MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe Stephen Kebwe ameomba serikali ifute sheria inayoruhusu watu kutembea na silaha kama vile sime, panga, mkuki au mshale mkoani humo.
Amesema hatua hiyo itapunguza vifo na majeruhi katika migogoro ya wakulima na wafugaji mkoani humo.

Ametoa ombi hilo kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba katika mikutano ya hadhara ya wananchi wa vijiji vya Tindiga na Dumila.
Nchemba amesema kuanzia jana ikitokea mkulima ama mtu yeyote akijeruhiwa kwa sime, panga, mkuki au mshale mkoani Morogoro, serikali itafuta sheria inayoruhusu watu kutembea na silaha.
Amesema hatua hiyo inatokana na ombi la Mkuu wa Mkoa, Dk Kebwe la kufuta au kurekebisha sheria hiyo ili kupunguza vifo na majeruhi katika migogoro ya wakulima na wafugaji.
Waziri huyo ameunda tume itakayokuwa na jukumu la kuwaorodhesha viongozi wa serikali wilayani Kilosa mkoani Morogoro, wanaodaiwa kwenda kinyume na sheria ya utendaji kazi.
Majina yao yatawasilishwa ofisini kwake kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kisheria.
Ametoa kauli hizo kwa nyakati tofauti wilayani Kilosa jana, alipozungumza na viongozi wa Serikali ya wilaya hiyo na mkoa, wakiongozwa na Dk Kebwe.
Aliwaambia wafugaji na wakulima kuwa hakuna sababu yoyote ile, itakayosababisha mtu kuchukua hatua za kumuua binadamu mwezie, kwani uhai haulinganishwi na thamani ya kitu chochote kile.
Amewaonya viongozi wa ngazi mbalimbali, kuacha urafiki na wauaji. Alisisitiza kiongozi yoyote atakayebainika kuwa na ushirikiano na muuaji, basi na yeye ataunganishwa kwenye kesi ya mauaji .
Waziri Nchemba alivitaka vyombo vya dola na vya kisheria, kutosubiri wananchi wachukue sheria mkononi, bali wachukue sheria na adhabu inayostahiki wote wenye kutenda makosa ili kuhakikisha vitendo hivyo vinakomeshwa mara moja.
“Duniani kote sheria isipochukua mkondo wake kwa wahalifu, basi wananchi watachukua sheria mkononi“ alisema.
Aliwataka wafugaji kukutana na kujadili wao wenyewe namna ya kuacha tabia hizo.
Amesema kwa yule atakayefanya mauaji au kujeruhi, basi wafugaji wenzake wawe wa kwanza kumkamata na kufikisha kwenye vyombo vya sheria.
Amewaonya wakulima kuwa atakayechukua hatua za kumuua mfugaji kwa sababu ya kulisha shamba, basi naye atafikishwa mahakamani na kupewa adhabu kali.
Amewataka wakulima kutolipiza visasi kwa yote yaliyotokea, kwani watuhimiwa wote wameshakamatwa na kufikishwa mahakamani na watakuwa mfano kwa wengine .
“Nimesikia kuwa wafugaji wanafanya mauaji kwa makusudi kutokana na viburi vyao kwa kigezo watauza mifugo yao ili washinde kesi, kama wamezoea hivyo, basi watafilisika na mifugo yao na jela watakwenda “ alisema.
Dk Kebwe alisema pamoja na wafugaji wengi kutembea na silaha, chanzo kingine cha migogoro ya wakulima na wafugaji ndani ya wilaya na mkoa huo ni viongozi wa ngazi za vijiji, kupokea rushwa na kuwakaribisha wafugaji maeneo ya vijiji vya wakulima kinyume cha sheria.
“Nimeanza kuchukua hatua za kuwachunguza viongozi wote wa vijiji na kata zenye migogoro na watakaobainika kuhusika na vitendo vya kinyume cha sheria, watawajibishwa mara moja,” alisema Dk Kebwe.
Waziri aliwaonya wananchi wenye tabia ya kutaka fedha kwa njia haramu, kwa kushikilia mifugo ya wafugaji.
Alisema kuna watu wamekuwa wakishikilia mifugo ya wafugaji bila kosa lolote ili tu wapate fedha. Alitaka vitendo hivyo, vikomeshwe mara moja.
“Tukio kama hili si migogoro ya ardhi, bali ni ujambazi sawa na uhalifu mwingine , na watu wa aina hii washughulikiwe kisheria ili kukomesha tabia hizo” alisema Nchemba.
Waziri Nchemba alitembelea vijiji vya Tindiga na Dumila wilayani Kilosa kwa lengo la kutatua changamoto za migogoro ya wakulima na wafugaji.