Wakulima wadogo nchini Tanzania hivi karibuni wataweza kupata taarifa mbalimbali za kijiditali kuhusu masuala ya pembejeo, ukiwemo ushauri utakaosaidia kutatua matatizo yanayowakabili kama vile upatikanaji wa fedha, pembejeo na mafunzo. Mradi huo umezinduliwa na taasisi tatu za Alliance for a Green Revolution in Africa (AGRA), Positive International Limited (PIL), na Grameen Foundation katika sherehe zilizohudhuriwa na maofisa wa serikali, wawakilishi wa vyama vya wakulima, taasisi za fedha, kampuni za mbegu, wafanyabiashara wa nyenzo za kilimo na wale wanaojishughulisha na biashara za mazao ya sekta ya kilimo. Kifaa hicho cha dijitali kitawawezesha wakulima kulipia mapema pembejeo wanazohitaji kupitia simu za mkononi kwa bei nafuu. Pia kifaa hicho kitawapa wakulima pembejeo kulingana na mazao na malengo yao ya uzalishaji na pia kupata taarifa za ushauri kuhusu matumizi bora ya pembejeo hizo. “Moja ya changamoto kubwa zinazowakabili wakulima ni kwamba hukosa fedha mwanzoni mwa msimu wa upandaji mazao, jambo ambalo huwalazimisha kutafuta fedha hizo kwa ajili ya ununuzi wa pembejeo na hivyo kuwaongezea mzigo,” alisema Hedwig Siewertsen, kiongozi anayeshughulikia masuala ya fedha wa shirika la Alliance for a Green Revolution in Africa (AGRA). “Kifaa hicho cha dijitali kwa ajili kusaidia upatikanaji pembejeo za kilimo ni ufumbuzi wa kipekee. Kitawaimarisha na kuwasaidia wakulima kutenga fedha kwenye akaunti zao za simu ili waweze kununua pembejeo bora kwa muda muafaka na kwa bei nafuu ya asilimia 30.” Wakulima wadogo nchini Tanzania huzalisha asimia 70 ya chakula ingawa karibu nusu yao hawazalishi chakula cha kutosha kwa ajili ya mauzo. Wanakabiliwa na ukosefu wa teknolojia ya kilimo cha kisasa, hawana uwezo wa kujipatia pembejeo bora na wanakosa huduma za kiufundi za ughani zinazoweza kuwasidia kukuza kilimo pamoja na ukosefu wa mafunzo. [caption id="attachment_2253" align="aligncenter" width="1404"] Mwakilishi wa AGRA nchini, Bw. Vianey Rweyendela akifafanua jambo wakati wa uzinduzi huo.[/caption] Badala yake wakulima hawa wanategemea zaidi kilimo cha mvua, zana duni za kilimo na mbegu hafifu ambazo ubora wake hupungua kila msimu wa kilimo. Isitoshe, wakulima wanaotaka kuwekeza katika kilimo cha kisasa wanashindwa kupata mikopo kwenye taasisi za fedha kwa vile ni asilimia 6 tu ya mikopo ya benki ndio imetengwa kusaidia sekta ya kilimo. Wakulima wanatumia fedha zao chache kununua pembejeo za kilimo kutoka kwa walanguzi; pembejeo ambazo mara nyingi hazina uthibitisho wa ubora. Wakati huo huo, wafanyabiashara wa pembejeo za kilimo wa sekta binafsi wamegundua kwamba usambazaji wa huduma bora maeneo ya vijijini una faida ndogo kutokana na gharama kubwa za kufanya biashara hiyo, uwezo mdogo wa kifedha kwa upande wa wakulima na umaskini uliokithiri miongoni mwa wananchi wengi vijijini. Matokeo yake ni kwamba wastani wa uzalishaji wa mazao mengi kwa hekta unakadiriwa kuwa ni tani 1.7 na kwamba mavuno ya mazao muhimu ya chakula kama vile mahindi yamekuwa yakipungua kwa sababu ya uharibifu wa ardhi na hali mbaya ya hewa. Jinsi ya kupeleka kifaa cha dijitali kwa wakulima Kifaa cha dijitali kitakuwa na mpango mahsusi wa mazao utakaowawezesha wakulima kupata pembejeo kwa kuzingatia malengo yao ya uzalishaji. Pia, kupitia simu za mkononi, kitawezesha upatikanaji wa huduma za ughani kwa njia ya ujumbe (SMS) kuwaelimisha wakulima matumizi ya pembejeo. AGRA, shirika linaloongozwa na Waafrika wenye weledi wa kuwasaidia wakulima wadogo