SERIKALI imeombwa kuangalia uwezekano wa kuongeza viwango vya pensheni kwa wastaafu wa utumishi wa umma ili waweze kukabiliana na kupanda kwa gharama za maisha.
Ombi hilo lilmetolewa leo jijini Mwanza na baadhi ya wastaafu wa utumishi wa umma wakati wa uhakiki wa taarifa zao uliofanywa na wataalamu kutoka Wizara ya Fedha na Uchumi walioko jijini Mwanza kwa kazi hiyo.

Mstaafu Sabato Mkama, aliyekuwa askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) aliyestaafu mwaka 2009, amesema pensheni anayolipwa baada ya kustaafu kwa sasa ni ndogo na haitoshelezi mahitaji yake, familia na kusomesha watoto.
"Kiwango cha fedha ya kustaafu ninacholipwa kwa sasa cha Sh 124,000 kwa mwezi ni kidogo, ikilinganishwa na kazi kubwa tuliyoifanyia nchi hii, tumepigana vita ya Uganda mwaka 1978 na baadhi ya nchi nyingine katika Bara la Afrika, wenzangu wengine walipoteza maisha na wengine wamepata ulemavu wa kudumu, naomba serikali ifikirie uwezekano wa kuongeza kiwango cha pensheni maisha ni magumu," alifafanua.
dalawa Bugarika, aliyekuwa Ofisa Usalama wa Viwanja vya Ndege, aliyestaafu mwaka 2000, ameipongeza serikali kwa uamuzi wake wa kufanya uhakiki wa wastaafu wanaolipwa pensheni na Wizara ya Fedha na Mipango.
"Naipongeza serikali, uhakiki huu ni muhimu, naomba liwe endelevu, kila baada ya miaka miwili uhakiki kwa wastaafu ufanyike, alisema Bugarika. Mkazi wa Mahina na askari mstaafu wa Jeshi la Polisi, Tabu Denis, aliyestaafu utumishi wa umma mwaka 2000, ameipongeza serikali kwa kuamua kufanya uhakiki ili kuweka kumbukumbu sawa za watu waliolitumikia taifa.
"Wastaafu sasa watapata ukweli wa taarifa zao baada ya kustaafu utumishi wa umma," alisema na kuwataka wahusika kuangalia taarifa za viwango ya mishahara ambayo hailingani na muda wa utumishi kwa mtumishi aliyestaafu kujua stahiki ya malipo yake ya kustaafu.
Mkaguzi Mkuu wa Serikali Msaidizi kutoka Wizara ya Fedha, Stanslaus Mpembe alisema kuwa lengo la uhakiki huo ni kuiwezesha wizara kuhuisha taarifa za wastaafu ili kupata kanzi data iliyo sahihi, kuwatambua wastaafu na kuiwezesha kulipa wastaafu wanaostahili.
Alisema uhakiki huo ulianza Oktoba 10, mwaka jana katika mkoa wa Pwani na kuendelea katika mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe, Ruvuma, Songwe, Katavi, Rukwa, Morogoro, Dodoma, Singida, Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga.
"Mpaka kufikia leo, tayari uhakiki umefanyika katika mikoa 13 ya Tanzania Bara, na kuanzia leo (jana), uhakiki unafanyika katika mikoa ya Mwanza, Kagera, Mara, Shinyanga, Simiyu na Geita, kazi ya uhakiki inafanyika katika ofisi za halmashauri za wilaya kwenye mikoa hiyo na wastaafu watatakiwa kufika katika halmashauri husika kwa ajili ya kuhakikiwa," alifafanua Mpembe.
Alibainisha kuwa wastaafu wanaohusika wanatakiwa kufika wenyewe na si kuwatuma wawakilishi kwenye vituo vya uhakiki.
Alisema wanapaswa kuwa na nyaraka muhimu ikiwemo barua ya tuzo la kustaafu, barua ya kustaafu au kupunguzwa kazini, nakala ya hati ya malipo ya kiinua mgongo au mkupuo.
Nyaraka nyingine muhimu ni barua ya kwanza ya ajira, kitambulisho cha pensheni, barua ya kuthibitishwa kazini, kadi ya benki na picha mbili za passport size zilizopigwa hivi karibuni.
Alisema kuwa wastaafu ambao hawana nyaraka kutokana na sababu mbalimbali wanashauriwa kufika katika Ofisi za Hazina ndogo zilizopo kila mkoa ili waweze kutambuliwa.
Kwa wastaafu ambao ni wazee na wagonjwa, alisema wao watakuwa wanahakikiwa mwisho mwa uhakiki ili kutoa nafasi pana ya kuwahudumia.
Akijibu, Mpembe alisema suala hilo la kuomba nyongeza atalifikisha wizarani lifanyiwe kazi.