Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho akiwa na Mkurugenzi wa World Economic Forum kanda ya Afrika kwenye mkutano huo unaofanyika Durban, Afrika Kusini. Kabla ya hapo Bi kanza alikuwa mshauri wa Uchumi wa Rais Mstaafu Kikwete wakati wa uongozi wa awamu ya nne.
Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ameshiriki Mkutano wa World Economic Forum for Africa unaofanyika Durban, Afrika Kusini. Mkutano huo muhimu unaokutanisha wafanyabiashara, wanasiasa na viongozi wa kiserikali unalengo la kutoa fursa kwa wadau wa maendeleo barani Africa kukutana na kujadili mustakhabali wa maendeleo na uwekezaji barani Afrika.
Katika Mkutano huo, Mheshimiwa Rais Mstaafu aliwakilisha Kamisheni ya Kimataifa ya Elimu (The Education Commission) ambapo alikutana na wadau wa elimu na vyombo vya habari kuelezea Mpango wa Kizazi cha Elimu barani Afrika.
Rais Mstaafu pia alipewa heshima ya kuhutubia hafla ya chakula cha jioni kutathmini mafanikio ya mpango wa Kilimo wa Grow Africa ambao chimbuko lake ni Mkutano wa WEF Africa uliofanyika Tanzania Mei, 2010 na Mpango wa Uwekezaji wa Kilimo wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT).
Katika hotuba yake, Rais Mstaafu alisisitiza umuhimu wa kuendelea kuchochea ushiriki wa Sekta Binafsi na uwekezaji katika Kilimo barani Afrika. Alitoa angalizo kuwa mafanikio ya mapinduzi ya kilimo hayawezi kufanikiwa kwa kuondoa wakulima wadogo bali kuwaongezea tija. Alitoa rai kwa viongozi wa Afrika kuhakikisha kuwa kilimo cha Wakulima wakubwa kinashamirisha na kustawisha kilimo cha wakulima wadogo na kuwa ni vitu vinavyoweza kwenda pamoja.
Akiwa Durban, Rais Mstafu amehudhuria pia amefanya mazungumzo na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini na Profesa Klaus Shwab ambaye ni Mtendaji Mkuu wa World Economic Forum. |
0 Comments