Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) ambao hutumiwa na Marekani kutoa misaada kwa nchi za nje, limesitisha ufadhili wake kwa miradi ya afya nchini Kenya.
Taarifa kutoka kwa shirika hilo imesema hatua ya kusitisha ufadhili kwa miradi yote ya Wizara ya Afya ya Kenya imetokana na hatua ya Kenya kutotimiza "masharti ambayo hayajaelezwa".
Maafisa wa USAID wameagizwa kutojishughulisha na "shughuli zozote za kibiashara" na taasisi za serikali ya Kenya pamoja na mashirika mengine yenye uhusiano na serikali.
Hatua hiyo ya Marekani inatarajiwa kuathiri miradi mbalimbali ya serikali ikiwemo mipango ya kukabiliana na malaria, kifua kikuu na Ukimwi pamoja na miradi ya uzazi wa mpango, huduma za afya kwa wajawazito na watoto.
Kwa miezi kadha sasa, wizara ya afya nchini Kenya imekubwa na tuhuma za ulaji rushwa.
Sekta ya afya Kenya pia ilitatizwa na mgomo wa taifa madaktari ambao ulidumu kwa siku 100 kuanzia Desemba.
Mwaka uliopita, mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali alisema jumla ya dola 50 milioni hazikubainika zilivyotumiwa katika wizara ya afya.
Maafisa wakuu katika wizara ya afya pamoja na jamaa za baadhi ya viongozi wakuu serikalini walidaiwa kuhusika katika kufujwa kwa pesa hizo.
Wizara ya afya hata hivyo ilijitetea na kusema madai hayo yalikuwa kwenye ripoti ambayo ilifichuliwa mapema kabla ya wahasibu wa wizara hiyo kujibu maswali yaliyokuwa yameibuliwa na mkaguzi huyo kuhusu matumizi ya pesa hizo.
Mwandishi wa BBC Abdinoor Aden anasema hatua ya sasa hivi ya serikali ya Marekani itaibua maswali zaidi kuhusu usimamizi wa fedha katika Wizara ya Afya Kenya licha ya hatua ya rais Kenyatta ya kumhamisha Katibu Mkuu wa wizara hiyo.
Hatua ya USAID inatarajiwa kuathiri sana miradi ya serikali pamoja na miradi ya mashirika mengine ya afya ambayo hutumiwa an USAID kutoa huduma maeneo mbalimbali Kenya
|
0 Comments