uelewa tofauti kuhusu baadhi ya vipengele (articles), vinavyohusu Mkataba wa Roma unaounda Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai.
Kwa upande wake, Balozi Manongi alisema ushauri na mapendekezo ambayo yametolewa na Tanzania pamoja na nchi nyingine, hayalengi katika kutaka kubadili Mkataba wa Roma au kuipunguzia nguvu ya kiutendaji mahakama hiyo.
“Tungependa sana ieleweke kwamba tunaposhauri kukaa na kuzungumza, kusitafsiriwe kana kwamba tunataka kupunguza nguvu ya utendaji wa chombo hiki, ambacho wote tunaamini kwamba kinastahili kuwapo. Tunachosema na kusisitiza ni kwamba kila upande una hoja za msingi, basi tuzijadili kwa kuzungumza,” alisisitiza Balozi Manongi.
Rais huyo wa ICC na Balozi Manongi, walibadilishana mawazo juu na masuala mbalimbali kuhusu utendaji kazi wa Mahakama ya ICC, ikiwa ni pamoja na kuangalia ni maeneo gani ambayo Mahakama na wanachama wake wanaweza kujadiliana.