Rais mteule wa Marekani Donald Trump amesema wafungwa zaidi hawafai kuachiliwa kutoka kwa gereza la Marekani la Guantanamo Bay, Cuba.
Amesema wafungwa waliosalia gerezani humo ni "watu hatari sana na hawafai kuruhusiwa kurejea kwenye uwanja wa mapigano tena".
Rais Barack Obama alikuwa ameapa kuwa angefunga jela hiyo kabla ya kuondoka madarakani na amewahamisha wengi wa wafungwa waliokuwa wakizuiliwa humo.
Kwa sasa, wafungwa 60 wamesalia gerezani na ikulu ya White House ilisema baadaye Jumanne kwamba inapanga kuwahamisha wafungwa hao kabla ya tarehe 20 Januari.
Bw Trump alikuwa amepinga mpango wa Obama wa kufunga jela hiyo wakati wa kampeni.
Mwezi Februari alisema: "Asubuhi hii, nimemtazama Rais Obama akiongea kuhusu Gitmo, sawa, Guantanamo Bay, ambayo kusema kweli, ambayo kusema kweli, hatutaifunga.
"Tuaicha iendelee kutumika... na tutawarundika watu wale wabaya huko, niamini mimi, tutawaweka watu wengi huko."

Tweet

Mnamo 17 Desemba, vyombo vya habari Marekani viliripoti kwamba Pentagon inapanga kuwahamisha wafungwa wengine 17 siku chache zijazo.
Bw Obama ameidhinisha kuhamishwa kwa wafungwa lakini Bunge la Congress ambalo linadhibitiwa na chama cha Republican limewekwa masharti mengi.
Bunge hilo linaitaka wizara ya ulinzi kutoa taarifa kuthibitisha viwango vya kiusalama vimetimishwa angalau siku 30 kabla ya hatua kama hiyo kuchukuliwa.
Nchi kadha zimewapokea wafungwa wa zamani wa Guantanamo, zikiwemo Ghana, Senegal, Umoja wa Milki za Kiarabu (UAE), Uganda na Cape Verde.
Watu 780 walizuiliwa Guantano tangu 2002, lakini kwa sasa ni 105 pekee waliosalia gerezani. Hamsini kati ya hao wameidhinishwa kuachiliwa huru.
Jela hilo ilijengwa na Marekani baada ya mashambulio ya tarehe 11 Septemba mwaka 2001 na hutumiwa na Washington kuwazuilia "wapiganaji maadui".
Gereza hilo hugharimu Marekani $445m (£316m) kila mwaka.
Ramani ya Guantanamo Bay