barani Afrika, ndilo linalogharimia ukuzaji wa kifaa hicho cha dijitali kupitia ufadhili wa MasterCard Foundation. Taasisi ya Grameen Foundation, ambayo ni taasisi inayojitegemea inayotumia teknolojia ya dijitali kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya umaskini, ndio inasisimia ukuzaji wa chombo hicho cha dijitali. Kifaa hicho pamoja na huduma zake kitatolewa na kampuni ya pembejeo za kilimo ya Positive International Limited, ambayo nembo yake ya kibiashara ya Snow Brand imesaidia sana kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayowakabili wakulima nchini Tanzania. Mfumo huo wa ununuzi wa pembejeo utazingatia uwepo wa huduma za fedha za simu za mkononi zinazokua kwa kasi nchini Tanzania. [caption id="attachment_2254" align="aligncenter" width="1404"] Uzinduzi ukifanywa na Mkuu wa AGRA nchini Bw. Vianey Rweyendela (wa pili kulia) kwa kushirikiana na wawakilishi wa Positive International Limited (PIL), na Grameen Foundation.[/caption] Mradi huo utatekelezwa kwa kipindi cha miezi kumi na nane, ikiwemo awamu ya miezi sita ya utafiti na maendeleo, na miezi kumi na mbili ya awamu ya majaribio ya kifaa hicho cha dijitali. Majaribio yataanza na wateja 15 wa kampuni ya Positive International na wakulima wadogo 15,000 wa mikoa ya Arusha na Mbeya. Mazao yatakayohusika katika mradi huo ni mahindi na maharage, ambayo ni muhimu sana katika maeneo hayo. Kwa mfano, mkoani Arusha – moja ya maeneo yanayohusika katika mradi – mazao hayo mawili hulimwa katika eneo la hekta 150,000 ingawa kuna pengo la mavuno la asimilia 213 kwa upande wa mahindi na asilimia 152 kwa upande wa maharage. Matumizi ya pembejeo bora ndio njia pekee itakayosaidia kuongeza mavuno kwa asilimia 150 ili kutosheleza mahitaji ya chakula katika ngazi ya kaya na pia kukuza mapato. Mkurugenzi Mtendaji wa Positive International, Karan Kapoor, anasema soko la matumizi ya kifaa cha dijitali kwa mauzo ya pembejeo za kilimo nchini Tanzania ni kubwa. “Mamilioni ya wakulima wadogo Tanzania wanahitaji upatikanaji wa pembejeo bora za kilimo kwa bei nafuu. Tutaanza matumizi ya kifaa hiki cha dijitali kwa kuwahusisha wafanyabiashara 15 kwa kipindi cha miezi 18 ijayo. Lengo litakuwa kuwafikia wakulima 15,000 ili kuthibitisha matumizi endelevu ya kifaa hicho.” “Baada ya hapo, tumepanga kupanua matumizi yake ili kuwafikia wafanyabiashara 500 nchini bila ya kuwepo miundombinu mpya.” “Watanzania milioni 19 wanaishi kwa kutegemea mashamba madogo ingawa mtu mmoja kati ya watu 25 hupata huduma ya umeme na watu wengi hawana maji safi na salama majumbani mwao,” anasema Raphael Wolf, Meneja Mradi wa Grameen Foundation. “Kifaa hiki kitaleta mapinduzi makubwa ya dijitali mashambani. Kwa mara ya kwanza, wakulima wengi wataweza kupata raslimali wanazohitaji kuongeza uzalishaji na mapato yao.” Jinsi wakulima wanavyopata pembejeo muhimu za kilimo kama vile mbolea na kuongeza mavuno yao, shirika la AGRA litapata fursa ya kutumia uwepo wa ubia wake na vitega uchumi vilivyopo Tanzania kuwaunganisha wakulima na masoko kupitia ushirikiano na wanunuzi wa kimataifa, wawezeshaji wa biashara na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yanayoshughulika na upatikanaji wa masoko. Mradi huu ukifanikiwa Tanzania, washirika wake wanakusudia kutumia uwezo wao wa pamoja kuanzisha dhana hii na kifaa hicho cha dijitali katika nchi nyingine za Afrika, ukiwemo mtandao wa wafanyabiashara za kilimo katika nchi za Malawi, Msumbiji, Zambia na nchi nyingine katika bara hili.
0 Comments