Aidha Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ametoa rai kwa wataalamu wa ardhi kusoma alama za nyakati kwa kugawa viwanja bila kuangalia uwezo wa kifedha na endapo ikibainika vinatolewa kwa wenye fedha pekee watapokonywa.
Gambo ameyasema hayo leo wilayani Karatu wakati alipokuwa akisikiliza kero za wazee na viongozi wa dini.

Amesema lazima wataalamu wa ardhi kwenda kutatua migogoro badala ya kuitumia kujinufaisha huku mwananchi wa hali ya chini akiwa hajui anaanzia wapi kupata kiwanja au kutatuliwa mgogoro.
Gambo amesema, ni vyema wataalamu wa ardhi kusoma alama za nyakati na kuendana na kasi ya Rais John Magufuli kwa kuwajali wanyonge ambao wanahitaji kutatuliwa migogoro yao lakini wamekuwa wakidhulumiwa ardhi zao na watu wenye uwezo.
“Hivi sasa Mkoa wa Arusha umejipanga kuhakikisha hadi ifikapo Desemba mwaka huu, kusiwe na migogoro yoyote ya ardhi badala yake wananchi wapate fursa za kimaendeleo na kuinua uchumi wa mkoa pamoja na wilaya za mkoa huu," amesema.
Kaimu Ofisa Ardhi na Maliasili Wilaya ya Karatu, Faraji Rushagama amekiri kuwa malalamiko ya wananchi kupewa viwanja ni mengi na kukiri ni kweli kuna changamoto za ugawaji wa ardhi.
Amesema hivi sasa atatumia mfumo unaotekelezwa na Tasaf kwa ajili ya kuwapata wananchi wenye mahitaji ya ardhi ambao ni maskini na si matajiri.
Akizungumza kuhusu maeneo ya watu kutopimwa, alisema halmashauri ya wilaya hiyo inajitahidi kupima maeneo ya miji yanayokuwa ili yaweze kuwa na ramani inayoeleweka na yale yasiyoendelezwa kupangwa kisasa ili kuweka mji katika hali ya ubora na hatimaye wananchi waweze kupata mikopo kwenye benki na taasisi za fedha kwa ajili ya kuleta maendeleo.