RAIS John Magufuli amefanya ziara ya kushtukiza katika Shule ya Msingi Chato alikosoma darasa la kwanza hadi la saba na kuzungumza na walimu na wanafunzi wa shule hiyo, huku akitaka wahakikishe hakuna wanafunzi hewa katika shule hiyo.
Magufuli pia ameahidi kujenga madarasa matatu na ofisi moja ya walimu katika shule hiyo, kufuatia ombi la walimu kuwa shule hiyo inakabiliwa na uhaba wa vyumba vya madarasa ikilinganishwa na idadi ya wanafunzi wanaosoma shuleni hapo.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu jana, ilieleza kuwa Rais alifanya ziara ya kushtukiza shuleni hapo.
Akizungumza na wanafunzi shuleni hapo, Magufuli aliwaasa kutilia mkazo masomo ili waweze kufaulu na kuwataka walimu kuhakikisha wanatumia vyema fedha zinazotolewa na serikali kila mwezi za elimu bila malipo na pasiwe na wanafunzi hewa.
Rais alisema yapo maeneo na shule mbalimbali nchini kumebainika kuwa na wanafunzi hewa katika uhakiki unaofanywa na serikali na kuwaasa shule hiyo kuwa wasiwe kama shule hizo.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Chato, Mwita Chacha alimshukuru Rais Magufuli kwa msaada aliowapatia katika kukabiliana na uhaba wa madarasa uliokuwa unaikumba shule hiyo, pia kuitembelea shule yao jambo ambalo limewatia moyo walimu na wanafunzi shuleni hapo.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli pia ametembelea eneo la stendi ya zamani na kuzungumza na baadhi ya wananchi waliokuwepo eneo hilo na kutoa msaada kwa kikundi cha wasafisha viatu ili kuongeza mtaji wa biashara yao.