Maelfu ya watu wameandamana katika mji mkuu wa Ubelgiji, Brussels, baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kuwasili katika mkutano wa viongozi wa Ulaya na NATO.

Waandamanaji hao walikuwa wamebeba mabango ambayo baadhi yalikuwa yakisomeka ''Hatumkaribishi Trump''.
Wakati wa kampeni za Urais nchini mwake, Rais Trump aliwakasirisha Wabelgiji wengi kutokana na kuielezea kwake Brussels kama Jahanam.
Awali Rais huyo wa Marekani alikutana na mwenyeji wake mfalme Philippe wa Ubelgiji na malkia Mathilde.
Aliwasili mjini humo akitokea Roma Italia, ambako alikutana na kiongozi wa Kanisa katoliki duniani Papa Francis.