Mahakama kuu nchini Gambia itasikiliza ombi la rais Yahya Jammeh dhidi ya matokeo ya uchaguzi wa urais uliofanyika mwezi jana.
Matokeo ya uchaguzi huo yalimpa ushindi Adama Barrow kwa asilimia 43 ya kura, kwa mujibu wa tume ya uchaguzi ya nchi hiyo.

Lakini Jammeh anataka mahakimu wapitishe kwamba Adama Barrow hakuchaguliwa kutokana na mapungufu yaliyokuwepo wakati wa upigaji kura.
Nyuma ya milango ya mahakama kuu, mahakimu wake wanapaswa kumsikiliza rais Yahya Jammeh akipinga matokeo ya uchaguzi, lakini kunaweza kuwa na watu wachache.
Baadhi ya mahakimu wa kigeni wameamua kutokwenda Banjul, akiwemo Nicholas Browne-Marke wa Sierra Leone ambae amesema yuko Israel.
Lakini sio mahakimu wa mahakama kuu pekee ambao hawatakuwepo, waziri wa habari wa Gambia pia inasemekana ameondoka nchini humo.
Bado haijajulikana hali itakavyokuwa siku ya leo.
Yahya Jammeh ambae mwanzoni alikubali kushindwa katika uchaguzi wa urais wa mwezi jana, ghafla alibadili msimamo na kutaka uchaguzi huo ubatilishwe, kwa madai kuna makosa yaliyofanywa na tume ya uchaguzi.
Wakati huo huo, Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika magharibi ECOWAS inajaribu kutafuta suluhu ya kidiplomasia ili kuepusha vurugu na machafuko ambayo yanaweza kuenea nchi nzima.
Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari, ambae ametajwa kama ndio msuluhishi, ataelekea Banjul kesho na Ellen Johnson Sirleaf wa Liberia pamoja na aliyekuwa rais wa Ghana John Dramani Mahama.
Hii inaweza kuwa ndio safari ya mwisho ya kujaribu kumshawishi Jammeh kuachia madaraka na kumpisha rais mteule Adama Barrow.
Sherehe za kuapishwa kwa rais mpya zimepangwa kufanyika siku ya Alhamisi, tarehe 19 mwezi huu.